Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akipokea vitabu vinavyohusu kilimo cha mboga mboga kutoka kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya TAHA COLMAN NGALO, walipokutana ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa kilimo kutoka Finland, jumuiya ya TAHA na watendaji wa Wizara ya Kilimo Zanzibar ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wadau wa kilimo kutoka Finland na jumuiya ya TAHA ofisini kwake Migombani. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar, Affan Othman Maalim. (Picha na Salmin Said, OMKR).
Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amepongeza hatua ya Wizara ya Kilimo kushirikiana na washirika mbali mbali wa maendeleo katika kuendeleza kilimo cha mboga mboga nchini.
Amesema kilimo hicho ni muhimu katika kuongeza pato la wakulima na kupunguza tatizo la ajira linalowakabili wananchi wengi wa Zanzibar.
Akizungumza na wataalamu wa kilimo hicho kutoka Finland na Jumuiya ya kilimo cha mboga mboga Tanzania (TAHA), ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema Zanzibar ambayo ina eneo dogo la kilimo, inaweza kupata mafanikio mazuri iwapo litatumika vizuri kulima kilimo kinachokwenda na wakati kikiwemo cha mboga mboga na viungo.
Amefahamisha kuwa kilimo cha aina hiyo kinaweza kuwakomboa wakulima kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Amewasisitiza wakulima kuwatumia wataalamu wa kilimo ili kuweza kuzalisha mazao yenye ubora ambayo yataweza kuhimili ushindani wa soko la mazao hayo.
Ameahidi kuwa serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha kuwa wataalamu na jumuiya hiyo wanafanya kazi zao vizuri katika kuendelea kilimo hicho ambacho kitasaidia kukuza uchumi na pato la wananchi.
Nae mwenyekiti wa jumuiya ya (TAHA) COLMAN NGALO amesifu mashirikiano mazuri waliyoyapata kutoka Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar katika kuendesha shughuli zao za kuwashajiisha wakulima katika kilimo hicho.
Amesema chini ya jumuiya hiyo wamekuwa wakiwahimiza wakulima kujishughulisha na kilimo cha kibiashara, kutoa mafunzo kwa wakulima wa mboga mboga pamoja na kuwapa taarifa za mara kwa mara juu ya upatikanaji wa soko la mazao hayo.
Ngalo amefafanua kuwa ikiwa kilimo hicho kitaendelezwa kitaleta faida kubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake mtaalamu wa kilimo hicho kutoka Finland TIIMA HUVIO mesema watafanya kazi kwa karibu na vikundi vya wakulima ili kuona kuwa wanaongeza uzalishaji na ubora wa mazao yao.
Amesema ni lazima wakulima wawekewe msisitizo kuzalisha bidhaa bora zitakazoweza kuwavutia wateja na hatimaye kuweza kukidhi matakwa ya wakulima na mahitaji ya wateja.
No comments:
Post a Comment