Na Salum Vuai, Maelezo
BAO lililofungwa na mchezaji Jaku Juma dakika tatu kabla mchezo kumalizika, lilitosha kuwaadhiri mabingwa wa soka Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati Yanga, katika mechi ya pili ya kundi B kwenye
michuano ya Kombe la Mapinduzi juzi usiku.
Jaku aliuwahi mpira wa juu uliotua miguuni mwake baada ya kuwazidi maarifa walinzi wa Yanga, na kumtazama mlinda mlango Said Mohammed kabla kufumua shuti la nguvu lililokwenda nyavuni moja kwa moja. Bao hilo lilikuja wakati kila mmoja akidhani kuwa mpambano huo ungemalizika kwa sare.
Hata hivyo, Mafunzo ilistahili kushinda kutokana na kuonesha mchezo wa kushambulia kwa muda mwingi, na kuwaweka katika wakati mgumu walinzi wa vijana hao wa mtaa wa Jangwani.
Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wengi wakiongozwa na Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume,
Mafunzo ililiandama mno lango la wapinzani wao, ambapo washambuliaji wa timu hiyo akina Sadik Habib, Jaku Juma, na wenzao, walipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Yanga nayo ilipeleka mashambulizi mara chache langoni mwa Mafunzo, lakini ilikatishwa tamaa na umahiri wa mlinda mlango Suleiman Janabi, ambaye alikuwa shujaa kwa kupangua michomo mikali ya Jerry Tegete,
Rashid Gumbo na Idrissa Rashid.
Yanga ilikianza kipindi cha pili kwa kasi ambapo mnamo dakika ya 59, nusura Atupele Green aipatie goli, baada ya walinzi wa Mafunzo kupasiana bila uangalifu, lakini shuti ya mchezaji huyo ilitoka nje kidogo ya goli.
Kosakosa za timu zote ziliendelea kuwapa kashikashi walinda milango wa pande zote, lakini milango ilikuwa migumu, hadi ilipofika dakika ya 42, ambapo Jaku Juma alifanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu
na mashabiki wa soka waliojazana uwanjani hapo.
Baada ya pambano hilo, Kocha Mkuu wa Yanga Kostadin Papic, alisema timu yake imekosa maandalizi ya kutosha, pamoja na hali ya uwanja kuwa mbaya, huku msaidizi kocha wa Mafunzo Omar Abdi akisema ameridhishwa na kiwango cha timu yake, ambayo iko katika maandalizi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment