Habari za Punde

MAALIM KHALFAN - JUHUDI ZAKE ZA KUTETEA HAKI NA UMOJA HAZITOSAHAULIKA

.Maalim Khalfan... Alikuwa mwalimu wa walimu,
Chem chemu iliyowasaidia wengi haipo tena

Ni pengo kubwa kwa Watu wenye Ulemavu Zanzibar
.
Juhudi zake za kutetea haki, umoja hazitasahaulika.

MAKALA HII IMEANDIKWA NA MUANDISHI SALIM SAID KATIKA GAZETI LA ZANZIBAR LEO.

MAALIM Khalifan Hemed Khalifan, sasa hayupo tena . Ni kwa sababu ya uwezo wa Mungu ya kumuhitaji atangulie mbele ya haki. Lakini wengi wataendelea kumkubuka kutokana na mengi mema aliyowatendea wazanzibari hasa jamii ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar. Yeye alikua na juhudi za mfano katika kuasisi na kuendeleza utetezi wa haki za watu wa jamii hiyo hapa Zanzibar na Dunia kwa jumla. Katika Makala haya Mwandishi Salim Said Salim, pamoja na mambo mengine anaelezea sifa za Maalim Khalfan aliyefariki mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzikwa katika Makaburi ya Mwanakwerekwe Zanzibar.


Maalim Khalfan. Ni jina lisiotaka maelezo zaidi Zanzibar kuelewa ni nani mtu huyu na kwa kiwango kikubwa katika nchi jirani na nje na hata Umoja wa Mataifa.

Aliyekuwa akitambulika kwa jina hili ni ndugu yetu, kaka yetu, mzee wetu, sahiba na maalim wetu, Khalfan Hemed Khalfan, sasa hatunaye tena. Aliitwa na Mola wake Jumamosi iliyopita na akaitika na kutuachia majonzi, huzuni na masikitiko yasioelezeka kwa kauli wala maandishi. Laiti kama moyo ungelikuwa unasema basi ingekuwa kielelezo kinachofaa cha kumueleza marehemu huyu.

Lakini Mola halaumiwi na majaaliwa ya mitihani ya maisha katika ulimwengu huu na ikikuta shukuru, kama vile na sisi tunavyopaswa kushukuru kwa kutokuwa naye Maalim Khalfan. Lakini japokuwa hatunaye kimwili, bado tunaye kiakili na moyoni na matunda ya elimu yake kama mwalimu hayafutiki katika maisha ya mamia ya watu aliowasomseha skuli mbali mbali na maelfu aliowatumikia katika nyanja mabli mbali na hasa ile ya watu wenye ulemavu.

Kwa mama watoto wake na dada yangu Bi. Ashura niliyeelewana naye tokea wadogo, tukiwa chuoni na baadaye kuwa naye karibu zaidi kama ilivyokuwa kwa marehemu na famlia yake, watu wenye ulemavu wa Visiwani na wengine wengi ndani na nje ya Zanzibar ninawaambia sote tumeondokewa na tupo kwenye majozi. Tushukuru kwani kazi ya Subhana haina mjadala ila tuendeleze mema aliyoyafanya maalim wetu, mwalimu wa wote na malimu wa walimu .Ni kazi ya Mola na hatuna njia nyengine ila kumuombea toba ma maghfira.

Hapana ubishi Maalim Khalfan alikuwa muungwana aliyetimia, mtu mwenye hekima, busara na murua, mbunifu,kiumbe aliyekua na ustahamilivu na subra ,mtu mwenye kujituma na mfano kwa jamii juu ya umuhimu wa binaadamu kutokata tama na zaidi ya yote kujiamini na kuzipokea rehma za Mola wetu kama zinavyotuteremkia.

Ni mtu aliyewafundisha wengi, ndani na nje ya skuli na alikuwa kiongozi mahiri na wa kupigiwa mfano wa shughuli za kijamii, na hasa kwa masuala ya ulemavu. Maalim Khalfan, aliyeiaga dunia tarehe 28 Machi ametuacha mkono, lakini ametubakishia hazina yenye historia iliotukuka na inayofaa kupigiwa mfano na jamii ya hivi sasa na vizazi vijavyo.

Maalim Khalfan alikuwa darasa la kuchota mengi, kisima kiliokuwa hakikauki na chemchemu iliokuwa ikinawiri.Ninakiri nilichota mengi na leo ninabaki kama yatima na ninajiuliza nitanenda wapi kupata ushauri wakati Maalim nilimtegemea na nataasaf kusema kudeka kwake hayupo? Wengi ambao hawakubahatika kufundishwa na Maalim Khalfan skuli walijifunza mengi kutoka kwake katika mikusanyiko mengine, kama mikutano, warsha ,semina na makongamano.

Alikuwa mwalimu wa walimu aliyejuwa mahitaji ya aliowafundisha au kuwahutubia na alizifahamu njia za kupita za kufikisha ujumbe kwa lugha mwanana iliojali maingira na umti aliokuwa akizungumza nao.

Maalim Khalfan ambaye ni muanzilishi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) katika mwaka 1985 na Mwenyekiti wa kwanza wa umoja alijituma sana kwa dhana ya kuwa na umoja huo kuanza kukubalika Visiwani. Hii ilitokana na watu wengi wenye ulemavu na hata viongozi katika serikali kuona kuwa alikuwa katika ndoto ya aina yake , si ya asubuhi, mchana wala usiku.

Suku moja nikiwa naye pamoja katika mazungumzo yetu ya kila jioni nje ya nyumba yake hapo Kisiwandui, jumba namba 8 la Michenzani , na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kimo na Mifugo na baadaye Waziri Kiongoziwa Zanzibar na Makamo wa Rais wa Tanzania, marehemu Dk.Omar Ali Juma, nilimuambia Maalim Khalfan kwamba nilikuwa naona kama vile wana jamii na hasa watu wenye ulemavu hawaelewi tulichokuwa tunakusudia kukifanya.

Lakini Dk.Omar ambaye alikuwa mtu wa karibu sana na MaalimKhalfan na kumtembelea karibu kila siku , hata alipokuwa Waziri Kiongozi, alisema kwa wakati ule kila safari Zanzibar, hata ya masafa mafupi, ilikuwa lazima ichukuwe muda mrefu, kutokana na vikwazo vya watu kutojiamini na kutokuwa tayari kupokea kitu kipya.

“ Hata tunapopata mbegu za kisasa za mazao au ng'ombe ambazo zimefanyiwa utafiti basi huwa kazi pevu kwa watu kuziamini”, alisema marehemu Dk. Omar.

Hapo Maalim alisema huku akitabasamu : “ Nilitegemea mambo kuwa magumu zaidi kuliko yalivyojitokeza. Tusikate tamaa , kumbuka jiwe hukata kamba. Jee na wewe ukiwa unatafuta habari na kupambana na vikwazo unawacha kuifuatilia hio habari au ndio unazidi kuwa na shauku ya kuipata? Tutafika, lakini lilio muhimu ni kwenda na sio kusimama na kusikitika”, aliniambia.

Kikundi cha watu wasiozidi sita tuliokuwa tunafanya nao kazi ya kutayarisha katiba , kanuni na mambo mengine ya UWZ kabla ya kuomba usajili nacho kilionekana kukata tamaa, lakini kikashajiishwa na Maalim Khalfan aliyekuwa akishikilia kuwa itawezekana na patakuwepo mafanikio. Na kweli imewezekana na yamepatikana mafanikio na leo UWZ inajulikana kila pembe ya dunia na kutambulika kama miongoni mwa taasisi bora za kiraia na zenye mipango mizuri inayowahusu watu wenye ulemavu katika Bara la Afrika na Asia.

Maalim Khalfan sio tu alisimamisha na kuiendeleza UWZ bali alisaidia kuundwa na kuimarisha jumuiya kama hizo nyingi Afrika, Asia na Amerika ya Kusini ambapo aliitwa kutoa ushauri na hata kuaidia kuwatengenezea katiba na kanuzi za umoja.Hiui ilepelekea kuwa mwaklishi wa watu wenye ulemavu wa Bara la Afrika katika jumuiya za kimtaifa, ikiwa panoja na mikutano ya Umoja wa Mataifa. Alikuwa mjumbe wa Jumuiya ya Kimataifa ya watu Wenye Ulemavu (DPI).

Sikushangaa wakati wa mkutano mmoja wa kimataifa wa watu wenye ulemavu wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika uliofanyika Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1990 kwa mama mmoja kutoka Mauritius, Zeenat, alipomueleza Maalim Khalfan kama “ Kichwa cha masuala ya ulemavu Bara la Afrika”.

Juhudi zake na moyo wa kujituma, pamoja na kushirikiana na wenzake kama aliyekuwa Makamo wake Mohammed Kassim na Katibu wa UWZ, Bi Mwandawa na ubunifu wake wa miradi mabli mbali ya maendeleo kwa watu wenye ulemavu Unguja na Pemba ndio kulionipelekea wakati wote tokea kuanzishwa kwake hadi leo kuwa karibu na kuutumikia umoja kama mmoja wa washauri wa UWZ na mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa UWZ hadi sasa. Nimekuwa nikiona fakhari na bahati ilioje kufanya kazi na Maalim Khalfan ambaye nimesoma mengi kiutoka kwake.

Sitamshau kama vile ambavyo watu wenye ulemavu na wanafunzi wake watavyomkumbuka muungwana huyu aliyejali zaidi wenzake kuliko nafsi yake.

Kwa ushauri wake na viongozi wengine wa UWZ nilianzisha na kusimamia gazeti la umoja huo liitwalo Nyota Njema ambayo hadi sasa inang’ara katika kuelimisha watu wenye ulemavu na jamii juu ya masuala mbali mbali ya ulemavu.

Maalim Khalfan hakunivutia mimi tu na wenzangu wengi hapa Visiwani, bali alikuwa mtu aliyejijengea heshima na kukubalika kimataifa. Siku moja nikiwa Sweden, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje alipoelewa kuwa ninatoka Zanzibar suala lake la kwanza lilikuwa kama nilikuwa ninamuelewa na kama niliwahi kukutana na Maalim Khalfan.

Nilipomueleza kuwa mimi na marehemu tulikuwa chanda na pete aliniamabia: “Jihesabu kuwa mmoja wa watu waliobahatika”. Nilipotaka ufafanuzi alinipa maelezo yalionithibitishia kwa mara nyengine tena uwezo mkubwa na kipaji alichokuwa nacho marehemu cha kupeleka ujumbe hata kwa walioziba masikio na kufumba macho.

Aliniambia siku moja marehemu alialikwa katika mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Mataiafa katika mji wa Stockholm, Sweden, kuzungumzia shida na matatizo ya watu wenye ulemavu, hasa katika Bara la Afrika na nchi zinazoendelea na matarajio yao kwa serikali zao na jamii.

Kabla ya kuwasilisha waraka wake, marehemu alifungua mkoba na kutoa vipande vya vitambaa vyeusi na kuwagawia washiriki na kuwataka wavifunge kuziba macho yao. Aliwaomba washiriki walipomaliza kufunga vitambaa wafumbe macho na taa zizimwe kwa dakika moja. Zilipoashwa aliwaambia washiriki hicho walichokibaini kwa nusu dakika na kuwapa shida ndio maisha ya kila siku ya mtu asiyeoona.

Wajumbe walitokwa na machozi na baadhi yao kukiri kuwa walipata somo liliowafungua macho juu ya maisha ya watu wasioona na wenye ulemavu kwa ujumla. Alipomaliza hotuba na kukaribisha masuali wajumbe wote walisimama na kumpigia makofi kuonyesha jinsi walivyoheshimu maelezo yake yaliojaa elimu, hekima na busara. Huyu ndiye Maalim Khalfan nimjuaye na wengi tuliyemfahamu.

Maalim Khalfan alikuwa sahiba wangu wa karibu sana, kaka yangu na mwana wa familia baaada ya familia yangu kuamua mmoja wetu (mdogo wangu) kuchangia damu na familia yake na hili limepeleka tuelewane zaidi kama chanda na pete.Alikuwa wangu na nilikuwa wake na kuondoka kwake katika dunia hii kongwe yenye mambo mapya kila siku kumeninyima mmoja wa walimu nitaowaheshimu na kuwaenzi maishani mwangu kote.

Nimechota mengi kutoka kwake ambayo yamenisaidia kimaisha kama yalivyowasaidia mamia, baadhi yao wakiwa mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Muungano, vyama vya siasa,mashirika ya hapa nchini na nje na jumuiya ya kimatafa.

Ujasiri, kujiamini na kutokata tamaa kwa Maalim Khalfan katika maisha kulipelekea kutengenezwa filamu maalum ya video inayoonyeshwa nchi mbali mbali juu ya maisha yake.Filamu hii inatumiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu katika nchi mbali mbali duniani wanaofanya utafiti juu ya masuala ya watu wenye ulemavu .

Maalim Khalfan ambaye alizaliwa mwaka 1942 wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikiwa vimepamba moto alipata elimu yake ya msingi Bumbwini na kumbukumbu zinaonyesha kuwa mmoja wa wanafunzi aliyefaulu vizuri katika historia ya shule hio.

Alikuwa hakamatiki kwa mbio za masafa mafupi, kama alivyokuwa baadaye hakamatiki kwa busara na hekima.Wenzake wa zama zile walimuita “paa” kwa jinsi alivyokuwa akitimua mbio wakati akiwa katika skuli ya sekondari ya H.H. Agakhan (sasa jumba la Tasisi ya Kiswahili) na kusifika kwa umahiri wake kwenye mjadala na riadha. Wakati akiwa anamaliza kidato cha kwanza ndio alipata mtihani mkubwa wa maisha yake wa ulemavu wa viungo baada ya kuchomwa na msumari na kwanza kupata ugonjwa wa peopo punda (tetanus).

Marehemu ameondoka duniani akiwa ameuacha Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar imara na vitega uchumi kadha , lakini kubwa zaidi ni mchango wake wa kuelimisha jamii juu ya masuala ya ulemavu na kusaidia kutetea haki zao katika jamii ambayo siku za nyuma iliwaona watu wenye ulemavu kama wasiokuwa na uwezo na mzigo kwa jamii.

Maalim Khalfan, kaka yetu, rafiki yetu, mzee wetu na mwalimu wetu ndani na nje ya darasa hatunaye tena. Ameitwa na Mola wake na kuitika. Tumeshalilia na kumshukuru Mungu ambaye halaumiki kwa kukipumzisha kiumbe chake na maisha ya hapa duniani. Njia nzuri ya kumkumbuka ni kujaribu kuwa kivuli chake .

Kwa familia ya marehemu , na hasa dada yetu Bi Ashura, watu wenye ulemavu na Wazanzibar kwa jumla, nasema tusilie bali tuendeleze kwa kauli na vitendo kazi nzuri aliyoifanya marehemu.


Tunamuomba Mola amlaze mahali pema peponi, ampe mghfira na rehma Maalim wetu Khalfan Hemed Khalfan! INNA LILAHI WA INNA ILAIHI RAJI'UNA!


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.