Habari za Punde

Maalim Seif Aitaka KCB Kusaidia Sekta ya Michezo Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya biashara ya Kenya KCB Bw. Moez Mir, wakati ujumbe wa benki hiyo ulipofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana mawazo.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya biashara ya Kenya KCB Bw. Moez Mir, akitoa ufanunuzi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad juu ya namna benki yake inavyoweza kushirikiana na Zanzibar katika kusaidia huduma za kijamii, wakati ujumbe wa benki hiyo ulipofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana mawazo. Kulia ni mkurugenzi wa biashara wa benki hiyo Respige Kimath

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa benki ya biashara ya Kenya KCB wakati ujumbe huo ulipomtembelea ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar. Kuliani kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw. Moez Mir akifuatiwa na meneja biashara tawi la Zanzibar Bw. Abdul Mshangama.
(Picha, Salmin Said, OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameiomba benki ya maendeleo ya Kenya KCB kuangalia uwezekano wa kusaidia sekta ya michezo Zanzibar ili kurejesha hadhi ya michezo nchini.

Amesema serikali ina nia thabiti ya kurejesha hadhi ya michezo Zanzibar na kufufua michezo ya asili ikiwemo ya ndani (Indoor games), lakini imekuwa ikikwazwa na ufadhili mdogo katika michezo mbali mbali ukiwemo mchezo wa soka.

Maalim Seif ametoa changamoto hiyo huko ofisini kwake Migombani alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa benki hiyo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Moez Mir.


Amesema serikali inajipanga kwa ajili ya kujenga uwanja wa michezo ya ndani, na kwamba iwapo lengo hilo litafanikiwa hadhi ya michezo Zanzibar inaweza kurejea katika hali yake ya awali ambapo ilikuwa ikisifikana kwa michezo mbali mbali ikiwemo table tennis na golf.

Amefahamisha kuwa miongoni mwa matatizo yanayokwaza sekta ya michezo kwa sasa ni upungufu wa viwanja vya michezo hasa ya ndani, pamoja na kuendeleza vipaji vya vijana vinavyoibuliwa kutoka maskulini na maeneo mengine ya michezo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo bw. Moez Mir amesema benki yake inalichukua wazo hilo na kulifanyika kazi sambamba na kuwasiliana na wadau wengine wa michezo ili kuona namna ya kuleta ufadhili wa michezo mbali mbali na kuinua hadhi ya michezo Zanzibar.

Amesema kitu cha msingi ni mashirikiano katika sekta hiyo, na kwamba benki yake pia inalizingatia suala hilo akielezea matarajio yake kuwa linaweza kutatuliwa kwa mashirikiano baina ya serikali na wadau wengine.

Wakati huo huo Bw. MIR amesema benki yake iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika jitihada zake za kukabiliana cha changamoto inazozikakabili ikiwemo dawa za kulevya, watu wenye ulemavu na uchafuzi wa mazingira.

Amesema benki yake ambayo imekuwa ikiunga mkono shughuli za kijamii hasa katika sekta za elimu na mazingira, itaendelea na jitihada hizo na kuongeza maeneo mengine ya kusaidia ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya kijamii yanaimarika Zanzibar.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais ameipongeza benki hiyo kwa mwamko wake wa kusaidia huduma za kijamii zikiwemo elimu, na kuiomba kuangalia uwezekano wa kuangalia maeneo mengine ya kusaidia yakiwemo mapambano dhidi ya dawa za kulevya na masuala ya watu wenye ulemavu.

Maalim Seif amesema Zanzibar inafarajika kuona taasisi za fedha ikiwemo benki ya KCB zinashirikiana na serikali katika kusaidia kutatua kero zinazowakabili wananchi, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo, ili ziweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi zaidi.

Mapema meneja wa biashara wa benki hiyo tawi la Zanzibar Bw. Abdul Mshangama, ameiomba serikali kuzitumia kikamilifu fursa zinazotolewa na benki hiyo ili iweze kunufaika na fursa hizo ambazo zitasaidia maendeleo ya wananchi na taifa kwa jumla.

Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.