6/recent/ticker-posts

Viongozi wa Wilaya watakiwa kupiga vita wizi wa karafuu

 Mkurugenzi wa mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Ali Suleiman akizungumza na viongozi  na Masheha wa Wilaya ya Kati katika mkutano wa kuhamasisha kilimo cha Karafuu Zanzibar  (kati)  Mkuu wa Wilaya kusini Vuai Mwinyi na  (kulia) Meneja  wa Mawasiliano wa ZSTC Ali Mohd.
 Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja Vuai Mwinyi akiwakaribisha viongozi wa Shirika Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) kuzungumza na viongozi wa Wilaya na Masheha wa wilaya yake  katika ofisi ya Dunga.


 Baadhi ya Masheha wa shehia za Wilaya ya Kati Unguja wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Karafuu (hayupo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika Ofisi ya Wilaya Dunga.

Mkuu wa Wilaya Kusini Unguja Khamis Jabir akitoa shukrani zake kwa viongozi wa Shirika la ZSTC waliofika Ofisini kwake Makunduchi kuzungumza na uongozi wa Wilaya kuhusu zao la Karafuu

Picha Na Ramadhan Ali -Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhan Ali, Maelezo

Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Zanzibar Ndugu Ali Suleiman Mussa amewataka viongozi wa Wilaya kupiga vita vitendo vya wizi wa Karafuu ambavyo vinapelekea hasara kubwa kwa wakulima  wa Karafuu na wananchi wanaofanya biashara ya kukodi zao hilo.

Alisema Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) limepokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa mashamba ya Karafuu na wale wanaokodi   kuibiwa karafuu zao hasa wakati wa usiku na baadhi ya wezi huikata mikarafuu mizima na kuihamisha maeneo mengine kwa ajili ya kupata karafuu.

Mkurugenzi Ali alieleza hayo alipokutana na  kufanya mazungumzo na Wakuu wa Wilaya sita za Unguja  na maafisa wao kwenye  Wilaya zao kuhusu  kadhia ya wizi wa karafuu na hatua nyengine ambazo Shirika linapanga kuchukua  kuimarisha zao la Karafuu.

Alieleza kuwa wizi wa karafuu unachangiwa na baadhi ya watu wanaonunua karafuu  mbichi kutoka kwa watu  wengine  jambo ambalo ni kosa kwani  ZSTC ndio Taasisi pekee  iliyopewa  jukumu la kununua karafuu kutoka kwa wananchi

Alisema vitendo hivyo vinarudisha nyuma juhudi za Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuliimarisha zao la Karafuu ambalo  ndio zao kubwa la biashara linaloingiza  fedha nyingi za kigeni.


 Aliwaeleza Viongozi hao kuwa ZSTC limekuwa likiwakopesha  fedha na vifaa vyengine vya kuchumia karafuu wadau wa  zao hilo na ikiwa vitendo vya kuibiwa karafuu havitadhibitiwa  watashindwa kurejesha mikopo yao na kuliingizia Shirika hasara kubwa.

Alitanabahisha  kuwa lengo  la Serikali la kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ni kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo  unaongezeka kama ilivyokuwa katika miaka  ya 1800 ambapo Zanzibar ilikuwa ikiongoza kwa uzalishaji wa Karafuu Duniani wakati sasa ipo nafasi ya nne.

“Historia inaonyesha kuwa Zanzibar ilifikia kuzalisha zaidi ya tani  35,000 kwa mwaka na hivi sasa tunazalisha chini ya tani 5,000 kwa mwaka,” alisema Mkurugenzi wa Mfuko wa Karafuu.

Akizungumzia suala la kuimarisha  ubora wa karafuu za Zanzibar, Mkurugenzi Ali amewataka viongozi wa Wilaya kushirikiana na Masheha kuhakikisha karafuu zinaanikwa katika majamvi ambayo Shirika  linauza na kukopesha   wachumaji wa Karafuu.

Alisema pamoja na uzalishaji mdogo wa Karafuu hapa nchini bado Karafuu za Zanzibar zinaonkena kuwa bora zaidi  kwenye soko la Dunia ukilinganisha na karafuu kutoka nchi nyengine na alitaka sifa hiyo iendelezwe kwa kuzishughulikia katika misingi sahihi wakati wa kuanika.

“Sio sahihi karafuu kuzianika barabarani, kwenye mabati ama vyombo vyengine kwa sababu  zinapungua ubora wake wakati  juhudi za kuzitafutia karafuu za Zanzibar uthibitisho zanafanywa,” alisisitiza Mkurugenzi  Ali Suleim Mussa.

Katika kudhibiti wizi wa karafuu na kuliimarisha zao hilo Mkurugenzi wa Mfuko wa Karafuu alisema Serikali imeamua kuanzisha mpango wa kufanya usajili kwa watu wenye mikarafuu na wanaokodi karafuu kwa lengo la kuwatambua na kurahisisha kuwapatia misaada wanapohitaji.

Mwanasheria wa Shirika la la Biashara la Taifa Zanzibar Ndugu Ali Hilal aliwakumbusha viongozi wa Wilaya kuwa  kukata mikarafuu kwa ajili ya kuiba  karafuu ama kwa matumizi mengine  ni kwenda kinyume na sheria namba 2 ya mwaka 2014 ambayo inakataza  kuihujumu mikarafuu na atakaebainika kufanya vitendo hivyo anawajibika kupelekwa katika vyombo vya sheria.#

Aliwashauri viongozi wa Wilaya kushirikiana kwa karibu na Kamati zao za  ulinzi za Wilaya, masheha na polisi shirikishi  kupambana na vitendo vya kukata mikarafuu ili visiendelee.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’  Mzee Haji Makungu Mgongo na wa Wilaya Kusini Ndugu Khamis Jabir waliahidi kushirikiana na Shirika la ZSTC kupambana na  tatizo la wizi wa karafuu  na kukatwa mikarafuu kwani wanaamini vitendo hivyo vinaathiri uchumi wa Zanzibar. 

Post a Comment

0 Comments