Na Laylat Khalfan
CHAMA cha CUF, kimeishauri Idara ya Uhamiaji kufanya operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu waliojificha Zanzibar ili kukabiliana na matukio ya uhalifu.
Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano na Haki za Binadamu wa CUF, Salum Bimani, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Mtendeni jana.
Alisema operesheni hiyo ambayo inafanyika katika mikoa ya Tanzania Bara, lazima ihamishiwe na Zanzibar kwa kuwa anaamini wako wahamiaji haramu na wanaweza kuwa wanashiriki katika matukio ya uhalifu.
Operesheni ya kukabiliana na wahamiaji haramu ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete baada ya kushamiri matukio ya kihalifu katika mikoa ya Mwanza, Kigoma na Geita, operesheni ambao imepewa jina la kipunga.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Masoud amemshauri Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, kupima baadhi ya kauli zake kabla ya kuzitangaza kwa waandishi wa habari kwa sababu zinaweza kuleta athari kubwa kwa uchumi wa Zanzibar.
Alikuwa akielezea kauli za Kamishna Mussa alizozitoa hivi karibuni katika vyombo vya habari, kwamba wamekamata watu 25, ambao baadhi yao walikiri kushabikia kundi la wanamgambo la kiislami la Al Shabaab la Somalia na kwamba walikuwa katika harakati za kwenda kupigana vita vya jihadi.
Alisema CUF inalaani kwa nguvu zote vitendo hivyo na vyengine vya kihalifu, lakini hakioni kuwa ni busara kudai kuna vijana wenye mafungamano na vikundi vya Al Shabaab kwa sababu kauli hiyo inaweza kuiathiri Zanzibar kiuchumi.
Alisema, mtu yeyote anapotajiwa vikundi hivyo, moja kwa moja hupata dhana ya ugaidi, jambo alilosema linaweza kuichafua taswira ya Zanzibar na kuwafukuza watalii ambao nchi inawategemea sana kwa kuingiza mapato na kuinua uchumi wake.
Alieleza kuwa, katika kipindi hichi ambacho nchi imekumbwa na matukio ya hujuma za aina hiyo, jeshi la polisi linapaswa kufanya kazi kitaalamu kwa kuwasaka na kuwashika wahusika wa kweli, badala ya kumshika kila mtu na hatimaye kudai hakukutwa na kesi.
Alisema CUF haikatai kwamba Zanzibar wapo wahalifu wanaohatarisha amani ya nchi na itafurahi kama watashikwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, lakini haipendezwi kuona jeshi la polisi linafanya kazi kwa kubahatisha.
Masoud ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Ole, alitahadharisha kuwa, iwapo jeshi la polisi litaendelea kutamka hadharani kauli kama hizo, ni wazi zitawajengea hofu watu wa mataifa ya nje wakiwemo watalaii.
Aliliomba jeshi la polisi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
1 Comments
Hapo hata mimi namuunga mkono mhe.Hamad Masoud, Kauli ya Kamishna Mussa kwamba vitendo vya kihalifu Z'bar vina uhusianao na Al-shabab ni hatari kwa utalii na uchumi kwa ujumla.
ReplyDeleteAkumbuke kwamba hata hizo nchi ambazo zimekua waathirika wa moja kwa moja wa al-shabab bado hawatangazi, wanaendelea kuficha na kupambana nao kimya kimya huku wakidai kua nchi yao ni salama ili kulinda uchumi wao.
Kamishna ni zaidi police, anatakiwa kuelewa mambo ya siasa, uchumi na diplomasia ili kuepuka kutoa maneno yenye utata!