Habari za Punde

Tume ya Pinda kuanza kazi


Na Kunze Mswanyama,DSM
TUME iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuchunguza chanzo cha matokeo mabaya ya kidato cha nne inatarajiwa kuanza kazi zake ndani ya siku mbili.

Tume hiyo inayojumuisha wajumbe kutoka Chama cha Walimu (CWT),serikali,Asasi za kiraia zinazojishughulisha na sekta ya elimu na Idara nyingine,iliundwa hivi karibuni.

Matokeo hayo yanayoonesha zaidi ya watoto 240,000 sawa na aslimia 60 wamefeli.

Baadhi ya wadau wameanza kuponda tume hiyo wakisema uundwaji wa tume umekuwa ukifanywa hadharani lakini matokeo yake hufichwa na bila kuelezwa wazi kwa wananchi.

Akifungua mazungumzo ya kujadili namna ambavyo sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na serikali (PPPs) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam,Waziri Mkuu alisema wanakamilisha taratibu za mwisho ili tume hiyo ianze kazi mara moja.

Alisema,wanaopinga tume hiyo hawana jipya na kuwa kutokana na baadhi ya wananchi kudai kosa ni la serikali huku wengine wakitupia lawama walimu na wanafunzi,Pinda alidai tume hiyo inatarajiwa kuja na majibu ya maswali hayo.

Pinda alikiri uwepo wa malalamiko ya wadau wa elimu kuwa tume hiyo haina tija lakini akasema baada ya tume hiyo kuingia kazini wananchi watapewa kile walichokibaini na kuahidi kuwa kitendo hicho hakitajirudia tena.

"Wanaolalamika ni kutokana na kuchukulia suala hili kwa wepesi sana,jamani suala hili ni kubwa sana na inabidi serikali kulifanyia kazi kutokana na namna jambo lenyewe lilivyo," alisema Pinda.

Aliongeza kuwa,hakuna anaeweza kukaa kimya wakati zaidi ya vijana 400,000 wamefeli mitihani yao na hawajui hatma yao ya baadae hivyo kuwataka wananchi kuacha kulalamikia kila serikali inapofanya jambo kwa manufaa ya nchi.

Awali Pinda alisema,serikali inaangalia upya sheria za mahusiano na mikataba baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP), ambapo alidai kuwa wanatarajia kuitumia sekta binafsi katika uwekezaji kwenye miradi mikubwa ambapo serikali itakuwa ni msimamizi wa jumla.

Alisema, serikali itakuwa ikikusanya mapato kutokana na uwekezaji huo ambapo mwekezaji hupewa miaka mingi ili ajilipe gharama zake na mara amalizapo hutakiwa kuurudisha mradi huo serikalini ili uendeshwe kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.