Habari za Punde

UPUNGUFU WA SINDANO ZA 'MODECATE' WAIKABILI HOSPITALI YA WAGONJWA WA AKILI

Na Mwantanga Ame

WAZIRI wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji, amekiri kuwepo matatizo mbali mbali hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu Mjini Zanzibar, ambapo tayari serikali imeanza kuyafanyia kazi.

Alisema sindano aina ya ‘Modecate’ imekosekana kwa muda mrefu kutokana na ukweli dawa hiyo haipo nchini kwenye ghala kuu la dawa Dar es Salaam (MSD), ambako Wizara hiyo ndiko inakoagizia dawa zote za hospitali zake.


Kutokana na upungufu huo madaktari wa hospitali hiyo wamebadilisha aina ya dawa zikiwa na lengo moja na modecate kuwapatia wagonjwa hospitalini hapo.

Kuhusu upungufu wa chakula kwenye hospitali hiyo, Duni amesema awali kulikuwa na upungufu wa mgao ‘resheni’ katika hospitali hiyo jambo ambalo hivi sasa limerekebishwa.

Amesema kabla walikuwa wakitoa shilingi milioni moja kwa chakula na hivi sasa wanatoa shilingi milioni moja na laki nane (1.8 milioni) kwa chakula hospitalini hapo.

Aidha amesema katika kuiangalia hospitali hiyo, Wizara tayari imepeleka madaktari watatu na kuimarisha ulinzi kwenye majengo na maeneo ya hospitali hiyo.


Maelezo ya waziri Dunia yanafuatia malalamiko yaliyotolewa na wagonjwa hospitalini hapo ya kukosekana sindano aina ya ‘Modecate’ katika hospitali hiyo kwa mwaka sasa huku chakula wanachopewa wagonjwa hao kudaiwa kukopewa madukani.

Mmoja wa wagonjwa wa akili, Mselem Daud, aliiambia Zanzibar Leo kuwa dawa hiyo imeanza kukosekana kwa muda mrefu sasa hali inayosababisha kuzorota kwa huduma hapo.

Mwananchi huyo alisema amekuwa analazimika kununua dawa hizo katika maduka ya dawa ya binafsi ambapo huuziwa sindano moja ya ‘Modecate’ kwa shilingi 6,000.

Aikaririw akisema hali hiyo imesababisha matatizo makubwa kutokana na ughali wa dawa hizo hasa kwa kuangalia hali ngumu ya mapato kwa wagonjwa na familia zao.

Alisema anajenga hali wasi wasi wa kuongezeka matatizo hayo kutokana na ukosefu wa fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya dawa hizo.

Pia waziri Duni alitoa ufafanuzi huo mbele ya Baraza la Wawakilishi, alipohojiwa kama serikali inafahamu kuwepo kwa matatizo hayo kwa kipindi kirefu hivi sasa.

Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, alilieleza Baraza hilo katika kipindi cha masuali na majibu kwamba ingawa serikali imekuwa na nia njema ya utoaji huduma katika hospitali hiyo, lakini hivi sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, chakula na dawa.

Alisema mbali ya tatizo hilo pia hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la sindano za aina ya ‘Modicate’ ambazo zimekosekana kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa jambo ambalo tayari wananchi wameanza kupatwa na wasiwasi na wagonjwa hao kuweza kupata msaada kwa vile ndio hospitali
wanayoitegemea.

Nae Mwakilishi wa Kiwani, Hija Hassan Hija, aliliambia Baraza hilo hivi sasa kuna taarifa kutoka kwa watumishi wa hospitali hiyo zikidai kuwa chakula wanachopewa wagonjwa hakitoshi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.