TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezishukuru Serikali za Marekani na Ireland kwa kuongeza fedha za misaada kiasi cha dola za Marekani milioni 8.7 kwa ajili ya mradi wa kuboresha lishe nchini (Scaling Up Nutrition – SUN) kuanzia mwaka huu.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumapili, Juni 12, 2011) wakati akiendesha kikao cha mazungumzo ya viongozi wa juu (high-level Roundtable meeting) kwenye hoteli ya Kempinski jijini Dar es Salaam ambacho kilihudhuriwa pia na mawaziri wa SMT na SMZ, makatibu wakuu na mabalozi wa nchi hizo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania imedhamiria kutimiza lengo hilo kwa kuweka vipaumbele sita cha kwanza kikiwa ni kukamilisha Sera ya Taifa ya Lishe Bora itakayoainisha majukumu ya wizara, wabia wa maendeleo, sekta binafsi na asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI).
“Kuanzia mwaka huu wa fedha (2012/2013), Serikali itaanzisha fungu maalum kwenye bajeti ya serikali kwa ajili ya program ya lishe bora ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya kitaifa itakayojumuisha wadau mbalimbali,” alisema wakati akiainisha kipaumbele cha pili na cha tatu.
Akitaja kipaumbele cha nne, Waziri Mkuu alisema mpango mwingine wa serikali ni kuingiza masuala ya lishe bora kwenye mipango ya maendeleo ya kilimo chini ya mpango wa uwekezaji katika kilimo na usalama wa chakula nchini Tanzania (Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan – TAFSIP).
“Kipaumbele cha tano kitakuwa ni kuharakisha uanzishaji na uendelezaji wa vituo maalum vya lishe bora katika ngazi ya wilaya, na mwisho ni kukamilisha mchakato wa kuongeza viinilishe kwenye mazao ya mafuta, ngano na unga wa mahindi ambao ulikubaliwa mwaka 2010 ili wenye viwanda vya kusindika waanze kuongeza viini-lishe,” alisema.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bibi Hlary Clinton aliipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuinua viwango vya lishe na kuahidi kutoa dola za marekani milioni 6.7 ikiwa ni mara nne ya misaada iliyokuwa imepangwa awali.
Alisema, Septemba 2010, yeye na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Michael Martin waliamua kuanzisha kwa vitendo mpango wa siku 1,000 za kuboresha maisha ya mtoto tangu akiwa tumboni ili kuongeza uhakika wa maisha ya watoto katika nchi zinazoendelea.
“Utafiti wa kisayansi unabainisha kuwa mtoto akipata lishe bora katika siku 1000 za mwanzo, maisha ni lazima yatakuwa ya tofauti ikilinganishwa na mtoto ambaye amepatwa na utapiamlo katika kipindi hichohicho,” alisema.
“Kila mwaka watoto milioni 3.5 wanakufa kutokana na utapiamlo au lishe duni… katika siku hizi 1,000 ambazo zitakamilika Juni 2013, tunataka tuone tofauti ya maisha kwa watoto ambao watazaliwa katika kipindi hiki na kupewa chakula chenye lishe bora.”
Alisema sehemu kubwa ya fedha hizo zitumika kuhamasisha jamii juu ya mapishi yasiyoathiri viini-lishe, utunzaji wa afya ya mama na mtoto na masuala ya usafi na uimarishaji wa miundombinu ya majisafi ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa SUN ambao unatoa misaada kwa kufuata mipango ya nchi husika.
Naye Naibu Waziri Mkuu wa Ireland ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara, Bw. Eamon Gilmore alisema serikali itatoa dola za marekani milioni kuanzia mwaka huu ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania.
“Sasa hivi tuko katika siku ya 264 tangu mpango huu uanze, nimetembelea miradi kadhaa nchini Tanzania na nimeridhika na juhudi za serikali katika mpango huu, alisema Bw. Gilmore.
Waziri Mkuu Pinda na Bibi Clinton mchana walienda Mlandizi kwenye shamba la Ushirika la kikundi cha akinamama cha Upendo ikiwa ni sehemu ya kuzindua mpango wa kujitosheleza kwa chakula nchini Tanzania (Feed the Future Programme in Tanzania - FTP).
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, JUNI 12, 2011.
No comments:
Post a Comment