6/recent/ticker-posts

Hafla ya uzinduzi wa Mashindano makubwa ya Qur-an Tukufu kwa Mabara yote Ulimwenguni


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na waumini  wa Dini ya kiislamu katika hafla ya uzinduzi wa Mashindano makubwa ya Qur-an Tukufu kwa Mabara yote Ulimwenguni kwa mwaka 2026 yanayoandaliwa na Taasisi ya Al-hikman Foundation katika Ukumbi wa Hoteli ya Kilimnjaro Dar es Salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Taasisi ya Al-hikman Foundation kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kueneza ya Dini ya Kiislamu kwa misingi ya elimu, hekima na maadili mema. 

Ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa mashindano makubwa ya Qur-an tukufu kwa mabara yote Ulimwenguni kwa mwaka 2026 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kilimnjaro jijini Dar es Salaam. 

Amesema ni jambo la faraja kuona Taasisi ya Al-hikman Foundation inatoa huduma mbali mbali za kijamii zinazogusa maisha ya watu bila ya kubagua dini wala kabila wakiamini kuwa binaadamu wote ni sawa na wanastahiki kupatiwa huduma kwa haki na usawa. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa kumekuwa na muitikio mkubwa wa Taasisi mbali mbali kuwekeza katika mambo ya kheri yanayotoa hamasa kwa vijana kuendelea kukisoma na kukihifadhi kitabu kitakatifu cha Qur-an abacho pia huwafundisha mfumo mzima wamaisha yao ya dunia na akhera. 

Aidha, amewataka wahitimu na washindani wote wa Qur-an kutambua kuwa ushindi sio kupata cheti na zawadi bali ni kuyazingatia mafundisho ya Qur-an na mafundisho ya Mttume Muhammad (S.A.W ) ili kupata radhi za Allah (S.W ). 

Mhe. Hemed amewakumbusha waumini wa dini ya kiislamu kuwa mwenye kushikamana na Qur-an tukufu na kuusambaza ujembe uliomo ndani ya kitabu hicho kitakatifu kwa waumini wengine  atalipwa ujira mkubwa na Allah (S.W ) hapa na kesho Akhera. 

Mhe. Hemed ameisihi jamii kuendelea kuimarisha maadili mema, kudumisha amani na mshikamano, maelewano pamoja na kupambana dhidi ya mmong'onyoko wa maadili kwa kutumia mwanga wa Qur-an tukufu. 

Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ifikapo tarehe Mosi mwezi Machi 2026, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kushuhudia mashindano hayo na kupata fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 

Hata hivyo ametowa wito kwa wadau mabli mabali, Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi kuendelea kudhamini na kuiunga mkono Taasisi ya Al-hikman Foundation ili mashindano hayo yawe endelevu na yenye kuleta athari chanya kwa vijana na jamii yote kwa ujumla. 

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Al-hikma Foundation na Mwanzilishi wa Mashindano hayo Sheikh Nurdin Kishki amesema mashindano hayo yalianzishwa mnamo mwaka 1998 yakiwa na lengo la kuwafundisha na kuwahifidhisha Qur-an wanafunzi wa Al-hikma Foundation na kukuwa hadi kufikia mashindano ya Mabara yote Ulimwenguni jambo ambalo linaendelea kukitangaza kitabu hicho kitakatifu cha Allah (S.W ). 

Sheikh Kishki amefahamisha kuwa kwa mwaka 2026 Mshindi wa kwanza wa mashindano hayo atazawadiwa fedha taslim shilingi Milioni thelathini (30) zilizotolewa na mdhamini mkuu wa mashindano hayo Benki ya watu wa Zanzibar ( PBZ ).

Sheikh Kishki amezitaja nchi zitakazoshiriki katika mashindano hayo kuwa ni Canada, Mexico, Barbados, Guyana, Sweden, Ujerumani, Uengereza, Newziland, Australia, Indonesia, Kazakhstan, Visiwa vya Yurion, Zambia, Uganda, Kenya, Tanzania, Zanzibar na wenyeji Taasisi ya Al-hikma Foundation. 

Mpema Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Eduard Mpogolo amesema Mashindano ya Qur-an yanayoandaliwa na Taasisi ya Al-hikmah Foundation yana umuhimu mkubwa katika kutoa mafundisho na miongozo itokanayo na maneno matukufu ya Mwenyezi Mungu yanayowajenga wananchi kiimani pamoja na kuwa na hofu ya Allah. 

Mpogolo amesema mashindano hayo yamekuwa ni chachu ya kuwajenga wananchi kimaadili, kuwa na Umoja na Mshikamano katika jamii na Taifa kea Ujumla. 

Kwa upande wake Mkurugenzi huduma za kiislam kutoka Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ ) ambao ndio Mdhamini Mkuu wa Mashindano hayo ndugu Rajab Mohammed Ramia amesema PBZ imekuwa ikidhamini mashindano hayo kwa miaka  minne (4) mfululizo wakiwa na nia thabiti na matarajio ya kuendelea kudhamini mashindano hayo . 

Mkurugenzi Ramia amesema Benki ya PBZ imekuwa ikishirikiana na kufanya kazi za kifedha na wadau mbali mbali hivyo katika kuendeleza mashirikiano hayo   wataendelea kudhamini mashindano kwa lengo la kukinyanyua kitabu kitukufu cha Qur-an, kulinda maadili mema na kuimarisha Umoja na mshikamano kwa Watanzania.

Post a Comment

0 Comments