Yawatowa Hofu Watalii, Wageni.
Mungu wa Mabaniani Bado Hajapatikana.
Polisi Watumia Magari, Pikipiki Kuimarisha Doria.
Na Juma Khamis, Ameir Khalid
SERIKALI imetangaza bingo la shingi milioni 10 kwa watu wataotoa taarifa za kupatikana wahalifu waliowamwangia tindi kali raia wawili wa kike wa Uingereza.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Sid Ali Mbarouk aliwambia waandishi wa habari jana ofisini kwake Mnazimmoja.
Alisema serikali pia itadhibiti uingizaji, usambazaji na matumizi ya tindikali na kuwataka wafanyabiashara wanaoingiza tindikali kushirikiana na serikali.
Kuhusu utalii, alisema serikali kwa kushirikiana na Ubalozi mdogo wa Uingereza na ubalozi wa nchi hiyo uliopo Tanzania wanafanya mazungumzo ili kuwahakikishia usalama watalii wanaotembelea Zanzibar akisema nchi iko salama na kuwahakikisha watalii ulinzi.
Aidha alisema serikali inalani tukio hilo kwa nguvu zote na kuahidi kwamba kwa kushirikiana na vyombo vya usalama wahusika watatiwa mbaroni.
Kwa niaba ya serikali ametoa pole kwa majeruhi, familia na serikali ya Uingereza na kuvitaka vyombo vya habari vya ndani na nje viache kuitangaza Zanzibar vibaya.
Raia hao wanaofanya kazi za kujitolea wenye umri wa miaka 18, wamejeruhiwa baada ya kumwagiwa maji yanayosadikiwa kuwa tindikali katika maeneo ya Vuga mjini Zanzibar majira ya saa 12:30 jioni juzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam akizungumza kwa njia ya simu jana, alisema tukio hilo limetokea baina ya ofisi za Shirika la Bima Zanzibar na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Alisema vijana hao wa kike Kate Gee na Kirstie Trup wanafanya kazi na Shirika la Arts in Tanzania lenye ofisi zake Kiponda mjini Zanzibar.
Alisema walikuwa wakitembea kwa miguu kutoka maeneo ya Vuga kuelekea Shangani na walipofika maeneo hayo ndipo walipokutana na vijana wawili waliokuwa wamepanda vespa na kuwamwangia maji hayo na kisha kukimbia.
Alisema vijana hao walikuwepo nchini kwa muda wa wiki mbili na nusu sasa na walitarajiwa kurejea nyumbani kesho.
Alisema baada ya tukio hilo, waliwahi kunywa kiwango kikubwa cha maji ili kupunguza madhara na baadae juzi usiku walisafirishwa hadi Dar es Salaam kwa matibabu.
Kamanda Mkadam alisema vijana hao wanatibiwa katika hospitali Agha Khan jinini Dar es Salaam na wanatarajiwa kurudi nyumbani kesho.
Alisema hawakupata majeraha makubwa ambapo mmoja ameumia kidogo sehemu ya uso karibu na jicho na mwengine sehemu ya mabega.
Hata hivyo, Kamanda Mkadam alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kuwasaka vijana hao.
Aliwataka wananchi kutokuwa na hofu kwani polisi wameimarisha doria kubwa kuanzia barabarani na maeneo mengine ikiwemo Mjini Mkongwe.
Mwandishi wa habari alishuhudia magari yenye askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wenye silaha yakifanya doria katika barabara zote za Mkoa wa Mjini Magharibi katika kipindi hichi ambacho Waislamu na wananchi kwa ujumla wanasherehekea sikukuu ya Eid el Fitri iliyoanza leo.
Kamanda Mkadam alisema polisi wamejipanga vya kutosha kukabiliana na aina yoyote ya uvunjaji wa sheria na kuwatahadharisha vijana wanaobeba silaha kwenye viwanja vya sikukuu waache kufanya hivyo, kwani mtu atakaekamatwa atahifadhiwa hadi sikukuu imalizike.
Kuhusu Mungu wa mabaniani alieibiwa katika Jamat la Kiponda, Kamanda Mkadam alisema polisi wanaendelea kuwatafuta wahusika ingawa anaamini wahusika ni waumini kwa Jamat hilo.
Nacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeelezea kulipokea tukio hilo kwa mshituko, masikitiko na huzuni kubwa.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Waride Bakari Jabu, imeviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kuwasaka, kuwakamata na kuwafikishwa wahusika kwenye vyombo vya sheria.
Imesema kitendo hicho kinakwenda kinyume na kukiuka misingi ya utu pia kuvunja haki za binaadamu na kwamba hakikubaliki katika jamii ya wapenda amani, umoja na mahusiano mema yaliyopo kati ya Tanzania na Uingereza.
Taarifa hiyo ilisema ni wakati muafaka kwa vyombo vya ulinzi vya ndani kwa kushirikiana na vile vya nje viendelee kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaka watu, makundi na wahalifu wanaofanya ukatili huo.
CCM kimetoa mkono wa pole kwa waathiria, familia zao na kutuma ujumbe wa simanzi kwa balozi wa Uingereza nchini na kuwaombea kwa Mungu wapone haraka.
Wakati huo huo Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu ambako tukio hilo limetokea, amelaani vikali tukio hilo.
“Nikiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, mwananchi wa Zanzibar ninayeipenda nchi yangu na pia nikiwa kama binadamu ninayethamini utu wa kila mtu nalaani vikali na kwa nguvu zote uovu na uhalifu huo ambao umekiuka misingi ya ubinadamu na utu,” alisema.
Aliwaomba Polisi na mamlaka nyengine za nchi kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka wa kuwajua waliohusika na tukio hilo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Alisema tukio hilo linakwenda moja kwa moja na kupiga moyo wa uchumi wa Zanzibar ambayo inategemea zaidi utalii.
Aliwapa pole wasichana hao na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kusema fikra, hisia na dua ziko pamoja nao.
Jussa aliwaomba polisi kuongeza doria ndani ya Mji Mkongwe ambao bado unabakia kuwa ndio mji mkuu wa Zanzibar na pia kituo kikuu cha harakati za kiuchumi ikiwemo biashara na utalii.
Aidha alisema muda umefika kwa mji Mkongwe kuwekewa kamera za usalama za kufuatilia nyenendo za watu hasa ikizingatiwa mji ndiko kwenye harakati nyingi zinazokusanya watu wengi.
Aliwataka wakaazi wa Mji Mkongwe na Zanzibar kwa ujumla kuwa makini na kufuatilia nyenendo zinazotia mashaka au zinazoashiria mwelekeo wa kufanya vitendo vya uhalifu.
Smz kama serekali imewashinda wajiuzulu wawapishe wengine, nijambo lakushangaza kuona nchi yenye watu miliono moja na nusu ina madarizen ya viongozi uhalifu wakikatili kama huu ikawa jambo la kawaida walianza kuwamwagia wenyeji, sasa wageni wetu walokuja kwa upendo kukuza elimu hapa visiwani. Hakuna muamsho hata mmjao anoweza kujitoea kw mchango wa elimu au maji kitendo hichi kama smz hawaja wakamata wahilifu wawajibike
ReplyDelete