Na Abdi Shamnah- PBA
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka masheha, Madiwani , viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na watendaji wa Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC), kuhakikisha wanafanikisha vyema zoezi la uchumaji wa karafuu msimu huu.
Aidha amewataka viongozi hao kujizatiti kukabiliana vilivyo na usafirishaji wa zao hilo kwa njia ya magendo, ili kuimarisha uchumi wa taifa.
Maalim Seif ametoa changamoto hiyo leo kwa nyakati tofauti, wakati alipozungumza na viongozi hao wa Mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba katika mikutano iliofanyika katika kituo cha Benjamin Mkapa Wete na Makonyo Wawi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kununua wastani wa tani 3,000 ya zao hilo msimu huu kutoka Mikoa yote ya Unguja na Pemba, na kuitaka ZSTC kusimamia watendaji wake ili kuhakikisha ni waaminifu na wanafanyakazi zao kwa uadilifu mkubwa.
Aliwataka kuondokana na kasoro zote ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi, ikiwemo ya ununuzi wa zao hilo kwa njia ya mkopo, upungufu wa vituo vya kununulia pamoja na uchakachuaji wa kiwango(grade) cha karafuu.
Aidha alililitaka shirika hilo kutoa taaluma kwa wakulima kuondokana na utamaduni uliozoeleka wa kukaa na karafuu majumbani na badala yake aliwataka kuzisalimisha ZSTC ili kuepukana na wizi au majanga mbali mbali ikiwemo moto.
Vile vile aliitaka ZSTC kuwashajiisha wakulima kufungua akanti katika Mabenki ili fedha zao ziendelee kuwa salama wakati wote, suala alilotaka liende sambamba na utoaji wa taaluma kupitia vyombo vya habari.
Aliishauri Wizara ya biashara, Viwanda na Masoko kukaa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na maendeleo ya kuchumi, ili kuhakikisha mji wa Wete unakuwa na Tawi la Benki pamoja na kuweka Mobile Banks katika vituo vikuu vya kununulia karafuu.
Katika hatua nyingine Maalim Seif aliwaeleza Mabalozi kuwa wao ndio kiungo muhimu katika ufanikishaji wa kazi hizo kwa kuzingatia kuwa ndio wanaoishi na wakulima na watu wanaoendesha vitendo vya magendo.
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, kila mwananchi ana jukumu la kulihami zao hilo, hivyo aliwataka masheha kuwa makini katika udhibiti wa karafuu na kuona hakuna karafuu mbichi zinazosafirishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Alionya kamwe kusiwepo visingizio vitakavyopelekea karafuu mbichi kuhamishiwa maeneo mengine kutoka pale zilipochumwa na kuainisha kuwa pale pasipo budi (iwapo mvua zimeshamiri), ni lazima vibali maalum vitolewe pamoja na kuwepo ufuatiliaji kutoka shehia zilipochumwa na kule zinakopelekwa kuanikwa.
Aidha Maalim Seif alivitaka vyombo vya Ulinzi na hususan Polisi kuharakisha kuwepo kwa utaratibu wa Polisi jamii ili kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu ikiwemo magendo na uvunjaji wa nyumba.
Alisikitishwa na taarifa za kuwepo kwa maamuzi yasioridhisha yanayofanywa kwa makusudi na baadhi ya Mahakama, kiasi cha kuwavunja moyo watendaji waliojitolea kupambana na vitendo vya usafirishaji wa karafuu kwa njia ya magendo.
Aliwahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inalenga kuhakiki utendaji wa kila taasisi ili kuhakikisha kiwango kilicholengwa cha ununuzi wa karafuu zinafikiwa.
Nae Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Ahmed Nassor Mazrui, alitoa masikitiko yake kutokana na takwimu za utoroshwaji wa zao hilo kupelekwa Kenya kwa kipindi kirefu sasa na kutoa mfano wa mwaka uliopita, ambapo nchi hiyo ambayo haina kabisa mikarafuu iliuza tani 2269 katika soko la Dunia na kuishinda Zanzibar iliouza tani 2100.
Alisema karafuu toka Kenya ziliuzwa zikiwa na nembo ya Zanzibar, kwa vile zililengwa kuvutia bei kubwa zaidi katika soko hilo kwa kuzingatia nafasi ya Zanzibar katika ubora wa kiwango.
Hata hivyo alisema tayari Serikali imeshafanya usajili katika Shirika la Biashara la kimataifa, ambapo pale mkataba huo utakapotiwa saini, Kenya haitoweza tena kuuza karafuu za Zanzibar kwa vile zitakuwa zinalindwa an sheria za Kimataifa na ikibainika kuuza itashtakiwa.
“Manufaa ya ‘Brand new’ ni kuwa huuzi karafuu, bali unauza karafuu ya Zanzibar, ambapo mkulima atapata asilimia 80 ya bei ya soko la Dunia’,alisema.
Mazrui alisema Sheha yeyote atakaetoa taarifa za kuwepo mpango wa kusafirisha karafuu kwa njia ya magendo, atapata zawadi ya kulipwa asilimia 20 ya thamani ya karafuu zilizokamatwa.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi aliwataka Masheha na Madiwani kutoa ushirikiano kama wanavyoshirikiana katika kazi nyengine za maendeleo na kubainisha kuwa atatumia mamlaka aliyonayo kumfukuza kazi mara moja sheha yeyote atakaebainika kujihusisha na vitendo vya usafirishaji magendo ya karafuu.
Mmoja kati ya viongozi waliohudhuria katika kikao hicho, Ali Abdalla Ameir (Diwani wa Wadi ya Shumba viamboni) akichangia katika kikao hicho, aliiomba Serikali kuangalia upya hatua yake ya kuchukua mashamba ya wananchi kwa kilimo cha mpira, zao linalodaiwa kukosa mafanikio.
No comments:
Post a Comment