KESI 260 za udhalilishaji wa kijinsia wa watoto zimeripotiwa kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu katika Mkoa wa mjini Magharibi.
Akizungumza na Zanzibar Leo huko ofisini kwake Madema, Mratibu Msaidizi wa Dawati la Wanawake na Watoto, Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Fakih Yussuf, alisema kati ya kesi hizo nyingi ni za shaka ya mimba chini ya umri wa miaka 18, kutorosha, ubakaji pamoja na za kudhalilishwa kinyume na maumbile kwa watoto wa kiume.
Fakih alisema kati ya kesi hizo 260 ni 40 tu ndizo zilizofikishwa mahakamani kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.
Alizitaja kesi hizo kuwa ni pamoja na kesi za ubakaji nane, kutorosha kesi 15, kinyume na maumbile kesi 12, kulawiti kesi mbili, shambulio la kuumiza mwili, kubaka kwa kundi moja na kuumiza mwili moja.
Aidha alisema kuwa nyingi za kesi zilizoripotiwa kituoni hapo zimeshindwa kufikishwa mahakamani kutokana na kuwa ziko katika upelelezi na nyengine zimemalizikia kituoni hapo kwa kushindwa kuwa na ushahidi wa kutosha.
“Kesi nyingi zimemalizika hivi hivi kutokana na kukosa masshiko ya kuweza kumpeleka mtu mahakamani na ndio sababu ya kuongezeka kwa matukio kama haya”, alisema.
Mratibu huyo wa dawati la wanawake na watoto, alisema nyingi ya kesi zinazoripotiwa Mkoani humo ni kutokea wilaya ya Magharibi kutokana na vitendo hivyo kushamiri katika maeneo hayo.
Alivitaja vituo vinavyoongoza kupokea kesi hizo kuwa ni Bububu, Ng’ambu na kufuatiliwa kituo cha Madema.
Fakih aliwataka wananchi kutoa mashirikiano ya kutosha hasa katika dawati hilo la wanawake na watoto kwa lengo la kuwatia hatiani watuhumiwa wa vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment