Na Khamis Amani
YUSSUF Mohammed Yussuf (46) mkaazi wa Beit el Ras wilaya ya magharibi Unguja, aliyeshitakiwa kwa makosa ya kukashifu na kumuingilia kinyume cha maumbile mwanafunzi wa kike wa skuli ya msingi Rahaleo mwenye umri wa miaka minane, amehukumiwa kifungo cha miaka 28 jela.Adhabu hiyo imetolewa na Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar George Joseph Kazi.
George Kazi ambae pia ni hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga, alitoa adhabu hiyo baada ya kumtia hatiani mshitakiwa kufuatia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Kabla ya kutoa adhabu hiyo, George Kazi alisema makosa kama hayo yamekuwa tishio nchini na inafaa kutolewa adhabu kali kwa wahusika.
Alisema inasikitisha kuona mengi ya matendo hayo yanafanywa na walimu wa skuli na madrasa ambao wanategemewa na jamii kuwa walezi wazuri na waelimishaji.
Alisema mahakama hainabudi kuungana na serikali kuu kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinaweza kuwapotezea mwelekeo wa maisha waathirika.
Kabla ya adhabu hiyo, baada ya mahakama kumtia hatiani upande wa mashitaka ulioongozwa na Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Abdallah Mgongo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa.
Yussuf Mohammed Yussuf, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mbele ya hakimu wa mkoa Khamis Ali Simai Septemba 6 mwaka huu na kusomewa mashitaka ya kutorosha mtoto wa kike, shambulio la aibu na shitaka kumuingilia mtoto huyo kinyume cha maumbile.
Katika mashitaka hayo, ilifahamishwa baina ya mwezi wa Juni na Julai mwaka jana saa zisizojulikana, huko skuli ya Rahaleo wilaya ya Mjini Unguja bila ya halali alimchukua mtoto wa kike wa miaka nane (jina tunamuhifadhi) kutoka skulini hapo na kumpeleka nyumbani kwake Beit el Ras bila ya idhini ya wazazi wake.
Kitendo hicho kimeelezwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 130 (a) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria Zanzibar.
Sambamba shitaka hilo na hilo kinyume na kifungu cha 131 (1) (2) cha sheria namba 6/2004 mshitakiwa huyo alishitakiwa kwa kosa la shambulio la aibu dhidi ya mtoto huyo.
Ilielezwa kuwa siku hiyo alimkashifu mtoto huyo kwa kumchezea maziwa na sehemu zake za siri akiwa ni mtoto mdogo.
Shitaka la mwisho alilosomewa ni la kumuingilia kinyume cha maumbile mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri za nyuma.
Mahakama ilifahamishwa kitendo hicho ni kosa chini ya kifungu cha 150 (a) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Mashitaka hayo alisomewa na Wakili wa serikali Suleiman Massoud ambayo aliyakana, na mahakama ilimpeleka rumande kwa muda wa siku 12 baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana.
Hadi kesi hiyo inatolewa hukumu, mshitakiwa alikuwa nje kwa dhamana.
Nje ya mahakama mshitakiwa aliwahi kuwa msanii maarufu wa taarab asilia nchini akikiimbia kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa (Malindi) na miongoni mwa nyimbo alizotamba nazo ni 'Raha ya moyo wangu', 'Umbrela' na nyenginezo nyingi zilizompatia sifa.
0 Comments