Habari za Punde

Oman kugharamia wanafunzi elimu ya juu

Othman Khamis Ame, OMPR
 
Serikali ya Oman inakusudia kusaidia  kugharamia wanafunzi wa Zanzibar wanaopata fursa ya kuendelea na  masomo ya ngazi ya juu kwenye vyuo vikuu tofauti Nchini humo pamoja na vile vilivyopo hapa Nchini Tanzania.
 
Hatua hiyo imekuja kufuatia maombi yaliyotolewa na Zanzibar kwa Nchi hiyo ambapo taratibu  zimeshaidhinishwa kupitia  mpango maalum wa Mfalme Qaboos Bin Said wa Nchi hiyo.
 
Balozi wa Oman Nchini Tanzania Bwana Yahya Moosa Al – Bafry alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 
Balozi Yahya Moosa alisema Mpango huo wa Mfalme Qaboos umelenga katika azma yake ya kuimarisha uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Nchi yake na Zanzibar ambao ni wa Kihistoria.
 
Balozi Yahya alimuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano huo wa pande mbili hizo utaendelea kuimarishwa kwa vizazi vya sasa ni vile vijavyo.

“ Si muda mrefu ujumbe wa Zanzibar  akiwemo mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA } ulikwenda Nchini Oman kwa mazungumzo ya kujenga mazingira ya kuelekea kwenye Mpango huo muhimu kwa ustawi wa Elimu kwa Vijana wa Zanzibar “. Alisisitiza Balozi Yahya Moosa.
 
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar itaendelea kuiona Oman kama mshirika wake katika uhusiano wa Kihistoria na Utamaduni unaooana baina ya wananchi wa pande hizo mbili .
 
Balozi Seif Ali Iddi alieleza kwamba Wananchi wa Zanzibar na Oman wamekuwa wakiishi kama ndugu kutokana na maingiliano yao ya  kidamu yaliyodumu kwa karne nyingi zilizopita.
 
Balozi Seif alisema mpango huo wa Oman wa kujitolea kwake kuunga mkono harakati za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuwajengea uwezo vijana wake utakaoiwezesha Zanzibar kwenda sambamba na mabadiliko makubwa ya Teknolojia Duniani.
 
Mazungumzo hayo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Balozi wa Oman Nchini Tanzania Bwana Yahya anayefanya kazi zake Mjini Dar es salaam yameshuhudiwa  pia na Balozi mdogo wa Oman hapa Zanzibar Bwana Sabhi Sulaiman.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.