Na Halima Abdalla
MTU Mmoja amekutwa akiwa amefariki pembezoni mwa fukwe za bahari ya kisiwa cha Chumbe kilichopo, wilaya ya Magharibi Mjini Unguja.
Akithibitisha kuokotwa kwa maiti hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Muhammed, alisema maiti hiyo imeokotwa Julai 11 majira ya saa 4:00 asubuhi.
Alisema maiti hiyo ni ya mtu mwanaume lakini jina lake halikuweza kufahamika na pia umri wake haukufahamika.
Alisema hadi sasa hajajitokeza mtu yoyote kumtambua marehemu huyo, makaazi yake kabla ya kupatwa na kifo hicho.
Kamanda huyo alisema kufuatia hali hiyo, na ukweli kuwa maiti hiyo imeharibika sana, ilikabidhiwa Ustawi wa jamii kwa mazishi siku hiyo.
Kamanda Aziz alitoa wito kwa jamii wanaposhuhudia matukio kama hayo, kutoa taarifa mapema kwa vyombo husika.
Aidha aliwataka wananchi wanaokwenda katika maeneo ya pwani kwa ajili ya uvuvi au kuogelea kuwa waangalifu katika kipindi hiki cha upepo mkali ili kuepukana na ajali zinazosababisha kupoteza maisha.
No comments:
Post a Comment