DAR ES SALAAM
BAADA ya kuwa mapumzikoni kwa takriban mwezi mmoja, wachezaji wa Azam FC wameanza kuwasili jijini Dar es Salaam kwa maandalizi ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Taarifa za klabu hiyo zimefahamisha kuwa, kwa mujibu wa programu ya maandalizi ya klabu hiyo, wanandinga hao wataanza mazoezi kesho, kujiweka sawa kwa ajili ya mashindano hayo yatakayofanyika nchini mwezi ujao.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Azam FC kushiriki mashindano hayo baada ya kumaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ikishika nafasi ya pili, ambayo pia inaipa nafasi ya kushiriki Kombe la Shrikisho la Soka Afrika (CAF), mwakani.
Imefahamika kuwa, wachezaji wa timu hiyo wanaotoka nje ya Tanzania, watawasili wiki hii, kwa maandalizi ya makazi kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo yatakayofanyika kwenye uwanja wa Azam Chamazi.
Hata hivyo, kambi ya klabu hiyo itaathiriwa kidogo na kambi za timu za taifa ambapo baadhi ya wachezaji wamo kwenye timu hizo.
Wachezaji waliopo kwenye timu za taifa ni Joseph Owino (Uganda Cranes), George Odhiambo (Kenya), Aggrey Morris, Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Salum Abubakar, Mrisho Ngasa, na John Bocco (Taifa Stars-Tanzania).
Aidha wanasoka wengine wa klabu hiyo, Abdulhalim Humoud, Khamis Mcha, Abdi Kassim na Abdulghani Ghulam wako na timu ya taifa ya Zanzibar iliyokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa mataifa yasiyo wanachama wa FIFA.
Usajili wa wachezaji ulifanyika kabla hawajaenda likizo, hivyo wachezaji wote waliosajili wataanza mazoezi isipokuwa wale walioko kwenye timu za taifa (Tanzania, Uganda na Zanzibar) ambao watajiunga na wenzao baada ya kumaliza michezo inayowakabili.
Programu ya maandalizi ya CECAFA itamalizika siku moja kabla ya kuanza mashindano hayo mwezi ujao, na mara yatakapomalizika, timu itakuwa na mapumziko ya siku chache kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya ligi kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao wa 2012-2013.
0 Comments