Habari za Punde

VIONGOZI MSIWACHEZE SHERE WANACCM - DK SHEIN

Asema wanachama muhimu wakati wote si kwenye uchaguzi tu
Na Mwantanga Ame

VIONGOZI wa CCM, wa majimbo, wilaya na mikoa wametakiwa kutosahau walikotoka kwa kuwacheza shere ya kuwakimbia wanachama wa chama hicho na badala yake wazitekeleze ahadi walizoziweka  ili waache kumbukumbu nzuri za utumishi wao.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, ambaye pia ni Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM wa  Jimbo la Kitope baada ya kufungua ukumbi wa mikutano ya jimbo hilo.

Dk. Shein, alisema Chama cha Mapinduzi, kipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na haipendezi kuona viongozi waliochaguliwa kuanza kuwadharau wananchi na wanachama kwa kuwacheza shere na badala yake wazitimize ahadi zao.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu, alisema baadhi ya viongozi wa majimbo, wilaya na Mkoa  wamekuwa na tabia ya kuwaona wanachama wa CCM na wananchi wazuri na muhimu sana wakati wa uchaguzi na baada ya kumalizika huwageuzia kibao kwa kuanza kuwakimbia huku wakiwa hawana kumbukumbu yoyote ya kimaendeleo waliyoiacha.

Alisema CCM haikubaliani na tabia hiyo na kama kuna viongozi ambao wanaojiona kuwa wao ni bora na hawawezi kuwatumikia wananchi ni vyema wakaanza kuondoa kabla ya Chama kuchukua hatua za kuwavua madaraka.

“Msisahau ulipochomea, msisahau mlipotoka viongozi wa majimbo, wilaya na Mkoa, mnawafanya wana CCM juzi walikuwa wazuri leo mnawaona wabaya, wao ndio waliowapigia kura, CCM ni moja fanyeni kazi kwa pamoja mkifanya hivyo Chama kitakuwa imara”, alisema Dk. Shein.

Alisema ikiwa viongozi hao wataweza kujipanga na kutekeleza vyema majukumu yao watakuwa wamekijengea sifa Chama chao na sio vyema kuanzisha mambo ambayo yatawakera wanachama wa CCM kwani wanaweza  kukiona chama chao hakina maana.

Dk. Shein alisema inafurahisha kuona Jimbo la Kitope limekuwa likipewa sifa kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM katika kuwapatia maendeleo wananchi wake na haoni sababu ni kwa nini viongozi wa majimbo mengine washindwe kufikia malengo hayo wakati wenyewe walikubali kuwatumikia wananchi.

“Nayasema haya kwa kuyajua ninachotaka kuwaambia wenzangu lazima mkae na watu ili mnayoyafanya yawe yenye faida kwao msikurupuke tu chama kina taratibu zake na chama hiki kila mtu ni chake sio cha mtu mmoja”, alisema Dk. Shein.

Alisema viongozi wa CCM, wanapaswa kutambua  ushindani wa kisiasa  bado upo licha ya kuwapo kwa  serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini inashindana kiustaarabu na haitakuwa vyema kuendelea kuwa na viongozi wasiokiendeleza Chama hicho.

Kuhusu suala la ulipaji wa ada za uwanachama Dk. Shein alisema kuwa anaamini kuwa wanachama wa CCM hawana tatizo kulipa ada zao, lakini kinachohitajika ni kuona viongozi wanawafuata na kuwakumbusha wajibu wao.

Mapema Mbunge wa Jimbo hilo, ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alieleza kuwa dhamira ya kujenga ukumbi huo ni kwa ajili ya kuwapatia kitega uchumi wananchi wa Jimbo hilo ambapo fedha zitazopatika zitawawezesha kutumia katika shughuli za maendeleo yao.

Alisema mara zote Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikiwataka viongozi wake kuwapatia maendeleo wananchi wake na Jimbo hilo litahakikisha linafanya kila njia kutimiza yote yaliomo kwenye ilani ambapo tayari hivi sasa wamekamilisha tatizo la ukosefu wa vikalio katika skuli saba za Jimbo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Kaskazini, alisema ujenzi wa ukumbi huo iwe ni funzo kwa viongozi wa Mkoa huo na wanapaswa kusoma hilo ili kukiimarisha Chama.

Akitoa shukrani kwa rais wa Zanzibar, Mbunge wa zamani wa Jimbo la Donge, Mzee Ali Ameir Mohammed, alisema kinachohitajika kuona viongozi wa CCM wanajipanga vyema kuweza kupata viongozi bora katika uchaguzi ujao na sio kuwapa sifa za kuwawekea alama ya A viongozi ambao wanashindwa hata kufika katika vikao vya Chama.

Mapema wanachama wa CCM wa Jimbo hilo wakisoma risala yao walishuru kufanyika ujenzi huo ambao umegharimu shilingi milioni 40 na hadi kumalizika kwake utafikia shilingi milioni 50 huku Mbunge wa Jimbo hilo kwa kipindi cha miaka sita akiwa tayari ameweza kutumia zaidi ya shilingi milioni 280 kwa shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.