Na Khamis Amani
MGOMBEA wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hussein Ibrahim Makungu 'BHAA', amejitokeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Uwakilishi kwa Jimbo la Bububu.
Mgombea huyo alichukuwa fomu hiyo jana asubuhi katika ofisi za Tume hiyo wilaya ya Magharibi Unguja, iliopo Kilimani wilaya ya Mjini Unguja, majira ya saa tano asubuhi.
Bhaa, alichukuwa fomu hiyo, akiwa na umati mkubwa wa Wanachama wa Chama cha Mapinduzi, waliojitokeza kumsindikiza katika afisi hizo za Tume wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, na Mkuu wa Oganaizesheni, Asha Abdalla Juma, na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Yussuf Mohammed.
Uchukuaji fomu huo ulishuhudiwa kupambwa na mbwembwe mbali mbali za wanachama hao kwa kuhanikiza sare za chama hicho za kijani na njano, huku kikosi cha vijana wa mapikipiki na kikundi cha Chipikizi wa ngoma za Bras Band wakinogesha sherehe.
Mgombea huyo akiwa ndani ya gari lililombeba alionekana kufurahia zoezi hilo, jambo amabalo lilisababisha baadhi ya njia alizokuwa akipita kufungwa kwa muda kutokana na idadi kubwa ya wanachama waliomsindikiza katika afisi hizo za Tume.
Hussein, ambaye aliteuliwa na CCM, kuwania nafasi hiyo, alichukuwa fomu hizo akiwa ni mgombea wa sita tokea zoezi hilo lilipoanza Agosti 22, mwaka huu.
Wengine waliochukuwa fomu za kuwania nafasi hiyo, ni Juma Mitu Domo (SAU), Seif Salum Seif (TADEA), Issa Khamis Issa (CUF), Aboubakar Hamad Said (AFP) pamoja na Suleiman M. Abdulla (NRA).
Akimkabidhi fomu hizo, msimamizi wa uchaguzi wa wilaya ya Magharibi Unguja Suluhu Ali Rashid, alimtaka mgombea huyo kufuata taratibu zote za kisheria zilizowekwa na Tume hiyo, ikiwemo pia kurudisha fomu hizo katika wakati uliopangwa.
Suluhu alimpongeza mgombea huyo kuteuliwa na Chama chake kushiriki katika kinyang'anyiro cha nafasi hiyo, iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wake Salum Amour Mtondoo.
Zoezi hilo urejeshwaji wa fomu linatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2012 si zaidi ya saa 10:00 za jioni ambapo majina ya wagombea hao yatawekwa hadharani ili kuwawezesha waananchi wenye pingamizi kuweza kutumia nafasi hiyo kwa kuwasilisha mbele ya Tume hiyo kazi ambayo itafanyika ndani ya muda wa masaa 24.
"Ukija kurudisha fomu hizi utalazimika kuja na fedha taslimu shilingi 200,000 kama dhamana, utarejeshewa mwenyewe iwapo utapata zaidi ya asilimia 10 za kura zitakazopigwa katika uchaguzi, chini ya asilimia hiyo fedha hizo zitakuwa ni mali ya serikali", alifahamisha Suluhu.
Kwa mujibu wa msimamizi huyo wa uchaguzi wa wilaya hiyo ya Magharibi, kampeni za uchaguzi za kuwania nafasi hiyo zinatarajiwa kuanza Agosti 31 2012, hadi Septemba 15, 2012, na uchaguzi utafanyika Septemba 16, 2012.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu, unafanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mohammed Ali Mtondoo, kufariki dunia kutokana na kuugua ghafla maradhi ya kiharusi.
No comments:
Post a Comment