Na Fatina Mathias, Dodoma
SHEREHE ya kukabidhiwa katiba
inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed
Shein, zitafanyika leo katika viwanja vya Jamuhuri mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa
habari mjini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Nchimbi, alisema tukio hilo la
kihistoria litafanyika kuanzia saa sita mchana na kuwaomba wananchi kujitokeza
kwa wingi kushuhudia.
Pamoja na viongozi hao, tukio
hilo pia litahudhuriwa na Marais wastaafu wa Muungano na Zanzibar, viongozi wa kitaifa na watendaji
wakuu, viongozi wakuu wastaafu, Maspika wastaafu, Mabalozi na wawakilishi wa
taasisi za kimataifa, taasisi za kidini, taasisi zisizo za kiserikali na
wamiliki wa vyombo vya habari.
Alisema kutakuwepo na makundi
mbalimbali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo ni pamoja na
wafugaji, wakulima, wavuvi, wanawake, vijana, wazee, wachimbaji madini wadogo,
walemavu na wasanii.
Aidha, alisema ulinzi na
usalama utakuwepo na utaendelea kuwepo.
0 Comments