6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA FEDHA AIMWAGIA SIFA TADB


Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.) kulia, akipokea  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, ya kipindi cha miaka 10 tangu ianzishwe mwaka 2015-2025, kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Frank Nyabundege,  katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

(Picha na KItengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-Dodoma

Na Benny Mwaipaja, Dodoma


Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.) ameimwagia sifa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ufanisi mzuri wa uendeshaji na kuchagiza maendeleo jumuishi na endelevu  yanayochochea mageuzi ya sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda vinavyochakata mazao ya kilimo nchini.

Mhe. Balozi Omar ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki hiyo ukiongozwa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Bw. Frank Nyabundege na kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Squire, jijini Dodoma.

Mhe Balozi Omary aliipongeza TADB kwa taarifa nzuri iliyoonesha safari ya mafanikio ya Benki, mwenendo mzuri wa mizania ya fedha na matokeo makubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo hususani katika uwekezaji wake kwenye uendelezaji wa viwanda vya kilimo, mifugo na uvuvi.

Aliishauri Benki hiyo kuelekeza mipango na mikakati yao katika kuendeleza mazao mengine ya chakula na ya biashara yenye thamani kubwa zaidi katika soko la Kimataifa ili wakulima waweze kunufaika zaidi na sekta hizo za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu ikiwemo ufugaji wa nyuki.

Aidha, Mhe. Balozi Omary aliahidi kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na TADB katika utekelezaji wa mkakati wake wa muda wa kati ili kuongeza tija ya sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi.

Akiwasilisha taarifa zake za fedha na mkakati wa Benki wa kipindi cha muda wa kati (2025-2030), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Frank Nyabundege, alisema kuwa TADB imekua kwa kasi kutoka kuwa na amana ya shilingi bilioni 362.8 (mwaka 2021) hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 (mwaka 2025).

Alisema kuwa kupitia ufanisi huo wa uendeshaji, TADB imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.3 ikinufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi zaidi ya milioni 1.9 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015.

Aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha, kwa kuiwezesha Benki kutimiza malengo yake kwa kuipatia mtaji jambo linaloonesha utashi wa kisiasa na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuikuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Bw. Nyambudege aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuendelea kuiwezesha Benki hiyo kimtaji Kupitia bajeti kuu ya Serikali pamoja na kuidhamini ili iweze kuyafikia Masoko ya Kimataifa yanayokopesha fedha kwa ajili ya kuwakopesha wakulima.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ally Munde, na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TaDB.
 

Post a Comment

0 Comments