UMOJA wa Ulaya (EU) umeahidi kuendelea kuisaidia Zanzibar katika sekta mbali mbali kwa lengo kusukuma mbele maendeleo ya jamii na Taifa.
Balozi mpya wa EU nchini Tanzania, Filiberto Ceriani Sebregondi alieleza hayo alipofanya mazungumzo na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho ofisini kwake Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Balozi Sebregondi alisema maeneo yatakayopewa kipaumbele na umoja huo kimisaada ni pamoja na kuzijengea uwezo asasi za kiraia, masuala ya haki za watoto na UKIMWI, habari, nishati na sheria.
Alifahamisha kuwa EU inavutiwa hali ya kisiasa iliyopo Zanzibar hivi sasa hasa kwa kuona wananchi wanaishi kwa amani na maelewano ikiwa ni matunda ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa uliopo.
Alisema hatua hiyo pia inapelekea wawekezaji wengi pamoja na wafadhili kushawishika kuja kuwekeza hapa nchini na yeye kwa upande wake atasaidia kuitangaza hali hiyo ulimwenguni.
Balozi huyo alisema kuwa EU iko tayari kusaidia katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi ili waweze kuuenzi vyema mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa uliopo hapa Zanzibar kutokana na mafanikio yake.
“Tunakusudia kuwasaidia viongozi namna ya kuulinda mfumo huo wa serikali ya umoja wa kitaifa kwani tunaona unasaidia katika kujenga umoja, utulivu wa kisiasa huku wananchi wakiendelea kuishi kwa amani”, alisema Balozi huyo.
Kwa upande wake, Spika Kificho alisema ingawa mfumo serikali uliopo hivi sasa ni mpya na haujazoeleka, lakini umekuwa na mafanikio makubwa ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Akitoa mfano, Spika Kificho alisema utendaji wa Baraza hilo hivi sasa unazidi kuimarika kwani kila mjumbe anatekeleza vyema majukumu yake bila ya kuzingatia itikadi ya chama chake.
Alisema mawaziri kutoka CCM na CUF wamekuwa wakishirikiana kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali za wajumbe wasiokuwa mawaziri ambao na wao wamekuwa kitu kimoja katika kuhoji utendaji wa serikali kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji.
“Huwezi kuamini, inawezekana waziri anatoka CCM anajibu hoja kwa mjumbe, lakini baadae akasimama waziri mwengine kutoka chama cha CUF akasaidia kutoa ufafanuzi, haya ni mashirikiano na mafanikio makubwa”, alisema Spika huyo.
No comments:
Post a Comment