Apongeza Bunge, Asema halikumfadhaisha
Na Mwandishi wetu, TANGA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema hatua dhidi ya mawaziri na viongozi wanaotuhumiwa bungeni hivi karibuni dhidi ya ufujaji wa fedha za umma zimeanza kuchukuliwa.
Rais Kikwete alieleza hayo jana mkoani Tanga, kwenye maadhimisho kitaifa ya kilele cha sherehe za siku ya wafanyakazi duniani ‘May Day’ yaliyofanyika katika kiwanja cha Mkwakwani
.
Alisema hajakasirishwa na mijadala ya wabunge waliyoitoa wakati wa kijadili taarifa za kamati za kudumu za Bunge za serikali za mitaa, serikali kuu na mashirika ya umma na badala yake mapendekezo ya wabunge hao yanafanyiwa kazi.
“Hatujakasirishwa wala kufadhaishwa na mijadala ya kamati hizo bungeni, nawapongeza sana wabunge kwa kujadili kwa kina na mapendekezo yenu yameanza kufanyiwa kazi”, alisema Rais Kikwete.
Pamoja na hali hiyo Rais alibainisha kuwa wakati wa mijadala hiyo hakuwepo nchini na alionesha kusikitishwa juu ya hatua ya baadhi ya vyombo vya habari kumlishia maneno akitolea mfano, JK ampinga Pinda.
Alifahamisha kuwa uwazi katika matumizi ya fedha za umma ni jambo la msingi ambalo amekuwa akilipigia kelele, huku akibainisha kuwa kufanya hivyo ni miongoni mwa nguzo za utawala bora.
Alisema fedha za umma katika mashirika, serikali na serikali za mitaa si kwa ajili ya kuvimbisha matumbo ya watendaji badala yake ni zilenge kutatua matatizo ya wananchi.
“Niliwahi kusema katika halmashauri kuna mcha wanaotafuna fedha za serikali, nadhani hivi sasa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa fedha za serikali zinatusaidia kuweka wazi”, alisema.
Hata hivyo alisema kazi kubwa ipo ya kuhakikisha udhibiti wa fedha za umma kwa kuwaeleza bayana wale wanaojinufaisha binafsi na wasiokua waadilifu na waaminifu.
Aliipongeza ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa fedha za umma kwa kazi kubwa inayoichukua katika kubainisha na kuweka wazi wale wanaotumia fedha hizo kinyume na taratibu.
Rais Kikwete alisema serikali inafahamu mazingira magumu yanayowakabiliwa wafanyakazi na kwamba taratibu zitafanyika katika kuhakikisha kidogo kinachopatikana kinagawanywa kwa wote.
Katika hotuba yake hiyo Rais Kikwete aliwasisitia wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kutoa maoni juu ya mchakato wa kuundwa kwa aktiba mpya.
Aidha alizungumzia juu ya umuhimu wa wananchi kujitokeza katika sensa ya watu na makaazi ambayo ni mihumu sana katika mikakati na mipango ya serikali.
No comments:
Post a Comment