Mradi wa Start
Small unaotekelezwa na Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Kitengo Shirikishi afya
ya mama na mtoto, kwa ushirikiano na MSI Tanzania na ZAFAYCO, unaendelea kuleta
matokeo chanya ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na kuimarisha
huduma za uzazi wa mpango hapa nchini.
Akizungumzia
mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia
mradi huo, Mratibu wa Kitengo
Shirikishi Afya ya mama na mtoto Saida Abubakar Muhammad amesema
takwimu zinaonyesha kupungua kwa vifo vya mama kutoka 79 mwaka 2023, hadi 66 mwaka
2024, na kufikia 45 Oktoba 2025, kipindi ambacho mradi unaendelea kutekelezwa
na hatua hiyo inaonesha mafanikio ya
moja kwa moja ya uwekezaji katika elimu na huduma za uzazi wa mpango.
Aidha, Saida
ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa huduma rafiki kwa vijana
kupitia vituo maalumu, sambamba na kufanya huduma mkoba katika jamii kwa kushirikiana na waelimishaji
rika, programu za vijana na viongozi wa maeneo mbalimbali. Juhudi hizo
zimewezesha kuwafikia vijana wengi katika Maskuli , vyuo na maeneo ya
mikusanyiko, hali iliyoimarisha uelewa kuhusu afya ya uzazi na njia salama za
kupanga uzazi.
Ameongeza kuwa wahudumu wa afya wamepatiwa usimamizi wa kitaalamu, mafunzo na ufuatiliaji wa karibu, hatua iliyosaidia kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango.
Kwa upande wake,
Meneja wa Mradi wa Start Small kutoka MSI Tanzania, Domitila Jacksin Masala, amesema mradi huo umesaidia kupunguza
mimba zisizotarajiwa na zisizosalama kwa wastani wa zaidi ya elfu arobaini na
tatu.
Amesema mradi
ulilenga kutatua changamoto zinazowakabili vijana hususan katika elimu ya uzazi
wa mpango pamoja na ujasiriamali kwa ushirikiano na ZAFAYCO, ambapo
wamefanikiwa kuwafikia vijana wengi wakiwemo asilimia 26 wa vijana chini ya
miaka 25.
Nae Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la kupambana na changamoto za vijana ZAFAYCO Abdalla Abeid amesema kuwa mradi ulijumuisha afya na uchumi ili kumjenga kijana katika sekta kuu mbili za afya na uchumi kwa kuwajengea uwezo vijana kuhusu ujasiriamali.
Amesema wameweza
kuwafikia vijana kwa asilimia sabini wa vyuo vikuu vilivyopo hapa Unguja na
wale ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kuweka mabonanza katika maeneo
mbali mbali.
Amina Haji Manzi ni miongoni mwa wananufaika wa elimu ya uzazi wa mapango na hapa anatueleza sababu zilizopekea kutumia njia ya uzazi wa mpango na kutoa wito kwa wanawake wenzake kutumia njia za uzazi wa mpango ili Watoto waweze kupishanisha na kupata muda wa kupumzika.
Mradi wa Start Small, ulioanza mwaka 2024 katika vituo sita na sasa umeongezeka hadi kufikia vituo 15, umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za muda mrefu za uzazi wa mpango pamoja na kuongeza idadi ya watumiaji, hatua inayoendelea kuleta matumaini katika kuboresha afya ya mama, mtoto na vijana Zanzibar.
0 Comments