Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Quality Group Limited, imeamua kueongeza dola 20,000 za Kimarekani (zaidi ya shilingi milioni 30 za Tanzania) kutunisha zawadi za michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Yussuf Manji, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality na Mwenyekiti wa Yanga, alimpa ahadi hiyo Rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati klabu ya Yanga ilipomtembelea Rais huyo katika Ikulu Rwanda iliyoko kijiji cha Urugwiro nchini humo, hivi karibuni.
Hatua hiyo inazifanya fedha za zawadi kwa washindiwa michuano hiyo kufikia dola elfu 80 kutoka 60,000 zinazotolewa na Rais Kagame.
Mwaka 2002, Kagame aliweka rekodi ya kuwa mdhamini wa kwanza kutoa zawadi za mashindano hayo, dola 60,000 ambazo zimekuwa zikigawanywa kwa washindi watatu wa juu.
Mbali na zawadi hizo, Rais Kagame pia anatoa dola 15,000 kila mwaka kwa maandalizi ya michuano hiyo na kufanya mchango wake jumla kuwa dola 75,000.
Kutokana na mchango wake huo mkubwa, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeyapa mashindano hayo jina la Rais huyo.
Mwakani, michuano ya Kagame imepangwa kufanyika mjini Kigali kuanzia Januari, kwa mujibu wa Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye.
Musonye anatarajiwa kwenda Kigali mapema mwezi ujao kukutana na viongozi wa Wizara ya Michezo kujadili zaidi kuhusu maandalizi ya michuano hiyo.
Yanga ndio mabingwa wa kombe hilo kwa miaka miwili mfululizo, ambazo mara zote hizo mashindano yake yalifanyika Dar es Salaam, na hivyo kutimiza mara tano za kuvaa taji hilo.
No comments:
Post a Comment