Habari za Punde

Kibaki Aagiza Ulinzi Mkali Chumba cha Kujumlisha Kura


Na Mwandishi maalum, Kenya

SERIKALI imetangaza ukumbi wa Bomas kuwa eneo lisilo la kuingia na kupita kiholela kuanzia sasa hadi shughuli ya uchaguzi zimalizike.
Kwenye kikao na Tume ya uchaguzi nchini (IEBC),Rais Mwai Kibaki ameviagiza vyombo vya usalama kuhakikisha ukumbi huo umewekwa chini ya ulinzi mkali kwa kuwa ndio utatumika kujumlisha hesabu ya kura kutoka kote nchini.
Aidha ukumbi huo ndio utatumika katika kutangazwa mshindi wa urais punde baada ya kumalizika hesabu ya kura.

Taarifa rasmi kutoka Idara ya habari za Rais (PPS), Rais ameridhia ujumbe wa awali wa Inspekta Mkuu wa Polisi kwamba maafisa 90,000 wa polisi wanatumwa kote nchini kushika doria wakati wa kampeni za mwisho na upigaji kura.
Kwenye mkutano huo katika afisi rasmi ya Rais Harambee House, Tume ya IEBC ilimhakikishia rais na wa Kenya kwamba imejiandaa kuandaa uchaguzi huru na haki.
Mwenyekiti wa Tume, Isaac Hassan alisema kwamba tayari wamekutana na wagombea urais na kuwafahamisha utaratibu wa upigaji kura na sheria za uchaguzi.

Wakati huo huo taarifa ya Jaji Mkuu imeendelea kuibua hisia kali nchini Kenya siku moja baada ya kutolewa.
Mapema jana vigogo wa muungano wa Cord, Waziri Mkuu Raila Odinga na Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka wamemtaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Kimemia kujiuzulu.
Kwenye kikao cha wanahabari katika uwanja wa ndege wa Wilson wawili hao wamesema Kimemia amekuwa akitumia vibaya mamlaka yake akiwa mkuu wa utumishi wa umma.
Raila alisema taarifa ya Jaji mkuu inathibitisha kwamba Kimemia anatumia idara ya utawala wa mikoa kuendeleza kampeni za muungano wa Jubilee kwa hivyo hafai kuendelea kuhudumu kwenye utumishi wa umma.
Wengine walioelezea hisia kali kuhusu kisa cha kutishwa kwa Jaji Mkuu ni mpeperushaji bendera ya muungano wa Amani Musalia Mudavadi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.