MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA BARAZA LA IDD EL FITRI MWEZI MOSI MFUNGUO MOSI, 1433 HIJRIYA, AGOSTI, 2012
Mheshimiwa Maalim
Seif Sharif Hamad,
Makamu wa Kwanza wa
Rais;
Mheshimiwa Balozi
Seif Ali Iddi,
Makamu wa Pili wa
Rais;
Mheshimiwa Dk. Amani
Abeid Karume,
Rais Mstaafu wa
Zanzibar;
Mheshimiwa Sheikh
Saleh Omar Kabhi,
Mufti wa Zanzibar;
Mheshimiwa Pandu
Ameir Kificho,
Spika wa Baraza la
Wawakilishi;
Mheshimiwa Omar
Othman Makungu,
Jaji Mkuu;
Mheshimiwa Sheikh
Khamis Haji Khamis,
Kadhi Mkuu;
Waheshimiwa
Mawaziri,
Waheshimiwa
Mabalozi,
Waheshimiwa Viongozi
wa Vyama vya Siasa,
Ndugu Wageni
Waalikwa,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana.
Assalam
Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh
IDD
MUBARAK WA KULLU AAM WAANTUM BIKHEIR
Nakupeni mkono wa Idd na natanguliza
shukurani kwa kukariri kwamba “sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye
ni vyake vyote vilivyomo Mbinguni na Ardhini. Na Akhera, sifa njema ni zake pia; Naye ni
Mwenye Hekima na Mwenye Ujuzi wa kila jambo”.
Katika Aya ya pili ya Surat Saba’ai,
Mwenyezi Mungu amesema: “Anajua yaingiayo katika ardhi na yatokayo
humo; Naye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu”.
Nimetanguliza aya hii kwa makusudi
wakati ambapo tumo katika sherehe za Idd baada ya kumaliza Mwezi Mtukufu wa
Ramadhan, mwezi unaoitwa Mwezi wa Mwenyezi Mungu. Huo ni mwezi ambao tumetekeleza amri ya Mola
wetu ya kufunga kama ilivyoelezwa katika Surat Al-Baqarah, katika aya maarufu
kwetu sote. Tunatarajia Msamaha na Rehma
zake.
Katika kutekeleza amri hii ya kufunga
sisi walengwa wa amri hiyo, yaani Waumini wa Uislamu tumepita katika kipindi
ambacho kinaweza kufananishwa na kipindi cha mafunzo na utoaji huduma katika Uislamu
ambacho kinakuja mara moja katika mwaka.
Matokeo ya mafunzo hayo ni kuibuka kwa umma wa Waislamu ambao wanamjali
Mola wa Walimwengu wote, viumbe wenye utaratibu katika maisha yao na wenye
nidhamu ya hali ya juu.
Ndugu
Wananchi,
Bila ya shaka yo yote, mwanafunzi huwa
na haki ya kusherehekea baada ya kumaliza mtihani na kutegemea kufaulu. Kwa hivyo, sisi tukiwa tumekamilisha kuufunga
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, tuna kila sababu ya kusherehekea. Kwa hivyo, kwa ukarimu na rehma zake Mwenyezi
Mungu nasi tunataraji kuwa tutafaulu, kama ilivyosema ile aya niliyoitaja. Lakini
mjuzi wa yote haya ni Mwenyezi Mungu. Katika kusherehekea sikukuu hii,
tuzingatie mafunzo tuliyoyapata kwenye mwezi wa Ramadhan; kwa kutofanya vitendo
vya maasi. Tuwe watiifu na tuwe
waadilifu na tuzingatie sheria za nchi.
Sherehe zetu kubwa ni sikukuu mbili za
Idd ambazo ni Idd el Fitr na Idd el
Hajj. Kwa mnasaba wa Idd hii ya kwanza
nitazungumzia kidogo juu ya mafunzo tuliyopata na baadae kugusia maana ya kusherehekea
lakini kabla ya hapo natoa pongezi kwa waumini wote kwa kumaliza Mwezi Mtukufu
kwa staha ifaayo. Nchi yetu ilifurahia
amani na utulivu na hata wageni waliokuwepo wakati huo wamesikika wakitoa
sifa. Wote waliotunza amani ya nchi yetu
wanastahiki pongezi. Aidha, natoa salamu
zangu za Idd kwenu na kwa wananchi wote, Zanzibar na Tanzania Bara. Huu ni wakati wetu wa kufurahi na kushereheka
baada ya Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Lakini wakati huo huo tupitie mafunzo tuliyopata katika mwezi huo
Mtukufu wa Ramadhan na tuwe tunafaidika nayo.
Ndugu
Wananchi,
Mafunzo makubwa kutokana na Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan, baada ya ibada ya saumu na kuwania ucha Mungu kwa njia
mbali mbali, ni yale ya kuwa watu wenye utaratibu mzuri na wenye nidhamu ya
hali ya juu. Binaadamu mwenye sifa hizi
ni mtu aliyekamilika kiutu.
Utaratibu na nidhamu tuliyojifunza ulitokana
na utiifu. Sote tulitii amri za Mola
wetu. Utiifu ni jambo ambalo limetajwa
katika Quran tukufu mara 13. Kwanza
limetajwa katika Surat Al Imran, Aya ya 132; “Na mtiini Mwenyezi Mungu na
Mtume ili mpate kurehemewa”.
Tena limetajwa
katika Surat An Nisaa Aya ya 59:”Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na
mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu, walio katika nyinyi. Na kama mtakhitilafiana juu ya jambo lo lote
basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu
na siku ya mwisho. Hiyo ndiyo kheri,
nayo ina matokeo bora kabisa”.
Ndugu
Wananchi,
Kuamrishwa kuwa na utiifu kuna sababu
zake. Kutokana na hilo tunafikia zile sifa za kuwa watu wenye utaratibu wa
mambo na pia kuwa na nidhamu ya hali juu kabisa na kutuwezesha kufanikiwa
katika maendeleo ya maisha yetu. Sifa
hizo zinatupelekea katika maisha bora kabisa.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wengi
wetu tulikuwa watiifu wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu na matokeo yake tulikuwa
na mshikamano, umoja, unyenyekevu, ukweli, wenye upendo na kusaidiana. Tulikuwa na utulivu wa nafsi na hatukuwa
waropokaji wa mambo bila ya kufikiri na kuzingatia.
Ndugu
Wananchi,
Jambo la kwanza ni kukumbushana na
kusisitiza suala zima la umuhimu wa kulinda na kuendeleza amani, utulivu na
mshikamano wetu ambao ndio siri kubwa ya mafanikio tunayoendelea kuyapata. Nimeamua kutumia fursa hii kwa kuzingatia
uzito wa siku ya leo kwa Waislamu wote na wananchi kwa jumla na kwa kuzingatia
amri ya Mwenyezi Mungu katika Quran aya ya 55 ya Suratul Adh-Dhaariyat
aliposema:
“Na endelea kuwakumbusha; maana ukumbusho huwafaa
walioamini”.
Jamii yetu ni ya watu waliochanganyika
sana, iwe kwa ndoa, kusoma pamoja, kufanya kazi pamoja, kusali pamoja au hata
kukutana mara kwa mara katika shughuli mbali mbali za kijamii na za kimaisha.
Katika hali kama hii tunapaswa kuihisi hali ya umoja tulionao ambao ndio
utakaotuwezesha kupanga mipango mbali mbali na kuitekeleza kwa kushirikiana na
Serikali kwa manufaa yetu na nchi nzima kwa jumla. Ni dhahiri kuwa maendeleo ya
mtu mmoja mmoja, vikundi na maendeleo yanayoletwa na Serikali kwa ajili ya watu
wake hayawezi kupatikana bila ya kuwepo hali ya amani na utulivu nchini. Haya yote yanatokana na utiifu, utaratibu na
nidhamu katika maisha.
Ndugu
Wananchi,
Katika siku za hivi karibuni, nchi yetu
imekabiliwa na viashirio vya kuondoka kwa amani, utulivu na mshikamano. Katika
kipindi hiki tumeshuhudia matukio mawili makubwa lile la tarehe 26, 27 na 28
Mei na la tarehe 20 Julai, 2012. Matukio haya yameitia doa jamii yetu na nchi
yetu ambayo imejijengea sifa nzuri ya amani na utulivu. Wahenga walisema “Thamani
ya amani anaeijuwa Yule iliyemponyoka”. Kuvuruga amani ni jambo la muda
mfupi sana lakini kuirudisha inachukuwa muda mrefu. Aidha, kuvunjika kwa amani
husababisha athari ya vitu na watu wasio na hatia. Natoa wito kwa wananchi wote
kuepuka vitendo vya uvunjaji wa amani na vinavyopelekea kuathiri watu na mali
zao.
Tunapaswa kuelewa kwamba vitendo kama
hivi vinaathiri sana jitihada za nchi yetu katika shughuli za maendeleo na
ukuaji wa uchumi hasa katika kuimarisha sekta ya utalii ambayo tumeamua kuiimarisha kwa kauli mbiu ya
“utalii
kwa wote” inayoambatana na mipango madhubuti. Matukio kama haya yanasababisha kuwakimbiza
wageni wanaopenda kututembelea. Sote
tunaelewa kwamba uchumi wa nchi yetu unategemea sana utalii ambao kwa sasa
unatupatia karibu asilimia 80 ya pato letu la fedha za kigeni. Baadhi ya nchi zinazojulikana katika utalii
kama vile Seychelles na Mauritius zinaendelea kupiga hatua na kutuacha
nyuma. Tufanye kila jitihada kwa lengo
la kuimarisha sekta ya utalii ili tusiachwe nyuma zaidi katika uchumi wetu na maisha ya
watu wetu.
Ndugu
Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii
kuwatanabahisha wanaopanga na kushabikia vitendo vya uvunjaji sheria, amani na
utulivu kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa
itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaosababisha vurugu na kukiuka
taratibu za kisheria. Hata hivyo,
napenda kuwanasihi wananchi wasijiingize kwenye vitendo vinavyopelekea
kuvunjika kwa amani na badala yake wafanye mambo ya uadilifu yanayozingatia
sheria ziliopo na maadili yetu.
Serikali ina wajibu wa kulinda haki na
uhuru wa wananchi wake na mali zao. Kwa mara nyengine tena nalipongeza Jeshi la
Polisi kwa kazi nzuri walioifanya ya kutuliza fujo zilizotokea.
Ndugu
Wananchi,
Tafauti ya mawazo na mtazamo baina yetu,
isiwe chanzo cha vitendo vya kuvunja amani na kutofuata sheria. Nchi yetu
inaongozwa na Katiba na sheria zinazozingatia misingi ya utawala bora, utamaduni,
mila na silka tulizoachiwa na wazee wetu za kustahamiliana na kuvumiliana kwa maslahi ya nchi yetu. Misingi
hii ndiyo iliyotuwezesha kufika hapa tulipo na kusifiwa na marafiki zetu mbali
mbali wa nchi za nje, majirani zetu na watalii wanaokuja kututembelea. Kwa
hivyo, ni vyema tuuendeleze ustaarabu huo.
Tutumie busara katika kuyatatua matatizo yetu yanapotokea, kwa njia ya
mazungumzo. Hii ndio njia peke yake
itakayoleta maelewano pale yanapokosekana. Mambo yote yanazungumzika. Hapana lisilozungumzika. Zanzibar tunao uzoefu mkubwa katika
kuutekeleza utaratibu huu. Kila mmoja
wetu ana wajibu wa kuzingatia utekelezaji wa haya ninayoyaeleza. Hili ni jukumu letu sote, viongozi na
tunaowaongoza; tuliopo Serikalini na waliopo kwenye taasisi na asasi zisizokuwa
za Kiserikali.
Lazima tushirikiane katika kuiendeleza
amani na utulivu nchini ili iwe chachu ya kusukuma mbele maendeleo ya nchi
yetu kwa haraka. Hapana njia yoyote ya
mkato itakayotusaidia katika kuijenga na kuiendeleza nchi yetu kwa haraka sana
isipokuwa kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana, kupendana, kuendeleza amani na
kuendeleza umoja wenye nguvu. Tukumbuke
usemi maarufu usemao umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Mwenyezi Mungu analitilia mkazo suala la umoja, mshikamano na kustahamiliana
katika aya mbali mbali katika Quran ikiwemo aya ya 46 ya Suratul Al Anfal aliposema.
“Na Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala
msizozane (msigombane); msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu zenu, na
vumilianeni (mstahamiliane). Bila shaka Mwenyezi Mungu yuko pamoja na
wanaovumiliana”
Hizi ni sifa ambazo leo tunapokuwa tunasherehekea
Idd el Fitr tunapaswa kuzizingatia na kuamua kuziendeleza katika maisha yetu ya
baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Huu
ni ufunguo wa maendeleo ya binaadamu.
Ndugu
Wananchi,
Ni dhahiri kwamba katika kipindi kifupi
tangu muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Umoja wa Kitaifa ulipoanza,
nchi yetu imeweza kupiga hatua kubwa katika nyanja mbali mbali za kijamii na
kiuchumi. Mafanikio hayo yamepatikana
kutokana na viongozi na wananchi kuishi kwa kushirikiana na kuvumiliana
kisiasa. Kwa upande wa Serikali,
viongozi tumekuwa na ushirikiano wa karibu ambapo tunafanya kazi kwa kuzingatia
misingi ya katiba, sheria na kuheshimiana kwa manufaa ya nchi yetu. Maendeleo
katika sekta ya miundombinu, elimu, afya, kilimo na kadhalika yameimarika ni kwa sababu
tumeanza vizuri na jitihada zinaonekana.
Aidha, misingi ya demokrasia na uwajibikaji imezidi kuimarika. Natoa wito kwa wananchi wote muendelee
kushirikiana na Serikali yetu katika kuyaendeleza mafanikio hayo.
Ndugu
Wananchi,
Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata
mafunzo mazuri katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kwa hivyo, hatuna budi
kutekeleza kwa dhati a suala la mani, utulivu na utiifu wa sheria ambazo
zinaendana na utaratibu na nidhamu katika mambo yetu ndani ya jamii na nchi
nzima kwa jumla.
Utaratibu ni ustaarabu ambao unaanzia
kwa mtu binafsi na kwenda mbele hadi kufikia katika familia yake, jamii na
hatimaye nchi nzima. Kama tunavyojua,
miongoni mwa utekelezaji wa sifa ya utaratibu ni kuwa na mipango. Kila mmoja wetu anajipangia nafsi yake,
familia yake na anapaswa kushiriki kupanga katika jamii na nchi nzima kwa jumla. Kuchangia katika maendeleo ya nchi ni wito
ambao unatokana na ile aya ya utiifu niliyoitaja kabla na ni jukumu letu sote,
kwani Wahenga wamesema, “Kidole kimoja hakivunji chawa”.
Nachukua fursa hii kuligusia jambo la
pili muhimu ambalo linalotukabili katika kutekeleza sifa za utaratibu wa maendeleo
ya nchi. Katika kipindi cha wiki moja ijayo,
nchi yetu itakuwa na zoezi la kuhesabu watu, yaani sensa, zoezi ambalo ni miongoni mwa utaratibu wa kupanga maendeleo
ya wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yo yote. Kushiriki katika sensa ni jambo la sheria na
ni zoezi ambalo nchi zote duniani zinalifanya kila baada ya miaka kumi (10) isipokuwa
kama itatokezea sababu isiyoweza kuepukika.
Matokeo ya sensa yanazipa Serikali taarifa halisi juu ya idadi ya watu
na mambo mengine muhimu katika kutayarisha mipango ya maendeleo.
Kwa hakika inasikitisha kusikia kuwa
kuna baadhi ya watu wanaowashawishi wenzao wasikubali kuhesabiwa kwa visingizio
visivyokuwa na msingi. Tutakumbuka kuwa nchi yetu imeshafanya zoezi la sensa
kwa vipindi mbali mbali huko nyuma kwa ufanisi mkubwa bila ya kuwepo kisingizio
chochote katika suala hili. Mafundisho
ya dini zote hayapingi suala la kuhesabiwa kwa nia ya kupanga na kuleta
maendeleo ya wananchi.
Kwa hivyo, natoa wito kwa wananchi wote
kutekeleza wajibu wao kwa kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kuwa wanahesabiwa
siku ya tarehe 26 Agosti, 2012. Tukiwa
Wazanzibari tuwajibike kufanikisha zoezi hili muhimu la kisheria kwetu na
tusiwape nafasi wasiotutakia mema katika mafanikio ya nchi yetu.
Ndugu
Wananchi,
Leo ni siku ya Idd. Hii ni siku ya kwanza ambapo Muislam humrejea
ruhusa yake ya kula na kunywa baada ya kujizuia navyo mchana kutwa katika mwezi
Mtukufu wa Ramadhan, akiwa amejitolea kwa ajili ya kupata radhi na msamaha wa
Mwenyezi Mungu.
Kadhalika, leo ni siku ya kwanza baada
ya Ramadhan, ambayo Muislam anahisi furaha mbili kubwa; furaha ya kutekeleza
wajibu wa kutii maamrisho ya Mola wake na furaha ya kupata malipo mema kutoka kwa Mola wake.
Mtume wa Mwenyezi Mungu, Sayyidna
Muhammad (SAW) alisema:
“Mwenye
kufunga ana furaha mbili: Furaha anapofungua na furaha anapokutana na Mola wake
– ama kwa ibada au kwa kupata malipo ya saumu yake”.
Miongoni mwa baraka za Idd ni
kudhihirisha umoja na mshikamano wa waislamu wa udugu, upendo, msamaha na
mahaba baina yetu . Nyoyo zinakutana
katika mapenzi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na kupendana kwetu kama ulivyo
mkusanyiko huu katika Baraza la Idd na kabla ya hapo katika jamaa za sala ya
Idd asubuhi yake na pia katika sala za taraweh.
Natoa pongezi kwenu nyote kwa kudhihirisha maneno ya Quran, Aya ya 10
Surat Al Hujurat “Kwa hakika waislamu wote ni
ndugu”.
Wakati huo huo, nawapongeza wananchi wote
kwa jumla, wakiwemo wasiokuwa waislamu kwa kushirikiana pamoja na kuupa mwezi
wa Ramadhan heshima yake. Huu ni ustaarabu
wa kujivunia. Pia, nawashukuru wakulima,
wavuvi na wafanyabiashara kwa kuhakikisha upatikanaji wa vyakula, nguo na
mahitaji mengine, wakati wa mwezi wa Ramadhan.
Masheikh wetu wanastahiki pongezi na
shukurani za pekee kwa kuendesha darsa za dini katika sehemu mbali mbali. Mwenyezi Mungu awalipe aliyowaahidi - Amin.
Ndugu
Wananchi,
Wakati tunasherehekea Idd el Fitr na
Inshaallah baada ya miezi mitatu tutasherehekea Idd el Hajj, inafaa tuwe na
hadhari juu ya mambo yasiyo mazuri katika jamii. Wakati huu wa Idd, wazazi tunapaswa kuwa
makini zaidi na waangalifu ili tuwaepushe watoto wetu wasipate madhara yo yote
yakiwemo ya ajali na mengineyo. Tuwe
waangalifu zaidi ili tuwawezeshe washerehekee
Idd kwa furaha.
Kabla ya kumaliza, ingawa leo
tunafurahikia Idd, lakini pia tuna wajibu wa kuwakumbuka wale walioathirika na
maafa ya kuzama kwa meli ya MV Skagit, tarehe 18 Julai. Leo tuna mayatima, vizuka, wazazi waliopoteza
watoto, wagonjwa na waathiriwa mbali mbali.
Tuwasaidie ipasavyo na tumuombe Mola wetu awape ndugu zetu hawa na sisi
subira na imani zaidi. Mwenyezi Mungu awalaze peponi wote waliopoteza maisha
katika msiba huo. Serikali imeshachukua
hatua mbali mbali kuhusu maafa haya. Katika kupunguza tatizo la usafiri wa baharini
nimekwishaipa maagizo Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango
ya Maendeleo kuhakikisha kwamba katika kipindi cha miezi miwili ijayo
wanakamilisha taratibu za kuagiza meli yetu wenyewe mpya, kubwa, kwa ajili ya
abiria na mizigo. Kwa uwezo wa Mwenyezi
Mungu katika kipindi cha miezi kumi na tano (15) ijayo tunatarajia meli hiyo kufika
nchini ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,000 na mizigo tani 200 itafika
hapa Zanzibar – Inshalla. Nina furaha
kupata taarifa kutoka Ofisi yangu inayohusika na Fedha, Uchumi na Maendeleo
kuwa fedha kwa ajili ya meli hiyo zitapatikana wakati wowote kuanzia sasa. Pamoja
na uamuzi huu, tutalifanyia mabadiliko makubwa Shirika la Meli la Zanzibar, ili
lijiendeshe kwa kufanya biashara kwa faida.
Ndugu
Wananchi,
Leo si siku ya kutoa hotuba ndefu kwa
kuwa kila mmoja wetu anataka kwenda kwenye shughuli za sherehe za Idd. Basi, tunaposherehekea tuwajali wenzetu ambao
hawana uwezo wa kufanya sherehe kutokana
na umasikini, afya na maradhi.
Tujitahidi kuwapa msaada watu wa aina hii, pamoja na kuwatembelea wagonjwa
na kuwapelekea zawadi. Pia, tuwafurahishe watoto wetu ili wawe na sikukuu nzuri
na tuwalinde na maovu. Waendeshaji wa
vyombo vya barabarani wachukue hadhari kubwa zaidi katika kipindi hiki cha
sherehe na maafisa wa polisi wafanye kazi ya ziada ili kuhakikisha kuwa usalama
barabarani na mitaani unakuwepo.
Tusherehekee Idd yetu kwa amani na utulivu. Kadhalika, tuwaombee taufiki
na Hijja ya kukubaliwa wenzetu walioazimia kwenda Hijja mwaka huu na Mwenyezi Mungu akiwajaalia kufika huko waiombee
salama, amani, baraka na kheri nchi yetu na wananchi wote kwa jumla.
Mwenyezi Mungu atuzidishie baraka na
mapenzi miongoni mwetu. Atuongoze katika
njia iliyonyooka na atuepushe
na kila shari. Atupe uwezo wa kuendeleza umoja, uvumilivu na
mshikamano nchini mwetu.
Kwa niaba yenu nimetuma salamu za Idd
kwa viongozi na waislamu katika nchi mbali mbali za kiislamu. Vile vile mimi na familia yangu nakupeni
mkono wa furaha ya Idd wananchi nyote.
IDD MUBARAK WA KULLU AAM
WAANTUM BIKHEIR.
Ahsanteni.
No comments:
Post a Comment