Habari za Punde

WAWAKILISHI SPORTS CLUB YANYESHWA GRAND MALT YA VIFAA

Na Salum Vuai, Maelezo

KAMPUNI inayotengeneza kinywaji cha Grand Malt, jana iliikabidhi timu ya michezo ya Baraza la Wawakilishi vifaa kwa ajili ya kutumika katika bonanza la kimichezo mkoani Arusha Septemba 8, mwaka huu.


Vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa uongozi wa timu hiyo na Meneja wa kinywaji hicho kisichokuwa na kilevi Consolata Adam katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya manispaa ya Zanzibar.

Vifaa hivyo ni pamoja na jezi, suti za michezo (track suits), viatu na soksi vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni kumi.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wanachama wa timu hiyo, Consolata alisema ni fahari kwa kampuni yake kuipiga jeki timu hiyo, na kwamba ni matumaini yake kuwa vifaa hivyo vitaipa ari ya kushiriki kwa ufanisi bonanza hilo.

"Grand Malt ndicho kitakachokuwa kinywaji kikuu cha bonanza hilo maalumu litakalojumuisha timu ya Wazee ya Arusha, hii ya Baraza la Wawakilishi na nyengine", alieleza.      

Aidha alifahamisha kuwa anatumai udhamini wa bonanza hilo utasaidia kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya kampuni yake na Baraza la Wawakilishi, huku akiwaombea wajumbe wake mapumziko mema baada ya shughuli nzito ya kikao cha bajeti ya serikali kinachoendelea.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, Katibu Mkuu wa timu Haji Omar Kheri na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Ali Abdallah, wote kwa pamoja walishukuru kwa msaada huo na kutaka iwe mwanzo wa ushirikiano kati ya taasisi hizo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.