Habari za Punde

Mufti Kaabi: Eid isherehekewe kiislamu


Hafsa Golo na Mwanajuma Mmanga
MUFTI wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi amewataka waislamu kusheherekea sikukuu ya Eid el Fitri bila ya kufanya maasi yanayomchukiza Mwenyezi Mungu.

Kiongozi huyo wa dini ya kiislamu alisema kuna tabia ya waumini kusherekea sikukuu ya Eid el Fitri kwa kufanya maasi na kuiga tamaduni za kigeni.

Mufti Kaabi alieleza hayo jana ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari hizi, ambapo aliwataka waislamu kusherekea sikukuu hiyo kwa msingi inayokubalika.

Alisema kusherehekea sikukuu za dini ya kiislamu kinyume na miongozo ni ya dini hiyo ni kujiweka kwenye hatima mbaya na kuisababishia jamii kukumbwa na majanga mbali mbali kutokana na maovu na machafu yanayofanywa.

Sheikh Kaabi alisema sikukuu ya katika dini ya kiislamu zimewekwa kuwa ni siku tukufu, hivyo sio vyema kuzisherehekea kwa maovu na machafu kwani kufanya hivyo ni kujichumia janga kwa kukaribisha ghadhabu za Mwenyezi Mungu.

Alisema siku hii ni siku ya kupata kibali cha ridhaa ya Mwenyezi Mungu, na fadhila zake hivyo ni vyema waumini wakatii maamrisho mema na kuepukana na mambo ya kishetani.

“Siku ya Eid el Fitri ni siku ambayo waislamu hutakiwa kukithirisha ibada kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, sio siku ya kutoka kifungoni kwa kuharibu swaumu kwa kufanya maovu”,alisema Sheikh Kaabi.

Aidha alisema uamuzi wa serikali kuweka muda wa sikukuu mwisho saa 12 uwe kwa wananchi wote na sio watoto peke yao ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kusherehekea sikukuu za dini ya kiislamu katika msingi ya kiislamu, kwani wahusika wakuu wa kufanya maasi ni watu wazima wenye akili timamu.

“Mtoto mdogo si rahisi kufanya maasi lakini watu wazima ndio wenye kufanya maasi katika siku za sikukuu, na wao ndio wanaovaa vimini na nguo za uchi, na wao ndio wanaotoka huo usiku kwa kwenda viwanjani kuendeleza kufanya maasi”,alisema.

Mufti huyo alisema athari mbalimbali hujitokeza baada ya kumalizika kwa sherehe za sikukuu ikiwemo kutoroshwa kwa watoto wa kike, kuongozeka kwa maradhi ya uasharati na hata ndoa zinazokiuka utaratibu na sheria za maamrisho ya dini ya kiislamu.

Sambamba na hayo alisema kuwa ofisi yake imepania kudhibiti matendo maovu ambayo yanasababisha kuondosha dhana ya sikukuu za dini ya kiislamu, hivyo wameamua kukua pamoja na taasisi husika zenye mamlaka ya kutoa vibali ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuporomosha maadili na mwenendo na taratibu za miongozo ya dini ya kiislamu.

Alisema katika kudhibiti ofisi yake imekutana na shehia 10 za wilaya ya Kati Unguja zikiwemo Jumbi, Tunguu, Jendele, Dunga na Urowa ambapo mashekhe na maulamaa wamefika kuelezea namna ya kusherekea dini hiyo kiislamu.

Alisema wamefurahishwa sana na uamuzi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wa kufuata mwenendo ulioamrishwa na mwenyezi Mungu, wa kusherehekea sikukuu za kiislamu katika misingi ya dini na kupiga vita upigaji wa ngoma katika viwanja vya sikukuu.

Pia alitoa wito kwa serikali ikiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa kuwa bega kwa bega katika kuzuia utowaji wa vibali vya kupingwa ngoma na miziki katika viwanja vote vya skukuu mjini na vijijini.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.