Habari za Punde

MATEMWE IKO SALAMA KIMAADILI

Na Mwanajuma Abdi

SHEHA wa Matemwe Haji Sheha amesema hakuna uvunjifu wa maadili katika kijiji hicho, kwani wameweka mipaka ili mambo yanayofanyika katika fukwe yaishie huko huko.

Akizungumza na gazeti hili, huko Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja, sheha huyo alisema kijiji chake kimeweka mipaka ya mambo kwani yanayofanyika ufukweni ni marufuku kuonekana juu ambako wananchi wanaishi.

Alisema kutokana na mipaka hiyo, kijiji hicho hakina tatizo kubwa la uvunjifu wa maadili kama vilivyo vijiji vyengine, ambako hufikia hadi kutokea uvunjifu wa amani.

Sheha huyo alifahamisha kuwa wanyeji wa kijiji hicho wameelezwa wazi kutokwenda ufukweni kuiga tamaduni za kigeni ambazo hazipendezi kwa jamii.

“Matemwe kuna tamaduni za wageni, ambazo sio mila za kizanzibari, lakini tumeweza kuwaeleza wananchi wanapokwenda huko desturi na tabia za huko wasizilete mitaani ili kuhofia uharibifu wa maadili kwa vijana”, alisema.

Alieleza baadhi ya viongozi wa dini walifika ofisini kwake na kumueleza kwamba watu wanatembea utupu kwenye pwani ya kijiji hicho, ambapo alikuwa mkali kwa kuwaambia wanafuata nini huko wakati hakuna msikiti wa kusalia?.

Akizungumzia upande wa wawekezaji, alifahamisha kuwa, wana maelewano mazuri na baadhi ya vijana wa kijiji hicho na wamekuwa wakinufaika na ajira kutokana na kukua kwa sekta ya utalii.

“Kasoro ndogo ndogo zipo, lakini sio kubwa za kuweza kutugawa”. Alieleza.

Alizishauri jamii zinazoishi katika maeneo ya wawekezaji hususani katika ukanda wa utalii wabakie na tamaduni zao kwani kujiingiza huko kunasababisha migogoro isiyo ya lazima.

Alisema watu wanapokwenda katika maeneo ya utalii watakutana na mengi kutokana na wageni kuingia nchini wakiwa na tamaduni zao, hivyo sio rahisi kuzifuata zile za Kizanzibari, na kuwataka wananchi kutojiingiza katika mazingira hayo kwa vile hakuna shughuli zinazowahusu kwenda huko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.