Na Halima Abdalla
BAADHI ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesikitishwa na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto na wanawake kutelekezwa vinavyofanywa na baadhi ya akinababa.
Waliishauri Serikali kuweka sheria kali na nzito kwa yeyote atakaepatikana na hatia hiyo kupewa adhabu nzito na itangazwe katika vyombo vya habari ili kuweza kutoa somo kwa wabakaji wengine.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, wanawake na Watoto, Asha Bakari Makame, aliishauri Serikali kuweka sheria kali kwa wanaume wanaofanya kazi Serikalini ambao wanatelekeza wanawake na watoto kuwakata kima cha mshahara wao kila mwezi ili aweze kupewa mwanamke kiweze kumsaidia yeye na mtoto wake.
Alisema wanawake sasa hivi wamekazana kwa kujishughulisha shughuli mbali mbali za kujipatia kipato, lakini wamekuwa wakirudi nyuma kutokana na kutelekezwa na akinababa kwa kuwaachia familia bila ya kuwashughulikia.
Sambamba na hayo aliwashauri kinababa kuwaonea huruma kinamama kutokana na kazi ngumu wanazozifanya pamoja na kuangalia familia na kazi nzito zinazowakabili.
Nae Mtumwa Kheir Mbarouk (Nafasi za wanawake ) aliwataka kinababa kuwa na imani kuacha kuwaharibu watoto wadogo walemavu na mataahira kwani vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Sambamba na hayo aliwashauri wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa vitendo hivyo kutokubali kuyamaliza mitaani, ila wayafikishe katika vyombo husika pamoja na mahakama zisichelewe kesi hizo pamoja na kutoa hukumu.
Aisha alimshauri Wizara ya Ustawi wa jamii kuelimisha wananchi kuwa wanapofanyiwa vitendo hivyo vya ubakaji wasifiche kwani wanaofanyiwa vitendo hivyo ni masikini na wenye uelewa mdogo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Micheweni, Subeit Khamis Faki aliishauri Wizara hiyo kubuni miradi mbali mbali ya kuweza kusaidia kuajiri vijana ili kuondokana na watoto wa mitaani kwani ajira za utotoni hazifanywi kwa maksudi ila hali hiyo inatokana na hali za wazee wao kuwa ngumu na yeye ili apate kuishi.
''Hawa watoto hawafanyi kwa hiari yao wanafanya kwa lazima ili waweze kupata chakula cha kuwasaidia ili waweze kuendelea kuishi,''alisema Subeit.
Aidha alishauri Serikali kuwasaidia vijana waliopo katika wilaya ya Micheweni kwa sababu inaongoza kwa ajira za utotoni pamoja na umasikini kwa kuweza kuwatembelea na kuwapatia elimu sambamba na kuwasaidia ili kuondokana na umasikini.
Nae panya Ali Abdalla (Nafasi ya wanawake) alizishauri mahkama kuacha kuwasumbua wanawake wanapofuatilia kesi za ubakaji mahkamani kutokana na nenda rudi za kila siku ambazo zinasababisha wanawake kukata tamaa na kupelekea kesi hizo kushindwa kuendelea.
Kwa upande wake Viwe Khamis Abdalla (Nafasi ya wanawake) aliishauri akinamama wanaojifungua kuacha kutelekeza watoto kwa kuwatupa aliishauri Serikali kuchukuliwa hatua kali wanawake hao kwani wanachofanya ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment