Habari za Punde

Wizara ya Miundombinu yabanwa . Mawaziri, Mwanasheria wasimama kuitetea. Waziri atangaza kuyakataa mafungu yaliyonona



Na Ramadhan Makame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi jana waliibana bajeti ya wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wakati wa kupitisha mafungu ya matumizi, huku wakihoji utendaji kwenye taasisi kadhaa za wizara hiyo.

Miongoni mwa vifungu vilivyohitaji ufafanuzi wa ziada wa serikali  ni pamoja na mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege, ulipaji wa fidia uwanja wa ndege, ujenzi wa barabara pamoja na kutuna kwa mafungu ya fedha zinazoombwa kwa safari.

Waziri mpya wa wizara hiyo, Rashid Seif Suleiman akisaidiwa na Naibu wake Issan Haji Ussi walilazimika mara kwa mara kusimama kutoa ufafanuzi na kujibu hoja wa wajumbe wa baraza hilo.

Aidha viongozi hao wa wizara hiyo walisaidiwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, waziri wa Nchi Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, pamoja na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed.


Kwa upande wake waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alisema atahaulisha matumizi ya vifungu vya fedha vilivyotononoka na vile vyenye matumizi yasiyo ya lazima kutoka Idara na wizara mbali mbali za serikali.

Waziri huyo alisema atalazimika kuvipitia vifungu hivyo vilivyotononoka na visivyo na matumizi muhimu ili aweze kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein, alilopewa wiki moja iliyopita la kutafuta fedha za ununuzi wa meli mpya.

“Nataka niwatoe hofu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya mafungu ya fedha ambayo hayana matumizi muhimu kuwa fedha hizo tutazihaulisha na tutazichukua kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya”,alisema waziri huyo.

Alisema vifungu vya fedha vitakavyohaulishwa na kupelekwa kwenye ununuzi wa meli mpya ni pamoja na safari za nje, semina, vikao na vuburudisho.

Waziri huyo alieleza hayo baada ya Mwakilishi jimbo la Mji Mkongwe, Ismal Jussa Ladhu kuonesha wasiwasi juu ya nyongeza maradufu ya fedha kwenye vifungu mbali mbali, akieleza kuwa ipo hofu ya kuwanufaisha zaidi watendaji.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa serikali, alisema kulijitokeza utata wa kisheria katika ujenzi wa jengo jipya la Uwanja wa ndege wa Zanzibar, ambapo kulikuwa na mikataba miwili yenye kima tofauti cha fedha iliyosainiwa tarehe moja.

Alisema pamoja na kumalizwa kwa tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo, lakini utata huo ilikuwa ni moja jambo gumu kuwahi kukumbana nalo katika utatuzi wake.

“Nikiri hili lilikuwa tatizo la kisheria, baada ya kuzungumza na wenzetu hivi sasa tumelimaliza na tuna mkataba mmoja”,alisema Mwanasheria huyo.

Awali akitoa ufafanuzi, waziri wa wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif Suleiman alisema ameingia katika wizara hiyo akiwa ameshajiwekea vipaumbele ambavyo atavitekeleza.

Alivitaja vipaumbele hivyo ni pamoja kulishughulikia suala la usalama wa wananchi wanaosafiri baharini angani na nchi kavu, matumizi ya fedha za umma, kuleta ufanisi katika utendaji pamoja na mashirika kufanya kazi kwa upeo na ufanisi.

Wakati wa kupitishwa mafungu ya matumizi ya wizara hiyo, Mwakilishi wa Mji mkongwe Ismail Jussa Ladhu, alisimama na kupiga buti akisema hakuridhishwa na majibu ya waziri na Naibu waziri wa wizara hiyo.

“Majibu ya waziri na Naibu waziri hayaridhishi na hiyo inathibitisha uoza wa wizara, kwanini mapato ya Mamlaka za wizara hiyo hayaonekani”,alihoji Mwakilishi huyo.

Hata hivyo Mwakilishi huyo aliwalalamikia watendaji wa wizara hiyo akisema kuwa hawawajibiki na wamekuwa wakitafuna ovyo fedha za wananchi.

Jussa alitishia kutaka kutoka katika kikao hicho huku akiwataka wawakilishi wenziwe waisusie bajeti ya wizara hiyo hadi pale Dk. Ali Mohamed Shein atakapoipanga wizara hiyo kwa kuteua watendaji wapya.

Hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa serikali alisimama na kueleza bajeti ipitishwe na kama kuna watendaji ambao hawawajibiki ipasavyo ni mamlaka ya uteuzi kuona lini inawawajibisha na sio kupewa shindikizo kupitia upitishaji wa bajeti.

“Tumuachilie Rais naamini anatusikia ataangalia tatizo liliopo kwenye wizara hii, kama ni utendaji ama uongozi”, alisema Mwanasheria huyo.

3 comments:

  1. Jambazi kubwa la wizara hiyo ni Katibu Mkuu. Hapa Rais lazima amuwajibishe kwani hili jamaa limejaa midudu ya RUSHWA. Halkadhalika mitendaji karibu yote katika wizara hii ni mikereketwa ya CCM ambayo ni mibovu, wala rushwa lakini hakuna anoweza kuigusa. Pia kuna tetezi eti Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi (Nzasa - asojua hili ndilo jina lake halisi alilokujanalo Unguja kutoka huko alikozaliwa kabla ya walezi wake familia ya marehem Sk. Amour Ali Ameir Al Marhouby kulidilisha na kumpa jina la Ali)kwamba alijaribu kumuomba Rais Sheni amrudishe Mustafa Aboud Jumbe katika ile nafasi yake pale bandarini, lakini inasemekana amegonga mwamba, kwani haja yake yarudi yale yale ya zamani wakati wafanyaji kazi pale bandarani hawataki hata kumsikia huyo Mustafa.

    ReplyDelete
  2. Wewe muache huyo mzee wa watu in peace. Issue hapa ni aliekuwa waziri Bw. Hamad Masoud na sio Mhe Ali Hassan. Unataka kumtukana Mhe Ali Hassan anza article yako mwenye na sio hii hapa. Hamad Masoud alikuwepo wapi uozo huu wa Contracts 2 kwa project moja unatokea?????? Hakuweza kumdhibiti huyo Katibu Mkuu? Inaonesha Bw. Hamad mwenyewe alikuwa ni uozo na kule kwenye Mzalendo.net kaelezwa vizuri kama ninavyoyanukuu hapa!
    "
    Said Sudi 08/08/2012 kwa 10:21 um · Jibu
    Sasa wengine ndio tunafahamu kwanini waziri aliepita wa wizara ya Mawasiliano na Miundombinu anataka kupelekwa korti. Kumbe wenzetu waliyaona zamani haya na sio ya MV Skagit tu.
    Ikiwa Mhe Jussa ambae sote tunamuamini “alitishia kutaka kutoka katika kikao hicho huku akiwataka wawakilishi wenziwe waisusie bajeti ya wizara hiyo hadi pale Dk. Ali Mohamed Shein atakapoipanga wizara hiyo kwa kuteua watendaji wapya”, hii inamaana waziri aliepita Shk Hamad Masoud aliiozesha kweli hii wizara!!!!
    Inatia uchungu vipi Shk Hamad Masoud alikuwa ovyo hivi hata nd. Jussa anasikitika hivi.
    Mikataba miwili ya project ya Uwanaj wa Ndege inatiwa sahihi siku moja na halafu wengine mnasema huyu waziri asipelekwe korti!
    Shk Jussa ninakuvulia kofia. Huku ndio kuweka maslahi ya nchi mbele na ya chama chako nyuma!
    Ninakupa mkono wa EID Shk Jussa na mapema sana na ahsante kwa kutupigania sisi wanyonge na tusio na hali katika Zanzibar hii ya leo.
    JUSSA FOR THE PRESIDENCY IN 2015!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!"

    ReplyDelete
  3. JAMANI NIMEONA HILI SHIRIKA LA MAGARI LINATAKA KUVUNJWA CHINI YA WIZARA YA BIASHARA LKN JEEE TULITIZAMENI HILI SHIRIKA LA MELI LINAFANYA NINI??? HALINA HATA MELI 1 BAADA YA UKOMBOZI TENA WAMEIKODISHA TUJIULIZE MASWALI HUYU MKURUGENZI WAO ALHAJJ SURURU ANA FANYA NINI???? BAADA YA KUJENGA MIJUMBA MIKUBWA MIKUBWA BEITRASS, KIBWENI NA PIA MBWENI NA TUNAONA ANA MIRADI MIKUBWA MIKUBWA LKN WANAMTIZAMA TUUU ATI KUWA NI MTOTO WA MWANA AFRO SHIRAZI ANAZIUNGUZA PESA ZA WAZANZIBARI WALALAHOI LKN HILI SHIRIKA WALA HALITIZAMWI KAMA LINAVOZITAFUNA PESA ZA NCHI USHAURI WANGU LIBINAFSISHWE LINAENDESHA HASARA SEREKALINI WITH NO RETURNS

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.