6/recent/ticker-posts

Maalim Seif apongeza juhudi za urejeshaji wa rasilmali asilia

 Mkurugenzi mtendaji wa Community Forest Pemba, Mbarouk Mussa Omar, akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi wao, wakati alipokutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seeif Sharif Hamad, Ofisini kwake Migombani.
 Mkurugenzi mtendaji wa “Community Forest International” Jeff Schnurr, akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi wao, wakati alipokutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seeif Sharif Hamad, Ofisini kwake Migombani
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seeif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira kutoka Canada, pamoja na watendaji wa ofisi yake, baada ya mazungumzo na wadau hao Ofisini kwake Migombani. (Picha na Salmin Said, OMKR).
 
Na Hassan Hamad OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesifu juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya inayojihusisha na urejeshaji wa rasilimali asilia ya “Community Forest Pemba”, katika kuwapatia wananchi elimu juu ya utumiaji wa nishati mbadala na kuhifadhi mazingira kisiwani humo.
 
Maalim Seif ametoa pongezi hizo leo wakati alipokutana na uongozi wa Jumuiya hiyo, pamoja na watendaji wa Community Forest International ambao wamekuwa wakifanya shughuli hizo kwa mashirikiano.
 
Amesema elimu ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo nishati mbadala, upandaji miti na utaalamu wa uvunaji wa maji ya mvua inahimizwa sana na Serikali, na kwamba hatua ya jumuiya hizo kueneza taaluma hiyo inasaidia sana juhudi za serikali.
 
Maalim Seif amezihimiza jumuiya hizo kuendelea kuwa karibu na wananchi katika Shehia mbali mbali kisiwani humo, ili wananchi waendelee kunufaika na utaalamu wao, ambao ni rahisi na unaoepusha madhara ya uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Community Forest Pemba, Mbarouk Mussa Omar, wananchi wa vijijini wanaweza kupunguza gharama za matumizi kwa kutumia nishati mbadala na kuepuka uhariribifu wa mazingira, sambamba na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi.
 
Amesema mradi huo ambao pia unajihusisha na utengenezaji wa majiko sanifu, upandaji wa miti na kilimo, pia umefanikiwa kujenga skuli pamoja na hodhi linalohifadhi lita laki mbili  katika kisiwa kidogo cha Kokota Pemba, vitu ambavyo tayari vimeanza kutoa huduma kwa wananchi wa kisiwa hicho.
 
Amefahamisha kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi 14 ya Tanzania inayofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU), na kwamba wamebakiwa na mwezi mmoja kukamilisha mradi huo.
 
Naye Mkurugenzi mtendaji wa “Community Forest International” Jeff Schnurr, amesema Zanzibar inavyo vianzio vingi vya upatikanaji wa nishati mbadala vikiwemo takataka zinazozalishwa pamoja na upepo.
 
Amesema Jumuiya yake itawahamasisha wadau wengine wa mazingira duniani kuja kufanya utafiti Zanzibar, ili kuona maeneo zaidi ambayo yanaweza kusaidia kupatikana kwa nishati mbadala na uhifadhi wa mazingira ya visiwa kwa ujumla.
 

Post a Comment

1 Comments

  1. Mahodhi ya maji yaliojengwa sio moja tu. Mahodhi yaliojengwa na Community Forests Pemba (CFP) ni Mahodhi mawili, moja katika katika kisiwa cha Kokota ambalo lina uwezo wa kubeba lita zaidi ya 250,000 na katika kisiwa cha Uvinje kiliopo katika Shehia ya Fundo tumejenga Hodhiambalo lina uwezo wa kubeba lita zaidi 150,000. Mahodhi yote hivi sasa yameshannza kutumiwa na wananchi wa visiwa hivyo.

    ReplyDelete