Na Khamis Haji, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu hatua ya Misri kutaka kuleta miradi ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu kwa vile sekta hiyo itatoa fursa nyingi za ajira na kuinua uchumi wa nchi.Maalim Seif aliyasema hayo jana ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar,wakati akizungumza na Balozi mdogo wa Misri Zanzibar, Mhe. Walid Mohammed Ismail.
Alisema Zanzibar ina utajiri mkubwa wa maliasili za baharini ambazo bado hazijatumika ipasavyo katika kuinua uchumi na maisha ya Wazanzibari, hivyo hatua ya kukaribisha uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ni muhimu kwa wakati huu.
Alisema iwapo miradi ya uvuvi inayokusudiwa kuanzishwa na kampuni za Misri italeta mafanikio, wananchi wengi hasa vijana watanufaika na ajira na hivyo kuondokana na ugumu wa maisha.
Mapema Balozi huyo mdogo, alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa mipango ya kuwawezesha wawekezaji katika uvuvi wa bahari kuu kuja Zanzibar inaendelea na kwamba ujumbe kutoka Misri unatarajiwa kuwasili Zanzibar mwezi ujao.
Balozi huyo alisema anakusudia kuwashawishi wawekezaji hao kutoa muhimu mkubwa katika kufungua viwanda vya kusindika samaki na mazao mengine ya baharini, ili kutoa fursa kubwa zaidi ya ajira kwa wananchi.
Aidha, katika mazungumzo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais aliipongeza Misri kwa hatua yake ya kuongeza nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar, wanaosoma fani tafauti.
Alisema hatua hiyo inaisaidia Zanzibar katika kupunguza uhaba wa wataalamu wakiwemo wa sekta za afya na walimu wa fani mbali mbali, wakiwemo wa dini ya kiislamu.
Alimuahidi Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendeleza ushirikiano huo ambao umedumu kwa miaka mingi.
Akizungumzia hali ya siasa na usalama nchini Misri, Balozi huyo alisema hali ni shuari baada ya serikali ya mpito kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vurugu zilizokuwa zikijitokeza miezi kadhaa iliyopita na kusababisha kupotea maisha ya watu na uharibifu zinakomeshwa.
Balozi Wahid alisema maandalizi ya kupata katiba mpya ya Misri ambayo itatoa haki kwa wananchi wote inaendelea, na matarajio ni ifikapo mwakani nchi hiyo itapata utawala ulio imara ambao unatokana na ridhaa ya wananchi wote.
Maalim Seif akizungumzia hilo alisema hali iliyokuwa imejitokeza Misri iliwatia hofu watu wengi kutokana na nafasi muhimu ya nchi hiyo katika bara la Afrika pamoja na ulimwengu wa nchi za kiarabu.
Alisema kutokana na nafasi ya Misri, Zanzibar pamoja na nchi nyengine mbali mbali duniani, zimekuwa zikiiombea nchi hiyo kupata uongozi mzuri ili iendelee kuwa tulivu.
0 Comments