Habari za Punde

WAWEKEZAJI WA UINGEREZA BADO WANA NAFASI YA KUWEKEZA ZANZIBAR - BALOZI SEIF


Wawekezaji wa Uingereza bado wana nafasi ya kuwekeza ndani ya Visiwa vya Zanzibar katika sekta ya viwanda kwa lengo la kusaidia suala la ajira hasa kwa vijana .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo wakati akihojiwa na Mwandishi wa Gazeti la World Report lenye makao yake Makuu Mjini London Nchini Uingereza Bibi Barbara Yankovic.

Balozi Seif Ali Iddi amesema uamuzi wa Wawekezaji wa nchi hiyo kuwekeza katika eneo hilo la Viwanda ambalo linachukuwa ajira kubwa zaidi bado liko finyu katika Uwekezaji.


Amesema Changamoto kubwa inayoikabili Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa ni suala la ajira. Hivyo juhudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuona eneo hilo linapata ufanisi katika kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira.

“ Uingereza na Zanzibar zina Historia ndefu sana katika masuala ya Kibiashara. Hivyo nafasi hiyo itasaidia kuimarisha zaidi ukaribu huo ” Alisema Balozi Seif Ali Iddi.

Balozi Seif amemueleza Mwandishi huyo kwamba miundo mbinu katika sekta nyengine kama vile Afya, Elimu, Utalii na Kilimo imefikia kiwango cha kuridhisha.

Amesema kinachozingatiwa kwa sasa ni kuongeza nguvu zaidi katika sekta ya kilimo kwa vile inachukuwa asilimia 70% ya watu wote wa Zanzibar wanaoishi vijijini.

Kampuni Binafsi inayomiliki Gazeti la World Report imekuwa ikichapisha makala na kutangaza mambo ya Kiuchumi, Wafanyabiashara na Uwekezaji hasa katika Sekta za Utalii .

Hatua hiyo ina lengo la kuwashajiisha Wawekezaji tofauti wa Kimataifa kuwekeza katika Mataifa ambayo tayari yanasimamia vyema amani na kufuata utawala wa kidemokrasia.

Waandishi wa Gazeti hilo la World Report tayari wameshakutana na viongozi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } kwa mazungumzo na kuangalia mazingira ya kuyatangaza maeneo hayo kwa wawekezaji nje ya nchi.

Gazeti hilo tayari limeshafanya utafiti wa Utawala Bora na kutangaza mambo ya Kiuchumi na Uwekezaji katika Mataifa ya Cameroun, Angola pamoja na Tanzania Bara.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar.
19/8/2011.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.