Katika maeneo yasiyoruhusiwa
Na Said Abdul-rahman,Pemba
BARAZA la Mji Wete limepiga marufuku biashara ya samaki katika maeneo hasiyoruhusiwa.
Maeneo hayo ni kituo cha magari Wete na hoteli ya serikali Mtemani kutokana na kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi afisini kwake, Katbu wa Baraza la Mji Wete Hamad Khamis Hamad alisema kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara ya samaki kufanya kazi hiyo sehemu ambazo haziruhusiwi hali ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira.
Alisema Baraza la mji Wete limejitahidi kujenga masoko mengi ili kuwapatia wafanyabiashara sehemu nzuri za kuendeshea biashara zao hivyo wafanyabiashara wote wayatumie masoko hayo.
Hata hivyo, Katibu huyo alieleza kwamba baraza lake kwa kushirikiana na jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba litaendelea kuchukuwa hatua za kisheria kwa wale ambao watapuuza marufuku hiyo.
Akizungumzia soko lilioko bandarini Wete, alisema baraza lilitegemea kulifungua rasmi katika kilele cha sherehe za mwenge mwaka huu lakini kutoka na matatizo yaliojitokeza hawakuweza kulifungua.
Ameyataja matatizo hayo kuwa ni ukosefu wa choo na maji ambapo ameahidi kuchimba kisima ambacho kitaweza kutoa huduma ndani ya soko hilo
No comments:
Post a Comment