NA FAUZIA MUSSA
Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar (UTAHIZA) umeeleza kuwa zoezi la utoaji wa visa kwa mahujaji wa Hijja ya mwaka 2026 litaanza rasmi Februari nane 2026 na kufungwa Machi 20 mwaka huu, huku ukisisitiza kuwa hakuna nyongeza ya muda itakayotolewa baada ya tarehe hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Hijja wa UTAHIZA, Mohamed Mansour, alisema hatua hiyo ni ya mwisho kabisa katika maandalizi ya Hijja, na hujaji yeyote atakayeshindwa kukamilisha taratibu za visa ndani ya muda uliopangwa hataweza kwenda Hijja kwa mwaka huu.
Alisema kuwa kufikia Februari mosi 2026, zoezi la kufunga mikataba ya makaazi ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia litakuwa limekamilika, hatua ambayo ni muhimu katika maandalizi ya safari ya Hijja.
Aidha, Mansour alieleza kuwa kwa sasa kuna zoezi la upimaji wa afya kwa mahujaji wote, linalosimamiwa na taasisi wanachama wa UTAHIZA, ambapo mahujaji wanapelekwa katika Hospitali ya Alrahma Kwa Upande wa Unguja na Amal Hospital Kwa Upande wa Pemba kwa mpango maalum.
Alosema upimaji huo ni sharti la Hijja ya mwaka huu, linalolenga kubaini hali ya afya za mahujaji mapema ili kuhakikisha wanasafiri wakiwa na afya njema na bila usumbufu.
“Huu ni utaratibu wa lazima. Mahujaji wote wanapaswa kushiriki bila wasiwasi, kwani lengo ni kuhakikisha usalama na ustawi wao wakati wa ibada ya Hijja,” amesema Mansour.
UTAHIZA pia imetoa onyo kali kwa Waislam dhidi ya tabia ya kusubiri hadi baada ya Ramadhani kufanya maamuzi ya kwenda Hijja, ikieleza kuwa mfumo huo umepitwa na wakati kutokana na ratiba mpya za mamlaka za Saudi Arabia.
Mansour alisema kuwa mtu yeyote atakayeshindwa kukamilisha kujiandikisha au malipo yake kwa wakati ataandikishwa moja kwa moja kwa Hijja ya mwaka ujao kwani maandalizi ya Hijja huanza mapema mara baada ya msimu wa Hijja uliopo.
Kwa msingi huo, UTAHIZA imetoa wito kwa Waislam wote wenye nia ya kwenda Hijja mwaka 2026 kujiandikisha mara moja, ikibainisha kuwa muda uliobaki ni mwezi mmoja na siku 20 tu kabla ya kufungwa kwa mfumo wa utoaji wa visa.
“Tunasihi sana Waislam wasisubiri dakika za mwisho. Nafasi ni chache na muda ni mfupi,” amesema Mansour.
UTAHIZA imewahakikishia Waislam kuwa iko tayari kutoa ushauri na maelezo ya kina ili kuhakikisha maandalizi ya Hijja yanafanyika kwa utaratibu, utulivu na usalama.
.jpeg)

0 Comments