Na Mwanajuma Abdi, Dar es
Salaam
Serikali ya Tanzania imesema
zoezi la ufangaji mitambo ya video conference ya kurahisisha mawasiliano na
nchi za jirani na kimataifa bila ya kutumia gharama za kusafiri, limekamika
katika Ofisi ya Rais Ikulu na mikoa minne ya Zanzibar.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, aliyasema hayo jana wakati wa
uzinduzi wa mradi wa video conference, uliofanyika ukumbi wa mikutano wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar
es Salaam.
Uzinduzi huo ulijumuisha mikoa
ya Mwanza, Rukwa, Pwani, Dodoma, Mtwara na Shinyanga, ambapo Waziri Mnyaa
alizungumza moja kwa moja na mikoa hiyo kupitia video conference kwa kuonana
‘live’ kama wapo katika ukumbi wa mkutano na kufanyiana mahojiano.
Alisema mkandarasi tayari
ameshakamilisha zoezi hilo visiwani Zanzibar, ambapo hatua zinazoendelea ni
kuwapatia mafunzo watendaji wa serikali ili kuweza kuitimia katika kurahisisha
mawasiliano.
Aidha, alisema serikali
itahakikisha ifikapo Oktoba mwakani katika ofisi zote za halmashauri, wilaya, hospitali,
vituo vya polisi zitaunganishwa katika huduma hiyo ili kurahisisha mawasiliano.
Alisema katika kuhakikisha
matumizi ya Tehama yanakuwa kwa kasi hasa katika ofisi za serikali, wizara imefunga mitambo hiyo katika
ofisi zote mbili ya Dar es Salaam na
Dodoma, makao makuu ya mikoa 21 ya Tanzania Bara, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Tamisemi.
Alifahamisha huduma ya
teknolojia ya video conference ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji
wa majukumu ya serikali, ambapo utumiaji huo unaweza kuwasaidia viongozi au
watendaji na watalaamu kufanya kazi kwa kushirikiana na kuwasiliana na wadau
wengine katika sehemu zao za kazi bila ya kulazimika kusafiri kutoka sehemu
moja kwenda kwengine.
Alisema ujenzi wa mkonge wa
taifa wa mawasiliano unaotekelezwa na wizara yake, unasanifu mradi wenyewe,
utekelezaji unafanywa kwa awamu tano, ambapo ya kwanza na ya pili zimekamilika
na kutumika tokea mwaka 2012, ikiwa na jumla ya kilomita 7,560 ambao umechangia
kuleta mageuzi makubwa katika matumizi ya Tehama nchini.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa mradi
wa mafunzo kwa njia ya mtandao, Charles Senkondo, alisema teknolojia hiyo
imeongeza kasi ya uchumi na kijamii, ambapo vituo zaidi ya 120 vimeunganishwa
duniani, ambapo nchi nyingi za Afrika bado huduma hiyo lakini kwa Tanzania
imewahi.
0 Comments