Lampard apiga 2 akianza kuaga Bridge
LONDON, England
FRANK Lampard, jana alijikumbusha uwezo wake wa kuzifumania nyavu alipoifungia klabu yake ya Chelsea mabao mawili muhimu katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Everton, kwenye mechi ya ligi kuu ya England.
Ushindi huo umeipaisha Chelsea hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo ya Barclays, na kuongeza utamu wa resi za kuwania ubingwa kati yao na Manchester United na City.
Watoto hao wa darajani wamefikisha pointi 38 baada ya kushuka dimbani mara 19, nyuma ya Manchester City inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 42 kutokana na mechi 20 ilizocheza hadi sasa.
Usukani wa ligi hiyo unakamatwa na Manchester United ambayo pia imecheza mechi 20, ikiwa na akiba ya pointi 49.
Katika mechi ya jana iliyochezwa nyumbani kwa Everton katika dimba la Goodison Park, Chelsea ilionesha mchezo mzuri ingawa ilishindwa kutumia nafasi nyingi za kupachika magoli ilizozipata.
Hata hivyo, walikuwa wenyeji walioanza kuzisalimia nyavu za Chelsea mnamo dakika ya pili, kwa bao la Steven Pienaar aliyeuwahi mpira wa mchezaji mwenzake Victor Anichebe ambao uligonga nguzo na kurudi uwanjani.
Goli hilo lingedumu hadi wakati wa mapumziko, lakini Frank Lampard ambaye ameshapewa ruhusa ya kuondoka darajani msimu wa kiangazi, akasawazisha katika dakika ya 43 kwa mpira wa kichwa akiunganisha krosi iliyomiminwa na Ramires.
Baada ya timu hizo kuwa sare kipindi cha kwanza, wachezaji wa pande zote walianza ngwe ya pili kwa kasi na kuwaweka walinda milango katika wakati mgumu, huku Nikica Jelavic akishindwa kuifungia Everton baada ya shuti lake kugonga mwamba.
Lampard aliihakikishia Chelsea pointi tatu muhimu alipomudu kuandika bao la pili katika dakika ya 72 ya mchezo na kuifanya timu yake itoke uwanjani kifua mbele (BBC Sports).
No comments:
Post a Comment