KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mngereza Mzee
Miraji ameitaka kada ya uuguzi kuongeza weledi, nidhamu na uadilifu katika
utoaji wa huduma za afya, akisema kuwa Serikali inategemea mchango mkubwa
kutoka kwa wauguzi watarajali waliohitimu mafunzo yao.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mngereza Mzee Miraji ameitaka kada ya uuguzi kuongeza weledi, nidhamu na uadilifu katika utoaji wa huduma za afya, akisema kuwa Serikali inategemea mchango mkubwa kutoka kwa wauguzi watarajali waliohitimu mafunzo yao.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wauguzi waliomaliza mafunzo ya utarajali Tanzania bara na viongozi wa Wizara ya Afya kilichofanyika ofisi za wizara hiyo Mngereza alisema kuwa Serikali inaendeleza mkakati wa kuimarisha huduma kwa wananchi kupitia uinarishaji wa rasilimali watu, huku wauguzi wakiwa nguzo muhimu katika mpango huo.
“Tunatarajia muwe mabalozi wa huduma bora. Uadilifu, huruma na kufuata maadili ya kazi ni msingi wa hadhi ya kada yenu. Serikali inawahitaji, na wananchi wanawategemea,” alisema Mngereza.
Katika maelezo ya mpango mkakati wa Wizara ya Afya, Katibu
Mkuu alieleza kuwa Serikali inatekeleza vipaumbele kadhaa, ikiwemo kuimarisha
huduma za msingi, kuondoa changamoto za upatikanaji wa huduma vijijini, na
kuongeza ufanisi wa vituo vya afya na kubainisha kuwa Wauguzi ndio nguzo muhimu Katika kufanikisha mpango huo.
"Tunahitaji muwe sehemu ya mageuzi haya, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali na viongozi wenu wa afya,” alisisitiza Mngereza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Uuguzi na Ukunga, Mwanaisha
Juma Fakih aliwataka wauguzi waliomaliza
mafunzo hayo kuhakikisha wanazingatia kanuni na maadili ya taaluma kila
wanapokuwa kazini, akibainisha kuwa taaluma ya uuguzi inahitaji nidhamu na utu.
“Maadili na uwajibikaji ndio silaha yetu. Muuguzi
anayeheshimu muda wa kazi, anayefanya kazi kwa weledi na anayeheshimu utu wa
mgonjwa, huyo ndiye tunayemtaka katika mfumo wa afya. Taaluma hii haiwezi
kusimama bila maadili,” alisema Mwanaisha .
Aliongeza kuwa vitendo vinavyodhalilisha taaluma
havitavumiliwa na wizara, huku akiwasisitiza kuifahamu vizuri miongozo ili
kuepuka migongano ya kitaaluma.
Alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma zenye heshima, salama na
zinazozingatia thamani ya mgonjwa, huku akihimiza matumizi sahihi ya
rasilimali, lugha (customer care) na uwajibikaji wa kitaaluma.
"Utendaji wenu ni lazima uendane na muonekano wenu ni muhimu kuzingatia maadili
na kujali utu, hii itawaongezea thamani na kuonesha utofauti wa kiutendaji
kabla na baada ya kurudi masomoni" Alisema
Mwanaisha
Kikao hicho pia kilitoa mwongozo wa kina kuhusu usajili na
utoaji wa leseni ya uuguzi kupitia Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar ambapo
mrajisi wa Baraza hilo Vuai Kombo Haji aliwakumbusha wahitimu kufuata taratibu
zote za kujisajili na kubainisha kuwa usajili sahihi ni hatua ya kwanza ya
kutambulika kisheria kama mtaalamu.
“Ni wajibu wenu
kuhakikisha mnapata leseni, maana bila ya nyaraka hizi hamtaruhusiwa kutoa
huduma popote nchini,” alieleza Vuai
Baadhi ya wauguzi waliomaliza mafunzo ya utarajali waliipongeza Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo
Ambayo yamewajengea uwezo na uzoefu kutoka Katika hospital walizofanya Mafunzo hayo Kwa vitendo na
kubainisha kuwa yamewajenga kujiamini.
“Tumepata mwanga wa nini Serikali inatarajia kutoka kwetu.
Tuko tayari kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu utu wa wagonjwa.” alisema Amina
mmoja wa wahitimu hao.
Kikao hicho kililenga kuhakikisha wahitimu hao wanarudi
rasmi makazini wakiwa na uelewa wa pamoja, misingi ya maadili, na dhamira ya
kutoa huduma bora kwa wananchi.
0 Comments