HOTUBA YA MAKAMU WA
KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD
KATIKA UZINDUZI WA
NYUMBA SALAMA KWA WAATHIRIKA WA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE ZANZIBAR
HUKO OCEAN VIEW RESORT ZANZIBAR TAREHE 9 OKTOBA, 2013
Mheshimiwa Waziri wa Ustawi
wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto,
Waheshimiwa MawazirI,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
wa Mjini Magharibi,
Mheshimiwa Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi, Mwakilishi wa
Jumuiya ya Ulaya Tanzania,
Viongozi
wa Shirika la ActionAid,
Waheshimiwa
waalikwa nyote Mabibi na Mabwana,
Asslam
Alaykum
Awali ya yote sina budi kuelekeza shukurani zangu
kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai, uzima na wenye afya njema na
kuweza kukutana hapa leo kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa ustawi na maendeleo
ya nchi yetu na watu wake.
Vile vile nitowe shukurani zangu za dhati kwa
Jumuiya ya Ulaya pamoja na washirika wake Shirika la ActionAid kwa kuandaa
mradi wa kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake wa Zanzibar.
Aidha niwashukuru kwa kuona haja ya kunialika mimi
kuja kujumuika nanyi katika shughuli hii ya Uzinduzi wa nyumba salama kwa akina
mama waliopata athari za vitendo vya ukatili.
Najisikia faraja sana leo kuona kwamba nilipata
fursa ya kuzindua mradi huu wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto mwezi
Machi mwaka jana. Nilielezwa wakati wa uzinduzi wa mradi huu kwamba moja wapo
ya malengo ya mradi huu ni uanzwishaji wa nyumba salama kwa watu walioathirika
kwa vitendo vya ukatili.
Nifaraja kwangu kuona leo hii nipo tena katika
ukumbi huu kusikia muendelezo wa mradi pamoja na kuzindua nyumba salama kwa akina
mama hao waliopata athari za vitendo vya ukatili na udhalilishaji. Nasema
kwangu mimi binafsi hii naona ni heshima kubwa mliyonipa.
Waheshimiwa viongozi na
waalikwa
ActionAid
ni Shirika la Kimataifa ambalo limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi
ya umasikini, utetezi wa haki na kupiga vita vitendo vya ukandamizaji na
uvunjifu wa sheria. Shirika hili kwa hakika linatoa mchango mkubwa na wa
kipekee katika kukuza maendeleo ya watu wote Tanzania, ikiwemo Zanzibar.
Kuanzishwa kwa nyumba salama ambayo ni muendelezo wa hatua ya kupinga ukatili
dhidi ya wanawake Zanzibar itasaidia sana katika kulinda haki za akina mama na
hivyo kutoa fursa ya kujenga jamii nzima ya Wazanzibari iliyo na uadilifu.
Lakini
vile vile hatua hii ni muhimu katika kusaidia juhudi za serikali yetu hasa
katika kazi muhimu inayoendelea ya kupiga vita aina zote za ukatili na
udhalilishwaji wanawake na watoto.
Waheshimiwa viongozi na
waalikwa
Vitendo
vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni miongoni mwa matukio mabaya
yanayoendelea kujitokeza katika jamii mbali mbali duniani na kusababisha
madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na uhai wa binaadamu. Matukio ya aina
hiyo tunayashuhudia yakiongezeka pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa katika
ngazi za kitaifa na kimataifa kuyatokomeza.
Kimataifa
takwimu zinaonesha mwanamke mmoja kati ya watatu amekumbana na vitendo vya
ukatili, iwe wa aina moja au nyengine, hali ambayo inasababisha madhara
makubwa, sio tu kwa wanawake waliohusika kufanyiwa vitendo hivyo, bali kwa
watoto katika familia ambao hushuhudia vitendo hivyo.
Miongoni
mwa madhara makubwa yatokanayo na ukatili dhidi ya wanawake ni kukosekana usawa
katika jamii, athari za kisaikolojia, kurejesha nyuma maendeleo pamoja na
kuchangia kukosekana hali ya amani.
Ukatili
wa kijinsia ukiwemo ule unaolengwa wanawake hivi sasa ni uvunjifu wa haki za
kibinaadamu. Jumuiya ya Kimataifa
inalazimika kupitisha maazimio na mikakati mbali mbali kwa nia ya kutokomeza
kabisa matendo hayo. Miongoni mwa maazimio hayo ni lile la kupiga vita aina
zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake la mwaka 1993, ambalo limeweka
bayana vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa aina hiyo.
Aidha,
azimio maarufu la Beijing mwaka 1995 ambalo limeweza kutoa mwamko mkubwa kwa
mataifa katika vita dhidi ya ukatili kwa wanawake, pia limesaidia sana mataifa
mbali mbali kuweka mikakati na malengo ya utekelezaji katika kuinua hali za
wanawake, iwe katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, na vile vile limesaidia
kuibua harakati za kuelimisha jamii umuhimu wa kukomeshwa ukatili dhdi ya
wanawake na kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma maendeleo yao.
Tanzania
inaunga mkono kwa dhati hatua za kupiga vita aina zote za ukandamizaji, ukatili
na ubaguzi wa kijinsia, ikiwemo dhidi ya wanawake na watoto na imetia saini
makubaliano na itifaki mbali mbali zinazohusu mambo hayo na sasa inazitekeleza.
Waheshimiwa viongozi na
waalikwa
Hapa
kwetu Zanzibar, Serikali imeweka mikakati mbalimbali katika kushughulikia
tatizo hili ikiwemo Kamati ya Mawaziri iliyoanzishwa na Mheshimiwa Rais, Dk.
Ali Mohammed Shein, kwa ajili ya kuchunguza ukubwa wa tatizo hili, lakini pia
jukwaa ambalo litajadili changamoto zilizopo katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo
hili.
Pia
uanzishwaji wa Kamati za Makatibu Wakuu ambao hukutana kujadili na kupeana
miongozo juu ya utatuzi wa jambo hili. Serikali pia imeanzisha kamati mbali mbali
za kitaifa, wilaya na hata vijiji, ili kupambana na kadhia hii. Kuanzishwa kwa
vituo vya mkono kwa mkono na dawati la wanawake na watoto pia ni miongoni mwa
jitihada za serikali za kupambana na matatizo yanayo wakabili akina mama na
watoto.
Hata
hivyo, lazima tukiri kwamba pamoja na mataifa, ikiwemo nchi yetu kuchukua hatua
tofauti kukomesha ukatili dhidi ya wanawake, bado safari ndefu ipo mbele yetu,
kwasababu matukio hayo bado yanaendelea kujitokeza kwa wingi.
Sababu
zinazoelezwa kuchangia ukatili dhidi ya wanawake ni nyingi na zinatafautiana
kutokana na mazingira au jamii moja hadi nyengine, miongoni mwa hizo ni mifumo kandamizi
ya kimaisha ambayo imeota mizizi katika jamii zetu na kuonekana kama ndio
utaratibu wa maisha.
Kutokana
na hali hiyo, ili tuweze kuing’oa mifumo ya aina hiyo na kuleta usawa miongoni
mwa jamii pamoja na kukomesha kabisa ukatili dhidi ya wanawake, sote
tunahitajika tushiriki katika vita hivi, kuanzia serikali, jumuiya zisizokuwa
za kiserikali kama hii ActionAid na nyenginezo, lakini pia jamii nzima.
Waheshimiwa Viongozi na
Waalikwa
Kwa
masikitiko makubwa jamii ya Wazanzibari ni miongoni mwa zinazokabiliwa na aibu
hii ya ukatili dhidi ya wanawake pamoja na watoto. Tafiti chache zilizofanyika
katika baadhi tu ya maeneo zinadhihirisha ukubwa wa tatizo hilo, hali ambayo
inatulazimisha tusimame kidete kukabilina na vitendo hivyo, ili wanawake nao
waishi kwa amani bila ya bughudha kutoka kwa watu wengine na waweze kuchangia
kikamilifu kukuza maisha yao na taifa lao.
Miongoni
mwa sababu zinazoelezwa kuchangia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake Zanzibar
ni kuwepo mitazamo potofu juu ya wanawake, ukimya miongoni mwa wanawake wenyewe
na jamii inayowazunguka, kuona aibu na muhali kwa wanawake wanaofanyiwa vitendo
hivyo na hivyo kushindwa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.
Matokeo
ya hali hiyo ni matukio mengi ya udhalilishwaji wanawake kutoonekana kuwa ni
makosa ya jinai, na badala yake jamii inayaona kama ni masuala ya kifamilia na
hivyo kuyamaliza nje ya taratibu za kisheria ambapo haki za waliodhulumiwa
hazizingatiwi.
Kwa
upande mwengine kupungua kwa imani ya wananchi kwamba wanaweza kupata haki
katika mifumo rasmi, kama vile Polisi na Mahakama kutokana na hali ya
ucheleweshwaji wa kesi, ada za mahakama, gharama za usafiri kufuatilia kesi,
pamoja na kuwepo vitendo vya rushwa, ambapo hata wale wanaotiwa hatiani ni
wachache, hakuzuwii wahalifu kushawishika kuachana na matendo kama hayo.
Waheshimiwa viongozi na
waalikwa
Kukosekana
kwa mahali salama ambapo watu walioathirika watapatiwa huduma mbali mbali,
ikiwemo za ushauri nasaha, kunalazimisha watu hao kukata tamaa na kwamba
muendelezo wa kesi zao siku zote unakuwa ni wa vikwazo na mwisho haki
haipatikani. Kutokana na hali hii,
mapatano ya kinyumbani ndio mara nyingi yanayotumika ambayo kamwe hayawezi
kulimaliza tatizo.
Matukio
ya wanawake kupigwa na waume zao na mara nyengine hata kujeruhiwa, vile vile
yanaripotiwa siku hadi siku ndani ya jamii yetu ya Wazanzibari. Bila shaka
tabia ya kuacha na kudharau maadili yetu mema ina sehemu katika kukithiri kwa
ukatili na udhalilishaji wanawake.
Waheshimiwa Viongozi na
Waalikwa
Ukatili
dhidi ya Wanawake wenye Ulemavu ni mkubwa zaidi na unaoonesha sura mbaya zaidi
ya kutojali utu na ubinaadamu katika jamii zetu. Tabia ya Wanawake wenye Ulemavu
hasa wa akili kubebeshwa ujauzito mara kwa mara, kupigwa na kufanyishwa kazi
nzito na aina mbali mbali za udhalilishaji, unaonesha jinsi jamii isivyo wajali
wenzetu hao.
Aidha,
katika siku za hivi karibuni, kumeripotiwa matukio ya kuuwawa kwa wanawake na watendaji wa hayo ni
waume zao. Huo ni unyama wa hali ya juu na ya kutisha, hatuna budi kuupiga vita
kwa nguvu zote.
Kwa
mara nyengine tena nazipongeza jitihada za wadau mbali mbali wakiwemo Actionaid
na washirika wake katika kubuni mbinu zitakazosaidia kumaliza kabisa vitendo
vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.
Waheshimiwa Viongozi na
Waalikwa
Nazihimiza
kwa nguvu kubwa taasisi nyengine za Serikali na za binafsi, kutoa mashirikiano
ya hali na mali katika uendelezaji wa nyumba salama. Aidha serikali kwa kupitia
wizara husika itakuwa na jukumu la
kuhakikisha uendelevu wa program nzima ya nyumba salama zikiwemo upatikanaji wa
huduma za kiushauri kwa watu waliopata athari kutokana na vitendo hivyo,
kuangalia usalama wa wanawake wakiwepo ndani ya nyumba salama, uharakishaji wa
kesi zinazohusiana na matendo ya ukatili kwa wanawake na watoto. Serikali pia
itashirikiana na Actionaid na wadau wengine katika kutafuta ufadhili wa
uendelezaji wa nyumba salama.
Waheshimiwa Viongozi na
Waalikwa
Ni
imani yangu kubwa pia kwamba, Jumuiya ya Ulaya ambao ndio wafadhili wakubwa wa
jitihada hizi, hawatatuacha mkono katika kuendeleza jitihada hizo.
Kwa upande
wake serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali kukomesha aina zote za
ukatili dhidi ya Wanawake, pamoja na watoto wetu, kwa kuweka sheria mpya na
kuzirekebisha zile ambazo zitaonekana hazikidhi haja kutokana na wakati uliopo.
Vile vile
tutawapa nguvu kubwa wanawake katika masuala ya kiuchumi na kimaendeleo, ikiwa
ni pamoja na kuzipa msukumo wa kipekee jumuiya na taasisi zisizokuwa za
kiserikali zinazojitokeza kukomesha matendo maovu dhidi ya wanawake na watoto,
na kujenga mazingira ya kukuza maendeleo yao.
Waheshimiwa Viongozi na
Waalikwa
Baada
ya kusema hayo niruhusuni tena nitoe shukurani zangu kwenu nyote kwa
kunisikiliza na kuwa watulivu katika muda wote nilipokuwa nikizungumza.
Na sasa kwa
heshima na taadhima nachukua fursa hii kutamka rasmi kwamba, NYUMBA SALAMA KWA WATU WALIOATHIRIKA KWA
VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE ZANZIBAR, nimeizindua rasmi.
Ahsanteni.
0 Comments