Habari za Punde

Zoezi la sensa laongezwa kwa siku tatu Arusha

Na Mustafa   Leu, ARUSHA
MKOA wa Arusha, umeongeza siku tatu zaidi kuanzia leo Jumapili hadi Jumanne Septemba kwa ajili ya kukamilisha zoezi la kuhesabu sensa ya watu na makaazi kutokana na wananchi wengine kutokufikiwa kwenye zoezi hilo kutokana na sababu mbalimbali.

Mratibu wa sensa mkoa wa Arusha Margaret Martin, alisema mpaka sasa mkoa umefikia asilimia 95 ya kuhesabu sensa ya watu na makazi na hivyo umelazimika kuongeza siku hizo ili kutoa fursa kwa wananchi ambao hawakuhesabiwa waweze kushiriki na kuhesabiwa ili kuweza kupatikana kwa idadi kamili ya watu mkoani humo.

Alisema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha kamati ya sensa ya mkoa kilichofanyika Agosti 30 kufuatia kupokelewa kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi waliofika ofisini wakidai hawajaona makarani wa sensa katika maeneo yao.

Mratibu huyo alisema kutokana na malalamiko hayo imelazimika kuongeza siku chache ambazo zitakamilika Jumanne ili kutoa fursa wananchi ambao inakadiriwa kuwa ni asilimia tano waliobakia waweze kuhesabiwa katika zoezi hili.

Alisema zoezi hilo lilikumbwa na matatizo katika kijiji cha Osunyai, wilayani Longido, ambapo lililazimika kusimama kwa siku tatu kutokana na wanyama, wakiwemo Tembo na Simba, kukaa kwenye kijiji hicho kwa siku tatu na hivyo kuwazuia makarani wa sensa kuendelea na zoezi hilo hadi walipopatikana askari wa wanyamapori ambao waliweza kuwafukuza na zoezi hilo kuendelea.

Alifahamisha kuwa zoiezi hilo lililoanza nchini kote Agosti 26 mwaka huu na kukamilika ndani ya siku saba lilikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kutokuacha taarifa kwenye majumba yao pindi wanapokwenda katika shughuli zao.

Wengine walitumia mbinu chafu za kuweka alama ya mkasi kwa kutumia chaki nyeupe, kwenye nyumba zao wakiashiria kutokukubali kuhesabiwa  hali iliyowafanya makarani kushindwa kuwahesabu lakini mratibu wa sensa alipogundua mbinu hizo alilazimika kubadilisha na kuweka alama nyekundu ambayo hawawezi kuifuta ili kuashiria kuwa nyumba hizo hazikuhesabiwa katika zoezi la awali.

Changamoto nyengine ni ongezeko kubwa la watu katika miji tofauti na makasio ya awali hivyo kusababisha madodoso yaliyokuwa yameaandaliwa  kutokutosheleza  mahitaji.

Vifaa vichache kufika katika eneo kutokana na gharama kuwa kubwa, kukumbwa na matukio yaliyohitaji  fedha za haraka  kuyatatua  mfano la Simba na Tembo kuvamia kijiji cha Osunyai, wilayani Longoido, na kusababisha mtafaruku  kwa makarani wa sensa na watendaji wa kata na vijiji.

Pia Wilaya ya Ngorongoro kuhitaji fedha zaidi tofauti na bajeti kutokana na jiografia yake kuwa ni ngumu kufikika kwa mara moja, viongozi wengi  kujitokeza katika eneo moja kuwaongoza makarani na kusababisha sintofahamu kwa watendaji na makarani wa sensa.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.