Na Fatuma Kitima, DSM
POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti iliyotumika kusafirisha dawa za kulevya zilizowekwa tumboni mwake.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Suleiman Kova aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Nasir Omari (36) na Mwanaisha Salim (36) wakazi wa Kigogo Luhanga waliosafirisha maiti hiyo kutoka Mtwara.
Alisema tukio hilo lilitokea Tabata jijini Dar es Salaam jana.
Kamishna Kova alisema polisi walipata taarifa ya mtu aliyefariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga, ambapo makachero walifika eneo la tukio na kuhoji na hatimaye kuikuta maiti ikiwa imelezwa sebuleni.
Alisema Nasir Omar ndiye mmliki wa chumba alichokutwa marehemu aliyejuliakana kwa jina la Rajabu Kidunda (43) ambae ni mfanyabiashara.
Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa maiti hiyo ilisafirishwa kutoka Mtwara Septemba 21 ingawa watuhumiwa wanadai walimchukua akiwa mgonjwa kumleta Dar es Salaam kwa matibabu.
Alisema watuhumiwa wanadai marehemu alikwenda bafuni kukoga na kurudi katika chumba hicho na hatimaye kupatwa na umauti.
Alisema mazingira ya kifo hicho yalichangia polisi kufika eneo la tukio na kuchukua maiti na kuipeleka hospiatali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi.
Kova alisema uchunguzi ulifanywa chini ya madaktari wawili ukishuhudiwa na maafisa wa juu wa polisi pamoja na ndugu wa karibu wa marehemu.
Katika uchunguzi huo alisema walibaini tumbo la marehemu limetumika kuweka kete za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
“Uchunguzi zaidi unafanyika kuhusu tukio hilo ili kubaini mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo ambao umemuhusisha marehemu na wote watakao bainika watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,”alisema.
Aidha alisema marehemu alikutwa na hati ya dharura ya kusafiri nje ya nchi ambayo haijaonesha kuwa anasafiri kwenda nchi gani,pia alikutwa na fedha za Kenya shilingi 700, dola 100 za Marekani na fedha za Sychelles.
Aliongeza kuwa operesheni ya kukamata dawa za kulevya inaendelea na kuiomba jamii itoe ushirikaino ili kuchukuliwa hatua.
0 Comments