Habari za Punde

Mhe. Tabia akaguwa Daftari Wilaya ya Kusini.

Makarani  wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wakimsajili, Bi Khadija Mussa Fumu katika Daftari la kudumu la Wapiga kura katika Kituo cha Skuli ya Charity Bwejuu Wilaya ya Kusini.

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe.Tabia Maulid Mwita akihamasisha Vijana kuenda kujiandikisha katika Daftari la kudumu la Wapiga kura, linaloendelea katika Wilaya ya kusini.

Muangalizi wa Daftari la kudumu la Wapiga kura ambae pia ni  Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita ameridhishwa na idadi ya Wananchi kujitokeza kwa wingi katika Daftari la kudumu la Wapiga kura.

Ameyasema hayo huko Skuli ya Bwejuu wakati wa zoezi la Uandikishaji wa Daftari la kudumu la Wapiga kura, linaloendelea katika Wilaya ya Kusini.


Amewapongeza Wananchi kwa kupata hamasa na kujitokeza kwa wingi katika Daftari hilo, jambo ambalo litawawezesha kupata haki yao ya msingi ya kuchaguwa na kuchaguliwa.


Amewataka Wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu ili Viongozi waweze kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.


''Yanapotokea machafuko tunaoathirika zaidi ni sisi akina mama na Watoto wetu hivyo tujitahidi kuitunza Tunu yetu iliopo'' alisema Mhe. Tabia.


Hata hivyo amesema Watu wenye mahitaji maalum ni sawa na watu wengine hivyo wanahitaji kuandikishwa ili kupata haki yao ya Kidemokrasia.


Nae Katibu wa Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo  wa Chama cha Mapinduzi  Wadi  ya  Bwejuu Bw. Wajihi Simai Khatib amesema Watu wenye mahitaji maalum, Wazee na wasiojiweza wamepewa kipaombele ili kuwaondoshea usumbufu, unaoweza kujitokeza.

 

Nao Makarani wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) wamesema zoezi hilo, limeendelea vizuri kutokana na Uhamasishaji mkubwa uliofanywa na Viongozi mbalimbali ikiwemo Masheha na Vyama vya Siasa.


Zoezi la Undikishaji wa Daftari la kudumu la Wapiga kura katika Wilaya ya Kusini, limeanza tarehe 11.03.2025 na linatarajiwa kukamilika tarehe 13 mwezi huu.


Imetolewa na Kitengo Cha Habari,


WHVUM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.