Habari za Punde

WANANCHI CHAGUENI DK. SHEIN

Ni hodari
Muadilifu, muaminifu, mpenda uwajibikaji
Muendeleza Mapinduzi, Muuungano
Na Omar Said

UMUHIMU wa kuchaguliwa kiongozi aliye muadilifu, muaminifu na muwajibikaji ni wa kuzingatiwa na wapiga kura wote nchini kwa maslahi ya nchi na wananchi wake.

Nimnukuu Mgombea urais wa Zanzibar kwa tikeki ya Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, amewaomba wananchi wa Unguja na Pemba kumchagua yeye, kwani ndiye anayestahili kuiongoza Zanzibar, kutokana na uaminifu na uadilifu wake wa kuwatumikia wananchi.

Amesema kuwa Ikulu ni mahali patakatifu panapostahili kuongozwa na kiongozi wa yeye Dk. Ali Mohammed Shein, kwani anatambua na kuzifahamu kikamilifu shida na matatizo ya wananchi katika sehemu mbalimbali nchini, hivyo wananchi ni lazima wazingatie kikamilifu kauli ya mgombea huyo, kwa maslahi na mustakabali wa Zanzibar.

"Ndugu wananchi nawaombeni mnichague mimi Dk. Ali Mohammed Shein, kwani Ikulu napaelewa kikamilifu kwa milango yote ya kuingilia na kuitokea, lakini kubwa Ikulu ni pahala patakatifu panapohitaji mtu makini na mahiri wa kufuatilia na kusimamia kazi na majukumu, lakini kubwa ni uadilifu na uaminifu wa kiongozi naye si mwingine ni mimi"amefahamisha Dk. Ali Mohammed Shein, huko Chwaka.

Alisema kuwa kutokana na kulelewa ndani ya Chama cha Mapinduzi kwa muda mrefu na anafahamu kikamilifu kwamba Ikulu ni pahala patakatifu panapostahili kiongozi wa aina yake, kwa uaminifu na uadilifu wa kuwatumikia wananchi wa Unguja na Pemba, hivyo wananchi hawana budi kuhakikisha wanamchagua kiongozi huyo, ambaye katika nyadhifa alizoshika ameonesha kwa vitendo hali hiyo nchini.

"Chagueni kiongozi aliye muadilifu, muaminifu na muwajibikaji kwa kuwatumikia watu kwa maslahi ya watu wa Pemba na Unguja na Tanzania kwa jumla, kwani hakuna mgombea mwingine bali ni mimi Dk. Ali Mohammed Sheni"alisisitiza huku akishangiriwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni huko Chwaka, Wilaya Kati Unguja.

Dk. Shein aliongeza kwamba kwa nafasi kadhaa alizoshika katika taifa hili ana uzoefu wa kutosha katika kuwatumikia wananchi na anafahamu kwa ukamilifu funguo za kuingilia Ikulu, kwani Chama Cha Mapinduzi kina uzoefu wa miaka mingi, hivyo hakuna upinzani uliozoea jengo la Ikulu, kwa vile hawana ya kuwafanyia wananchi wa Unguja na Pemba.

Alifahamisha kwamba vyama vya upinzani havitaweza kuingia Ikulu kwa vile bado vyama hivyo havina viongozi waaminifu, watakatifu na waadilifu na wenye utashi wa uwajibikaji kama Dk. Ali Mohammed Shein, kutokana na uwezo, ujuzi na utaalamu mkubwa aliouonesha katika kazi na utekelezaji wake akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Ikulu wanakwenda watu watakatifu, waadilifu na wenye utashi wa uwajibikaji, hivyo mimi ninao uwezo na ujuzi wa miaka mingi, nipeni kura zote mimi, naomba kazi ya kuwatumikia naiweza ni muaminifu, muadilifu nimejiandaa kikamilifu kuitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwa maendeleo yetu sote"amekumbusha Dk. Ali Mohammed Sheni.

Aliongeza kuwa kwa kutambua hilo ni vyema wananchi wa Zanzibar pamoja na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kutambua umuhimu wa kumpa kura zote kwa kazi ya Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, ili aweze kuwapatia maendeleo endelevu, ambayo tayari Ilani ya CCM imewaandalia.

"Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo, imewaandalia kuwaletea mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa wananchi wa Unguja na Pemba ikiwemo Wilaya Kati, Kusini Unguja na kupitia sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, kilimo bora miundombinu ya barabara, maji safi na salama pamoja na makazi bora kwa umma wa Zanzibar.

Alikumbusha baadhi ya mambo yanayotarajiwa kuwa vipaumbele vyake mara akiingia Ikulu, Dk. Shein alisema kuwa atahakikisha wananchi walioishi kwa muda mrefu kwenye nyumba za maendeleo wanauziwa, kwa madhumuni ya kutekeleza azma ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwapatia makazi bora wananchi wa Unguja.

"Lengo la Mapinduzi ya Januari,1964 ni kuwapatia makazi bora na kwa mnasaba huyo nitahakikisha wananchi walioishi katika nyumba hizo kwa muda mrefu wanauziwa na mpango huo utakwenda pamoja na kuzifanyia matengenezo na marekebisho kadhaa nyumba, ambazo zinaonekana kuwa kwenye hali mbaya, kwa kushirikiana na wananchi, ambao watalazimika kuchangia kiasi kidogo cha fedha, ambapo kazi hiyo itafanywa kwa Unguja na Pemba"alifahamisha Dk. Ali Mohammed Shein, mgombea wa CCM.

Dk. Shein mgombea kwa tikiti ya CCM, alisema kuwa pindi akipata ridhaa ya kuingia Ikulu serikali yake itaendelea inandaa mazingira na utaratibu wa kuendeleza utoaji wa maeneo mbalimbali kwa ajili ya makazi mapya kwenye sehemu za Bambi, Wilaya Kati.

Dk.Ali Mohammed Shein, amejulisha kuwa serikali ijayo ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo anaamini CCM itashinda itakuwa inaandaa mazingira mazuri ya kuhakikisha kwamba utoaji wa dawa na chanjo unakuwa ni mpango endelevu, kwani huduma za afya zitaimarishwa kwa kupatiwa huduma za kumkinga mwananchi kwa maradhi mbalimbali.

"Kwani kinga ni bora kuliko tiba, hivyo tutafanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali na kuyapatia chanjo, kwa ajili ya kuwa na taifa la watu wenye afya nzuri"aliongeza Dk. Mohammed Shein, ambaye kitaaluma ni daktari wa maradhi ya binadamu.

Juu ya sekta ya elimu Dk. Shein alisema kuwa serikali yake pindi akichaguliwa kuiongoza Zanzibar siku chache zijazo, atahakikisha kuifanyia mabadiliko makubwa kwa kuzipatia vifaa vya maabara, kwa ajili ya skuli 37 za Unguja na Pemba, kwa dhamira ya kuwapatia elimu bora vijana wa taifa hili, ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia, ambapo baadhi ya vifaa vipo bandarini Unguja.

Alisema kuwa katika sekta ya elimu atahakikisha anaimarisha ujenzi wa maktaba mbalimbali, ambazo zitakuwa na vifaa vya kisasa, ambavyo vitaweza kuwasaidia wanafunzi wa Unguja na Pemba katika kukuza na kuimarisha taaluma zao.

"Serikali ijayo ya Chama Cha Mapinduzi itakayoongozwa na mimi itajenga vyumba maalumu vya kufanyia mtihani pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu ambapo moja itakuwa Charawe na nyingine tatu kwenye kituo cha Elimu Mbadala cha Binguni, ambazo zitasaidia kuimarisha elimu, ili kukidhi haja ya kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia"alifahamisha

Juu ya sekta ya Maji safi na salama Dk.Shein, alisema kuwa atahakikisha kwamba kazi kubwa ya utoaji wa huduma hiyo unakuwa wa kuridhisha, katika sehemu ambazo bado kuna matatizo ya upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu, kwa vijiji vya uroa Chwaka na Michamvi kwa kuchimba visima mbalimbali ambavyo vitakuwa vikitoa maji safi na salama yasiyo na chumvi.

"Pindi nikipata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar kuingia Ikulu nitahakikisha eneo la kijiji cha Cheju, litapatiwa huduma ya umeme, ili kuwezesha visima vilivyopo viweze kutoa huduma ya maji safi na salama kwa vile vya sasa vimekuwa vikikauka kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika"alidokeza Dk. Shein, huku ashangiriwa na halaiki ya wafuasi wa CCM.

Dk. Shein ambaye kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hupendelea kumwita 'Mr. Clean' alisema kuwa iwapo akichaguliwa atahakikisha utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa maeneo mbalimbali yanafikia wastani wa asilimia 80 kutoka sasa ambapo ni asilimia 60, hivyo kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu nchini.

" Iwapo nitachaguliwa serikali yangu itaongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, ili kuinua hali za wananchi wa Zanzibar na kupunguza shida ya kufuata huduma hiyo masafa marefu na pale yanapotoka kwa taabu yanapatikana kwa uhakika na kuondosha kabisa matatizo mbalimbali ya bidhaa hiyo muhimu" alisema Dk. Shein, ambaye amejijengea sifa kubwa ya kufuatana na mkewe Mama Mwanamwema.

Aidha Dk. Shein alisema kuwa upande wa miundombinu kama vile barabara nayo inatarajiwa kutokea makubwa kwa wananchi wa vijiji mbalimbali, kwani inakusudia kuzijenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami, kwa ajili ya vijiji vya Cheju, Jendele, Unguja Ukuu Kaebona, Mwajungoma, Mseweni, Tunguu, Umbuji, Uroa hadi Ukongoroni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.