Habari za Punde

Waandishi Waaswa Kujikita Katika Nyanja Maalum za Habari


Na Abdi Shamnah –WHUUM

WAANDISHI wa Habari nchini, wameshauriwa kuandika habari zao kuambatana na  nyanja maalum (speciallization) na kuondokana na utamaduni wa kuandika habari katika nyanja zote.

Changamoto hiyo imetolewa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk , wakati alipozungumza an waandishi wa habari kutoka Klabu ya Uandishi wa Habari  (Zanzibar Press Club), pamoja na Menejiment ya Baraza la Habari Zanzibar, Tawi la Zanzibar (MCT) katika ukumbi wa Ofisis za MCT zilizopo Mlandege.


Amesema katika muelekeo wa baadae upatikanaji wa ajira katika tasnia ya habari, utapanuka sana kupitia sekta binafsi, ambazo zitakuwa na mahitaji maalum.

Aliwataka waandishi hao kujibidisha kitaaluma katika Nyanja mbali mbali, ikiwemo uchumi,siasa,  michezo, mazingira na nyenginezo ili kuwa tayari kukabiliana na mabadiliko hayo.

Akiihusisha na hoja hiyo, Waziri Mbarouk alisema hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeelekeza nguvu zake katika kufikia dhana ya ‘Utalii kwa wote’, hivyo ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa na taaluma ya kutosha juu ya utalii, hivyo kuitaka Press Club kujipanga vyema na kuwaandaa wanadishi wake katika muelekeo wa sekta hiyo.

“Uwezo wa waandishi wengi tulionao katika dhana ya uandishi wa habari maalum ni mdogo mno, MCT saidieni kuona wanadishi  wanakuwa na taaluma ya kutosha na kuehgemea katika nyanja maalum ’, alisema Mbarouk.

Aliwakumbusha waandishi hao umuhimu wa kuandika habari zilizo sahihi na zilizofanyiwa utafiti wa kutosha ili kuepuka upotoshaji wa taarifa.

Aidha aliiomba MCT kusimamia kimalilifu suala la maadili kwa waandishi wa habari kwa kigezo kuwa litajenga mustakbali mwema kati ya wadau wa habari  na jamii.

Katika hatua nyengine Waziri huyo aliahidi kusaidia juhudi za kulipatia ufumbuzi tatizo la ofisi linaloikabili klabu hiyo, kwa kigezo kuwa  mahala ilipo sio muafaka kwa kazi zilizokusudiwa.

 Aidha alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara yake kuangalia uwezekano wa kuwapatia nafasi za mafunzo waandishi wa kujietegemea (freelance), pale Wizara hiyo inapopata nafasi za masomo kwa waandishi wa Serikali.

Mapema Mratibu wa Baraza la Habari Zanzibar, Shifaa Said alimwomba Waziri Mbarouk kutoa msukumo wa kuyashughulikia mapendekezo ya Baraza hilo juu ya  uundwaji wa sheria za Habari.

Alisema kuna miswada miwili ya mapendekezo ya wadau kuhusu sheria za habari, ikiwemo ule wa Media Service Bill na ITI  ambayo tayari imewasilishwa Wizarani kwa kushughulikiwa kwa muda sasa.

Alisema sheria hizo ni muhimu katika uhai na  ustawi wa fani ya uandishi wa habari hapa Zanzibar.

Mapema kwa nyakati tofauti Waziri Mbarouk alipata fursa ya kuzitembelea taasisi za Press Club na MCT na kupata maelezo mafupi juu ya utendaji wa kaz za kila siku. 
    

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.