6/recent/ticker-posts

Shamuhuna Asema Utoro Ulichangia Wanafunzi Kufeli Zenj..

Na Zainab Anuwar, ZABECS Pemba
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Ali Juma Shamuhuna, amesema utoro kwa wanafunzi ni moja ya sababu kubwa iliyochangia matokeo mabaya ya mitihani mwaka 2012.

Alisema hayo katika uwanja cha michezo Gombani Chake Chake Pemba, wakati akiwahutubia walimu na wanafunzi katika maadhimisho ya miaka 49 ya elimu bila ya malipo.

Alisema utoro kwa wanafunzi pamoja na walimu kutomaliza mtaala wakufundishia pia kwa kiasi kikubwa ilichangia matokeo mabaya.

Alisema mitihani inayotungwa inatokana na mitaala inayotumiwa na walimu hivyo aliwataka walimu kuhakikisha wanamaliza mitaala yao kwa wakati.

“Hili tulilibaini katika mikutano yetu tuliyoifanya kila mkoa kwa mikoa yote mitano ya Zanzibar,pale tulipokutana na walimu wakuu, kamati za skuli na baadhi ya wadau wa elimu, humo ndimo tulipopata taarifa hiyo,” alisema.

Akizungumzia suala la mishahara ya walimu, alisema serikali imeandaa mpango mzuri kwa walimu wenye mafanikio utakaowatunza walimu wake.

Alisema bado serikali ineendelea na jitihada za kufundisha walimu wa masomo ya sayansi katika vyuo vyake vikuu, ili kuwa na walimu bora.

Hata hivyo, alisema serikali itaendelea na juhudi zake za kujenga skuli za kisasa zenye ubora zaidi zitakazokidhi mahitaji ya wanafunzi ikiwemo vyumba vya maabara, vyumba vya kompyuta na mktaba.

Akimkaribisha Waziri wa Elimu, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Juma Kassim Tindwa, alisema walimu, wazazi na wanafunzi hawanabudi kushirikiana ipasavyo kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi, Nd. Uledi Juma Wadi, alisema lengo la tamasha la elimu bila ya malipo ni kutathmini utoaji wa wa elimu na vipaji vya wanafunzi kimichezo na utamaduni.

Nao wanafunzi wameiomba wizara kufanya utafiti wa matokeo mabaya ya mitihadi ya wanafunzi ili kugundua changamoto zilizosababisha tatizo hilo.

Post a Comment

0 Comments