Habari za Punde

DHORUBA YAWAFANYA ABIRIA MV SERENGETI KUOMBA MAKOTI YA KUOKOLEA

Wakitokea Pemba kwenda Unguja usiku

Na Haji Nassor - Pemba

ABIRIA waliosafiri na Mv. Serengeti kutoka Pemba kwenda Unguja juzi usiku walipatwa na hofu na kusababisha kuomba vifaa vya kuokolea maisha (life jackets) kutokana na chombo hicho kukumbwa na dhoruba, kabla ya kufikia mkondo wa Nungwi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari hizi aliyekuwa miongoni mwa abiria wa meli hiyo, alisema hali hiyo, ilianza kujitokeza saa 5:55 usiku, baada ya meli hiyo kuacha kisiwa cha Mtumbilini na kuanza kukumbwa na mawimbi mazito.


Alisema wimbi hilo lilitanguliwa na mvua iliyombatana na upepo, kabla meli hiyo haijaondoka Bandarini Mkoani saa 3:48, na baadae ikaanza kuyumba, huku abiria wakipiga kelele kuomba wapatiwe mavazi ya uokoaji.

Mwadishi huyo anasema wakati meli hiyo ikiendelea na safari huku ikipata msukosuko wa kuyumba, baadhi ya abiria hasa waliokuwa sehemu ya deki na juu walikuwa wameshavaa maboya hayo (life jakects ) wakijitayarisha kwa lolote litakalotokea.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa abiria hao, Mohamed Omar Hassan (50) alisema kutokana na uzoefu wake wa kusafiri baharini hilo kwake halikuwa jambo kubwa, lakini taharuki hiyo iliunganishwa na kumbukumbu za hivi karibuni za kuzama kwa Mv. Spice Islander 1.

''Mimi sikuona jambo kubwa maana meli kama hizi hasa Serengeti kuyumba kwa kasi hutokezea tena wakati mwengine huanza hata bandarini, lakini taharuki hii ya leo ilitokana na kuwa bado tuna kumbukumbu za ndugu na jamaa zetu waliozama hivi karubuni'',alieleza.

Nae Shadya Khamis Mussa ( 22) ambae alikuwa wa mwanzo kuvaa 'life jackets' alisema aliamua kumuita baharia mmoja, ampe kifaa hicho kwa kubaini hali ilianza kubadilika mapema.

Alisema kilichowatia wasiwasi zaidi ni kutokana na meli hiyo kuyumba kwa kasi hata kabla ya kufika kwenye mkondo wa Nungwi, ambapo alisema hali hiyo ilitokana na zaidi na mwenendo wa upepo.

''Niliona bado kisiwa cha Pemba hatujakiacha na hali siyo ya kawaida je tukifika huko Nungwi hali itakuwaje na ndio maana nikaomba 'life jackets' mapema na wenzagu kuyaomba kwa kelele sote tukawa sare'',alifafanua.

Baadhi ya abiria waliokuwa vyumbani (first class) walisema hawakubaini hali hiyo iliyosababisha baadhi ya abiria kufikia kuomba nguo za kuokolea maisha.

Hofu kubwa ambayo ilisababisha baadhi ya wenzao wengine waliokuwa deki hadi kufikia kuomba vifaa vya kuokolea maisha, abiria mwengine, Juma Mohamed, alisema alisikia hali ya kawaida na hakuwa na wasiwasi.

Hata hivyo, abiria waliuomba uongozi wa Mv. Serengeti kuacha tabia ya kusafiri usiku kwani panapotokezea ajali inakuwa vigumu kupata msaada wa haraka, kama uzoefu unavyoonesha.

Mabaharia ambao hawakupenda majina yao yachapishwe gazetini, walisema hali hiyo ilisababishwa na meli hiyo kukosa kago (mzigo) na kilichotokea kwa meli hiyo ni jambo la kawaida inapokosa mzigo.

Walisema kelele za abiria zilitokana na kumbukumbu waliyonayo kwa tukio la ajali ya hivi karibuni.

Mv. Serengeti ambayo karibuni ilisimamishwa kupakia abiria na kisha kuruhusiwa baada ya kufanyiwa ukaguzi, ilikosa abiria wa kutosha na hata mizigo ilipokuwa ikitokea Mkoani kuelekea Unguja.

Wataalamu wengi walisema kukosekana abiria na mizigo ya kutosha ni moja ya sababu za kuyumba kwa meli hiyo.

1 comment:

  1. Jamani! si tulishauri meli zisitembee usiku?...Ama kweli sikio la kufa halisikii dawa!..This is ZNZ!!!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.