Habari za Punde

Tuwape Elimu Watu wenye Ulemavu

Na Aboud Mahmoud

KATIKA jamii yetu ya Kitanzania tumezowea sana kusikia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwemo masuala ya kutopata elimu au mambo mengine muhimu.

Lakini pia katika jamii yetu mtu mwenye ulemavu tumezowea kumuweka ni mtu ambae hawezi kufanya jambo lolote katika jamii hii kutokana na ulemavu aliokuwa nao.

Lakini sio hivyo ni ukweli usiofichika kwamba lazima jamii ielewe kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kufanya mambo mengi yenye umuhimu kwa taifa kuliko wale wenye viungo kamili.

Kutokana na hilo,mwandishi wa makala hii alifanya utafiti wa kumtafuta mmoja wa watu wenye ulemavu ambae amekuwa mstari wa mbele katika kujiletea maendeleo yake binafsi na hata taifa kwa ujumla

Makala hii ilikutana na mwanadada Ruwaida Shaaban Khamis hapo nyumbani kwao Rahaleo, mwenye ulemavu wa macho ambae alimuelezea alipotoka alipofikia na matumaini yake ya hapo baaade.

Ruwaida amezaliwa Juni 26 mwaka 1989 akiwa ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano wawili wanawake na watatu wanaume.

Alisema kwaba tatizo la kutoona kwake alizaliwa nalo na wala hakukua na mtu yoyote kwenye familia yake ambae alikuwa na tatizo kama alilonalo yeye.

Mwaka 1996 Ruwaida alianza elimu yake ya msingi katika skuli ya Kisiwandui ambapo alisema darasa la kwanza hadi la pili alisoma katika madarasa maalum na baadae alichanganywa na wanafunzi wengine.

Ilipofika mwaka 2003 alichaguliwa kujiunga na skuli ya Sekondari ya Haile Selassie kuanzia kitado cha kwanza hadi cha sita ambapo kutokana na juhudi yake katika masomo alipofika kidato cha sita alipasi kwa kupata divisheni 3 .

Alisema kwamba mwaka 2010/2011 alijiunga na Chuo kikuu cha Zanzibar University kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu akisomea maswala ya sheria ambapo hivi sasa anaingia mwaka wa nne wa masomo.

Alisema kwamba fani ya sheria aliipenda tangu mdogo sana,lakini akiwa darasa la saba alitokea mtu mwenye ulemavu wa macho kutoka nchini Canada na alikuwa mwanasheria ndie aliempa moyo wa kujiunga na fani hiyo.

"Kwa kweli fani ya sheria nilikuwa naipenda sana tangu nikiwa mdogo,lakini nilipofika darasa la saba,alikuja mwanasheria kutoka Canada ambae anatatizo kama langu ndie alienipa moyo na mimi nijiunge na masomo haya,"alifahamisha.

Alifahamisha kwamba masomo yake ambayo husoma kwa kutumia Computer inayotumia sauti ambayo inamsaidia katika masomo yake ya kila siku.

Kuhusu changamoto alizokuwa akikabiliana nazo hapo awali,Ruwaida alisema wakati alipokuwa anaanza kusoma darasa la kwanza alikuwa akipata tabu sana kutokana na skuli ilikuwa mbali na yeyena hivyo kulazimika wazazi wake kupata wakati mgumu wa kumpeleka skuli mpaka pale alipozoeana na wenzake wakawa wanafatana nae.

"Hapo nilipokua naanza skuli ilikuwa napata tabu sana kwa sabbu skuli ni mbali na mimi peke yangu ilikuwa siwezi kwenda kwa hiyo wazazi wangu wakachukua juhudi ya kunipeleka skuli mpaka nilipozoeana na wenzangu nikawa nafatana nao,"alisema.

Changamoto nyengine alisema kwamba wakati anaomba kujiunga na masomo ya elimu ya juu alikuwa hakubaliki lakini sasahivi anakubalika na watu wote chuoni.

Lakini je kwa upande wa faida?

Ruwaida alisema kwamba kwake anaona anapata faida kubwa kwani familia yake kumpa mashirikiano ya hali ya juu ya kumpatia mahitaji mbali mbali ikiwemo elimu .

"Naamini kwamba kwa uwezo wa Mungu bila ya familia yangu kutonipa mashirikiano basi nisingeweza kufanikiwa na jambo lolote,mana wao ndo walionipatia elimu na mambo yote katika maisha yangu,"alifahamisha.

Mbali na hilo,lakini Ruwaida pia alisema kwamba anafarijika kwa kuwa yupo pamoja na wenzake na hawambagui wala kumdharau katika mambo mbali mbali pia kutokana na kujiunga na sehemu mbali mbali za kusoma ameweza kujulikana sana.

"Wenzangu wa chuoni na hata hapa nyumbani ndio wanaonifanya nijione kuwa mimi sina tatizo katika mwili wangu,kwani hawanibagui wala hawanidharau nipo nao kama kawaida,"alifahamisha.

Nilipotaka kujua kwamba je amepata elimu ya Quraan? alinijibu kuwa anafurahia kuwa amepata kukihifadhi kitabu cha Quraan na mbali ya hilo pia anazungumza lugha ya Kiingereza na kiarabu lakini sio sana.

Ruwaida ni Waziri wa Wanawake na mahitaji maalum huko chuoni kwao pia ana nafasi mbali mbali ikiwemo Mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Watu wasioona (ZANAB) na pia ni mjumbe wa jumuiya mbali mbali.

Nilipotaka kujua malengo ya baadae ya Ruwaida alisema kuwa malengo yake ya baadae ni kuwa wakili na sio jaji wala hakimu,kwani alisema kiwa wakili ataweza kushughulikia kwa undani zaidi kesi zinazowahusu walemavu ambazo humalizikia chini na hazifikishwi juu.

“Malengo yangu ya baade ni kuwa wakili ambae nitaweza kusaidia na kuzishughulikia kwa undani zaidi na hasa zile ambazo zinamalizikia chini tu hazifikishwi juu,”alisema.

Pia alisema kuwa matarajio yake ya baadae ni kuweza kufanya shughuli zake nyengine kwani akiwa jaji hatoweza kufanya shughuli zake nyengine na pia kujiendeleza zaidi kimasomo na kuwa na familia yake .

Hivyo Ruwaida alitoa ushauri kwa wazee wenye watoto wenye ulemavu kutokubali kuwaficha ndani na kuwapa uhuru wa kuwapatia elimu ambayo itaweza kuwasaidia baaade.

Alisema kwamba ipo haja kwa wazazi kuipokea hali hiyo kwa mikono miwili kwani hiyo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na haiwezi kukimbilika.

Ruwaida aliwashauri watu wenye ulemavu waachane na tabia ya kukata tamaa nao waige mifano kutoka kwa wenzao wengi walio nje ya nchi ambao hawajakubali kukata tamaa ya kubakia nyuma kila siku.

Pia mwanadada huyo msomi aliishauri Serikali kuhakikisha kwamba mradi wlaiouanzisha wa elimu mjumuisho waufikishe mpaka vijijini ili watoto wasipate usumbufu .

Aidha aliitaka Serikali kuwapatia vifaa watu wenye ulemavu ili wawezi kujifunza zaidi pamoja na kuwapatia mikopo wanafunzi wanaosoma kuanzia ngazi za cheti na diploma na sio kusubiri mpaka wafike chuo kikuu.

“Naiomba Serikali kuhakikisha kwamba elimu mjumuisho inafika mpaka vijijini ili kuwasaidia na waliokuwepo huko hawapati usumbufu na pia kuwapa mikopo wanafunzi wenye ulemavu kuanzia nafasi za cheti na diploma,”alifahamisha.

Kutokana na mambo mbali mbali ya Ruwaida ni uthibitisho tosha kwamba watu wenye ulemavu ni sawa sawa na watu ambao wapo wazima kwani mambo anayoyafanya yeye wapo wengi ambao hawana tatizo lolote na hawawezi kuyafanya.

Ni jambo la faraja kwa wazazi wa kijana huyo kutokana na bidii walioichukua ya kumsomesha mpaka hapa alipofikia bila ya kuvunjika moyo kwa kumpa ushirikiano wa hali na mali.

Hivyo kutokana na hayo Serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais ambayo ndio inayoshughulika na maswala hayo kumsaidia kijana huyo kutokana na bidii yake ya kutaka kujipatia maendele yeye na nchi kw aujumla

Aidha mbali na Serikali,hata kampuni,wafanyabiashara na taasisi mbali mbali zijitokeze kuwasaidia watu wenye ulemavu kwani wanaweza kujifunza na kuleta maendeleo makubwa katika nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.