Na Mwantanga Ame
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imesema haina mpango wa kuitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano kuipatia gawio la mapato ya muungano ili kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu.
Naibu Waziri wa wizara hiyo,Zahra Ali Hamad, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma aliyetaka kujua kwa nini serikali isifikirie kuomba gawio la asilimia 4.5 kutoka serikali ya Muungano.
Naibu Waziri alisema serikali haina mpango wa kuchukua hatua hiyo kwa sasa na ni vyema suala hilo kama linatakiwa kuwepo ni vyema likaaandaliwa mapendekezo katika kamati ya pamoja ya fedha.
Alisema ni vyema mapendekezo hayo yangelipelekwa huko kwa vile Kamati hiyo ndio inayoshughulikia mambo mbali mbali yanayohusiana na mgawanyo wa fedha katika serikali zote mbili.
Alisema serikali katika utoaji wa mikopo hiyo, imekuwa ikizingingatia zaidi vigezo vya msingi kwani Bodi ya Mikopo ya Tanzania imekuwa ikiwapatia mikopo wale wanafunzi waliokosa kukopeshwa na mfuko wa elimu ya juu Zanzibar.
Alisema ni kweli suala la elimu ya juu ni mambo ya muungano lakaini kasma inayotokana na mgao wa asilimia 4.5 hutokana na fedha za faida ya Benki Kuu na misaada ya fedha za wahisani hazihusiani na mgao wa kasma za bajeti za ndani inayoidhinishwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Kuhusu vigenzo vya kukopeshwa,alisema wanafunzi wa Zanzibar 237 walipewa mikopo lakini jambo la kusikitisha baada ya kufanyiwa uchunguzi walibainika walikuwa tayari wameshachukua mikopo katika Bodi ya Elimu ya Juu Tanzania.
No comments:
Post a Comment